Saturday, May 3, 2025

KECA YAUNGA MKONO SERIKALI UHIFADHI MAZINGIRA NA UFUGAJI NYUKI

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Kibaha Environmental Conservation Action (KECA) limedhamiria kuunga mkono jitihada za serikali kwa uhifadhi wa mazingira na kukuza uchumi kupitia ufugaji wa nyuki.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi wa (KECA) ambalo linajihusisha na utoaji elimu ya ufugaji nyuki na utunzaji wa mazingira Ibrahim Mkwiru wakati wa uzinduzi wa jengo la ofisi yao.

Mkwiru alisema kuwa nia yao ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi wa mazingira na kukuza uchumi wa wananchi kupitia ufugaji wa nyuki ili kuongeza kipato kwa wananchi.

"Tunaiomba Serikali kutupa kibali cha kupanda miti ya mianzi katika maeneo ya wazi karibu na chanzo cha Mto Ruvu ili kusaidia kuhifadhi mazingira na kuchochea maendeleo ya kijamii kupitia njia ya uhifadhi wa mazingira,"alisema Mkwiru.

Kwa upande wake Ofisa Tarafa ya Kibaha Catherine Njau alisema kuwa Serikali inaendelea na dhamira yake ya dhati ya kuunga mkono juhudi za wawekezaji katika sekta ya ufugaji nyuki ili kuhakikisha wafugaji wadogo waliopo vijijini wananufaika kiuchumi na kielimu. 

Njau alosema kuwa kwa muda mrefu wafugaji wa nyuki wanaoishi pembezoni mwa miji wamekuwa wakikosa elimu sahihi ya ufugaji wa kisasa na pia kukosa masoko ya uhakika kwa bidhaa zao.

Alilipongeza shirika la KECA kuwa kama daraja muhimu kwa wafugaji wa nyuki kupata elimu ya kitaalamu na fursa za kibiashara kwa wafugaji ili waweze kupata masoko makubwa.

"Nawasisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kitaalamu kabla ya kupanda mianzi kwenye maeneo ya vyanzo vya maji,huku akisema baadhi ya miti ina uwezo wa kutumia maji mengi na hivyo inaweza kuhatarisha uhai wa vyanzo vya maji kama mito,"alisema Njau.

Naye Mjumbe wa Bodi ya KECA Edwin Shunda aliwahimiza wananchi na wadau wa mazingira kujitokeza kwa wingi kujifunza mbinu za ujasiriamali na ufugaji wa nyuki wa kisasa.

No comments:

Post a Comment