KUFUATIA mpango wa Halmashauri ya Mji Kibaha kulibomoa na kujenga upya soko la Loliondo liwe a kisasa uongozi wa soko hilo umeridhia lakini umetoa maombi kwa Halmashauri hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwenyekiti wa soko hilo lililopo Kata ya Tangini Mohamed Mnembwe alisema kuwa wamekubali kubomolewa soko hilo ikiwa ni sehemu ya kuleta maendeleo.
Mnembwe alisema kuwa wametoa maombi yao kwa Halmashauri ya kuongezewa muda wa notisi kutoka miezi mitatu hadi sita, bei ya gharama za kodi kwa mita za mraba zibaki zile zile mara soko litakapokamilika.
"Kuwe na mkataba kati ya Halmashauri na soko juu ya wao kupewa kipaumbele cha kurudi kufanya biashara sokoni hapo bila ya masharti, ukubwa wa fremu ubaki uleule na waongezewe muda wa malipo nafuu hadi mwaka 2042 kwani fremu zitazobomolewa walijenga wao wenyewe kwa gharama zao,"alisema Mnembwe.
Alisema kuwa wanaomba makubaliano waliyoingia juu ya uboreshaji wa soko hilo yasibadilike kwani wao wanachotaka ni maendeleo na kuboresha mazingira ya biashara.
"Tunaunga mkono jitihada za serikali hivyo yale tuliyokubaliana na Halmashauri yawe ni yale yale na kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara waliopo na nafasi zikabaki wapewe wafanyabiashara wapya,"alisema Mnembwe.
Aidha alisema kuwa ujenzi huo utakuwa ni wa miezi 15 ambapo kwa kipindi hicho watahamishia biashara zao kwenye eneo jirani panapotumika kuuza mitumba na watajenga mabanda ya muda.
Soko hilo lina fremu 338 kati ya hizo zinazofanya kazi ni 155, mapaa sita na vibanda 155 ambapo kuna wafanyabiashara zaidi 800 wakiwa wanauza bidhaa za aina tofauti tofauti.
No comments:
Post a Comment