SERIKALI imesema kuwa elimu ni nguzo ya kuwalinda watoto na ukatili ndoa na mimba za utotoni na kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza haki ya msingi ya mtoto kupata elimu.
Hayo yamesemwa na Madina Mussa ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha wakati wa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika iliyoandaliwa na DMI Mission Tanzania.
Mussa amesema kuwa ili kutekeleza mazingira rafiki kwa watoto waweze kupata haki hiyo ya msingi imejenga miundombinu mizuri ya watoto kujisomea.
"Katika kukabiliana na ukatili na ndoa za utotoni wazazi na walezi lazima washirikiane na serikali kuhakikisha haki za msingi za mtoto zinalindwa ikiwa ni pamoja na elimu, kumlinda na ukatili na kuishi katika mazingira mazuri kwani haki za mtoto zinaanzia nyumbani,"amesema Madina.
Awali Mkurugenzi wa DMI Mission Tanzania Sister Fathima Jacintha Ran amesema kuwa dhima ya siku hiyo ni Kupanga bajeti na kuweka bajeti kwa haki za watoto.
Ran amesema kuwa lengo ni kuhakikisha ustawi, elimu, na hatma njema za watoto ikiwa ni kukumbusha wajibu wa pamoja kuhakikisha watoto wa Afrika wanapata haki za msingi za elimu bora, huduma za afya, ulinzi na fursa ya kukua.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii kitengo cha watoto Halmashauri ya Mji Kibaha Hanifa Mruma amesema kuwa mradi ulioanzishwa na shirika hilo wa kupambana na mimba za utotoni ni mzuri na utasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa upande wake moja ya wanufaika kwenye mradi huo wa Klabu za Wanawake Vijana Chiku Hamis amesema kuwa wanalishukuru shirika hilo kwa kuwapatia vifaa kwa ajili ya kutengeneza batiki na sabuni kwa ajili ya mafunzo ya utengenezaji vitu hivyo.
Mradi huo wa kupunguza mimba za utotoni unatekelezwa kwenye Kata tatu za Pangani, Tumbi na Kongowe.
No comments:
Post a Comment