WAKALA wa Vipimo Nchini (WMA) imetaka vipimo vya ujazo urefu na uzito wakati wa kupima bidhaa au kuhudumia wananchi lazima vihakikiwe kila baada ya miezi 12.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Kituo cha (WMA) kilichopo Misugusugu Wilayani Kibaha Mkoani Pwani Charles Mavunde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Mavunde amesema kuwa uhakiki huo ni takwa la kisheria ya vipimo sura 340 namba 19 ya mwaka 2002 inataka vipimo vinavyotumika kupima katika biashara au huduma nyingine za kijamii lazima vihakikiwe ndani ya muda huo.
Amesema kuwa sheria inatoa adhabu kwa mtu ambaye hata hakiki vifaa vinavyotumika katika kubebea au kupimia ambapo faini ni kati ya shilingi 100,000 hadi milioni 20 au kifungo jela miaka miwili.
"Kipimo chochote kinachopima kuhudumia wananchi kinatakiwa kufanyiwa uhakiki kila baada ya miezi 12 pia tunawapongeza wananchi kwa kuwa na mwamko kwenye uhakiki wa dira za maji kwani ni mkubwa," amesema Mavunde.
Amesema wanatarajia kuhakiki mita za maji zaidi ya 87,000 kufikia mwishoni wa mwezi Juni 2025 ili kutambua usahihi wake kabla ya kwenda kufungwa kwa wateja na wamefanya zoezi la uhakiki wa mita za umeme zaidi ya 5,500 za umeme mkubwa wa viwanda vya Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine ili kuona kama zipo sahihi kulingana na matumizi viwandani.
"Kwa upande wa dira za maji katika kipindi cha Julai hadi Mei mwaka huu tayari wamehakiki dira 57,997 huku wakiwa na uwezo wa kuhakiki dira 100,000 kwa mwaka
Naye Ofisa Vipimo Mkuu Gaudence Gaspery amesema kuwa hivi sasa wanahakiki dira za maji kwa kutumia mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kuhakiki dira 10 kwa wakati mmoja.
Gaspery amesema kuwa baada ya kuhakikiwa na kuonekana zinafaa kwa matumizi huwekewa rakili yenye rangi ya chungwa na ambazo zitagundulika zinahitaji kufanyiwa marekebisho hurekebishwa huku zile ambazo zitagundulika kwamba hazifai huteketezwa.
No comments:
Post a Comment