Wednesday, June 25, 2025

MATUMLA PROMOTION KUINUA VIPAJI VYA NGUMI KIBAHA

MATUMLA Promotion ya Kibaha imeandaa pambano la ngumi kati ya Abdully Said au Dully Bwengo na Rashid Hassan au Makali litakalopigwa kwenye baa ya UEFA Kongowe Kibaha Juni 28 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na pambano hilo ambalo litasindikizwa na mapambano mengine matano Mkurugenzi wa Matumla Promotion Abuu Matumla amesema kuwa maandalizi ya awali yamekamilika.

Matumla amesema kuwa maandalizi yakiwemo ya kuwalipa fedha za awali yameshafanyika na mabondia hao watakamilishiwa fedha zao baada ya pambano hilo kukamilika.

"Taratibu za awali zimekamilika ikiwa ni pamoja na malipo ya awali kwa mabondia, vibali na ulinzi vyote viko tayari kinachosubiriwa ni siku ya pambano hilo,"amesema Matumla.

Alisema kuwa malengo ya kuandaa mapambano hayo ni kuhamasisha mchezo huo kwa vijana wa Kibaha kwani mchezo huo ni ajira na kujenga afya bora na kuwaondoa vijana kwenye vitendo hatarishi.

"Tunataka tuinue mchezo wa ngumi Kibaha ambapo pia kutakuwa na pambano la wanawake ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha wanawake nao washiriki mchezo huo kwani hata wao wanauwezo wa kushiriki mchezo huo,"amesema Matumla.

Aidha alisema kuwa mbali ya mapambano hayo pia kutakuwa na burudani za muziki zikiongozwa na mkali wa Singeli Yuda Msaliti na waimbaji wengine wakali wa miondoko hiyo ya singeli.

"Nawaomba wapenzi wa mchezo wa ngumi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji vya vijana wao ili kuwapa hamasa wapende mchezo huo ambao umekuwa ukipendwa na wengi,"amesema Matumla.

No comments:

Post a Comment