VYOMBO vya Habari nchini vimetakiwa kutoa taarifa za vyama vyote vya siasa kwenye kampeni wakati wa uchaguzi wa mwaka huu ili wananchi waweze kujua sera za vyama na kuchagua viongozi bora.
Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Asasi ya Maendeleo ya Vijana (YPC) Israel Ilunde alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Ilunde alisema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutoa elimu ambayo itasaidia kujua sera za vyama vyote bila ya kupendelea baadhi ya vyama.
"Vyombo vya habari vitoe taarifa za vyama vyote kwa usawa bila ya upendeleo hata kwa vyama vidogo navyo vipate nafasi ili vieleze sera zao na wananchi wachague wagombea ambao wataona wanawafaa,"alisema Ilunde.
Alisema kuwa wananchi wakisikia sera za vyama vyote watakuwa na maamuzi mazuri ya kuchagua viongozi ambao wataona wana sera nzuri na watakuwa wamechagua wakiwa na uhakika wa wanao wachagua wana sera nzuri.
"Pia vyama vya siasa nchini vinatakiwa vitoe kauli za kulinda amani iliyopo na kuachana na kauli za chuki na uchochezi ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Aidha alisema kuwa amani ni tunu ya Taifa ambayo inabidi ilindwe ambapo kauli zisizo nzuri husababisha amani kutoweka na wananchi kutoelewana.
"Nayo Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ihakikishe inakutana na wadau wa siasa mara kwa mara ili kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi ambapo itasaidia kuondoa malalamiko wakati wa uchaguzi,"alisema Ilunde.
Aliongeza kuwa wananchi kwa maeneo zoezi la uhakiki wapiga kura linafanyika wajitokeze kuangalia taarifa zao na ikifika muda wa kupiga kura wajitokeze kwa wingi kwa wale wenye sifa.
"Kwa makundi ya vijana wanawake na watu wenye ulemavu wanaotaka kuwania nafasi za uongozi wajitokeze kuwania nafasi hizo kupitia vyama vyao na vyama vitoe nafasi,"alisema Ilunde.
No comments:
Post a Comment