Thursday, May 29, 2025

MWANASHERIA MATATANI AKITUHUMIWA KUGHUSHI AKAUNTI YA KIJIJI NA KUJIPATIA FEDHA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 385 fedha za mauzo ya ardhi ambazo ziliwekwa kwenye akaunti ya kughushi ya mtu binafsi badala ya akaunti ya Kijiji cha Msufini Kidete Wilaya ya Mkuranga.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Domina Mukama akitoa taarifa ya Januari hadi Machi alisema kuwa fedha hizo zilikuwa ni asilimia 10 ya malipo baada ya Kijiji kuuza ardhi.

Mukama alisema kuwa mtu anayetuhumiwa kughushi akaunti hiyo ya Kijiji na kuingia kwenye akaunti yake binafsi ni mwanasheria wa kampuni ya Briliant Sanitary Ware Company Limited ambayo ilinunua eneo hilo.

"Fedha hizo ni asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya Kijiji baada ya mauzo ambapo zilipoingia mtu huyo alizitumia kwa matumizi binafsi lakini Takukuru walifanikiwa kuzirejesha fedha hizo ambapo kwa sasa kesi yake iko hatua ya uchunguzi,"alisema Mukama.

Aidha alisema kuwa fedha hizo baada ya kuzirejesha fedha hizo kwenye akaunti ya Kijiji hicho zimepangiwa matumizi ya kujenga madarasa mawili ya Shule ya Sekondari Mbezi Gogoni na madarasa mawili Shule ya Msingi Msufini.

"Katika hatua nyingine Takukuru imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 338 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 18 na utekelezaji wake unaridhisha,"alisema Mukama.

Alibainisha kuwa wamewafikia wananchi wa makundi mbalimbali ili waweze kuiunga Serikali mkono katika kuzuia vitendo ya rushwa kwa kupitia semina 67, mikutano ya hadhara 72, vipindi vya redio 5, uimarishaji klabu za wapinga rushwa 130.

"Tumejipanga Kuzuia na Kupambana na vitendo vya Rushwa katika uchaguzi Mkuu kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi kwa kuwafikia wadau wote,"alisema Mukama.

Aliongeza kuwa wanatoa elimu kwa wadau ambao ni vyama vya siasa, wasimamizi wa uchaguzi, wanahabari, wananchi na jamii nzima kwa ujumla ambapo anawaasa wananchi kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuwa salama na kuepuka migogoro yenye kuleta viashiria vyenye rushwa.

"Katika kipindi tajwa Ofisi ilifanya chambuzi za mifumo 14 ikiwa ni pamoja na eneo la makadirio ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya
Mji Kibaha, Mafia, kituo cha Utalii Kazimzumbwi katika chambuzi wa mfumo wa usambazaji maji uliofanyika kuna mapungufu yalibainika na hatua zilichukuliwa.

No comments:

Post a Comment