Friday, June 2, 2023

AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA KWA KUUA WATOTO WAKE WATATU KWA KUWANYWESHA SUMU

MKULIMA na mkazi wa Ditere Wilaya ya Kipolisi Chalinze Mkoani Pwani Salehe Masokola amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua watoto wake watatu kwa kuwanywesha sumu.

Watoto hao watatu waliouwawa kwa kunyweshwa sumu ni Sheila Masokola (8), Nurdin Masokola (6) na Sabrati Masokola miezi (6).

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani (ACP) Muhudhwari Msuya alisema kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Novemba 26 mwaka 2018 baada ya kutoelewana na mke wake.

Msuya alisema kuwa baada ya kutengana mkewe aliondoka na watoto ambapo aliwafuata watoto wake kwa mama yao na kurudi nao nyumbani kwake ambapo alitekeleza mauaji hayo baada ya mkewe kugoma kurudi nyumbani ili waendelee kuishi.

Alisema kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo alikamatwa na kesi kufunguliwa kwenye kituo cha polisi Chalinze ambapo upelelezi ulifanyika na kupatikana na hatia na kuhukumiwa hadi kufa hukumu na Jaji wa Mahakama Kuu Elizabeth Mkwizu.

Thursday, June 1, 2023

KONGAMANO KUWAKUTANISHA WALIMU WANAWAKE NA UJASURIAMALI

 

WALIMU wanawake 300 kutoka Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani wanatarajia kukutana kwenye Kongamano la ujasiriamali ambalo litafanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Mwenyekiti wa CWT kitengo cha wanawake Rose Nyambweta alisema kuwa wameamua kuandaa kongamano hilo ili walimu hao wajifunze masuala ya ujasiriamali.


Nyambweta alisema kuwa kwenye kongamano hilo kutakuwa na vitu mbalimbali ambavyo walimu hao watafundishwa masomo ya ujasiriamali na masuala ya fedha ikiwa ni pamoja na kujiwekea akiba na ukopaji wa fedha usio na madhara.

"Kongamano hilo litakuwa na wataalamu wa mafunzo hayo ya ujasiriamali ikiwemo wa kutengeneza batiki, sabuni za vipande, vikoi na sabuni za maji ni vitu vya kijasiriamali ili wauze waongeze kipato chao,"alisema Nyambweta.

Kwa upande wake Katibu wa CWT Wilaya ya Kibaha Kitengo cha Wanawake Florence Ambonisye alisema kuwa kutokana na walimu kuwa na mahitaji makubwa wamejikuta wakiingia kwenye mikopo umiza maarufu kama kausha damu na mingineyo lakini ujadiriamali unaweza ukawaondoa kwenye mikopo hiyo inayowaumiza.

Naye Katibu wa CWT Wilaya ya Kibaha John Kigongo ambaye pia ni mjumbe alisema kuwa mara baada ya mafunzo hayo walimu hao wanawake wataunda vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitawezeshwa ili vifanye uzalishaji.

Wednesday, May 31, 2023

WADAU WA MAENDELEO WATAKIWA KUTUMIA TAKWIMU ZA SENSA

KAMISAA wa Sensa Tanzania Bara Anne Makinda amewataka wadau wa maendeleo nchini kutumia takwimu za sensa ambazo zimefanywa kisayansi ili kutumia rasilimali kikamilifu.

Makinda aliyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa mafunzo ya sensa kwa kamati ya mkoa na viongozi wa ngazi ya mkoa.

Alisema kuwa kwa kutumia takwimu hizo itasaidia wakati wa kupanga bajeti hivyo kuweka matumizi mazuri ya rasilimali ambapo viongozi mbalimbali wanapaswa kutumia matokeo ya sensa hiyo ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Naye Balozi Mohamed Haji Hamza Kamisaa wa Sensa Tanzania Zanzibar alisema kuwa hadi Juni mwakani machapisho 200 yatatolewa ili kuwajengea watu uelewa juu ya ripoti ya sensa.

Mwakilishi wa mtakwimu mkuu Adela Temba alisema kuwa matokeo ya sensa hutolewa kwa awamu ambapo ripoti kuu nne zimeshazinduliwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kuwa takwimu za sensa ni muhimu sana katika matumizi ya rasilimali.


Sunday, May 28, 2023

RC KUNENGE KUIPA KIPAUMBELE MICHEZO

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Mkoa utatoa kipaumbele kwenye michezo kwani ni moja ya ajira zenye utajiri mkubwa duniani.

Kunenge ameyasema hayo wakati akifunga michezo ya Umoja wa Michezo Taaluma Sanaa kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) mkoa wa Pwani kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Tumbi.

Alisema kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa duniani wanatokana na michezo hivyo ni sehemu ya kutoa ajira kwa watu wakiwemo vijana.

"Mkoa utaunga mkono kwa kuifanya sekta ya michezo kuwa kipaumbele kwa kutoa fursa mbalimbali zinazohusiana na michezo,"alisema Kunenge.

Aidha alisema kuwa ili nchi iweze kuwa na vipaji na wachezaji wazuri lazima michezo ianzie chini kabisa kama nchi ilivyoweka utaratibu wa michezo hiyo kwani washiriki ni watoto wadogo hivyo kuwajengea kujiamini.

"Michezo inakuza uchumi pia ni ajira na ni afya hivyo lazima iwezeshwe kwa kuwajengea vijana mazingira mazuri ya kuendeleza vipaji vyao,"alisema Kunenge.

Alisema kuwa michezo ya mwaka huu imebeba kauli mbiu ya Miundombinu ya elimu na taaluma nchini ni chachu ya maendeleo ya sanaa na Michezo. 

Aliwataka wanamichezo hao kudumisha nidhamu ili kuuletea mkoa ushindi.Jumla ya wanamichezo kutoka Halmashauri tisa zilichuana kwenye michezo mbalimbali. 

Friday, May 26, 2023

DK SAMIA AGAWA ARDHI HEKARI 5,520 KWA WANANCHI

Hayo yamesemwa leo Mei, 26 2023 na Mhe David Silinde (Mb.) Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakati wa makabidhiano ya ardhi  iliyokuwa sehemu ya Ranchi ya Ruvu kwenda kwa Wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo na Kibaha ambapo pande zote zimeridhia.

Ameeleza uamuzi huo wa  Serikali ni kuwawezesha Wananchi kupata Ardhi kwa ajili ya Shughuli za kilimo, Mifugo na shughuli zingine za kijamii.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Ranchi ya NARCO Ruvu ukishuhudiwa na Viongozi wa Wilaya,Tarafa, Kata, Vijiji na Viongozi wa Wakulima na Wafugaji na wawakilishi wa Wananchi kutoka Vijiji 10. 

Akipongeza uamuzi huo Mhe Kunenge Mkuu wa Mkoa wa Pwani  amewaagiza Viongozi wa Mkoa na Wilaya kutimiza wajibu wao wa kusimamia kupanga matumizi ya Ardhi hiyo na kuwataka Wananchi kuheshimu Sheria na kwamba wasivamie tena eneo hilo la Serikali.

MIAKA 30 YA MISA TANZANIA


Na Wellu Mtaki, Dodoma

MSEMAJI  Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amefungua Maadhimisho ya Miaka 30 ya Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara Tawi la Tanzania (MISA Tanzania) na akiwasisitiza waandishi wa habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.

Msigwa amesisitiza hilo leo Mei 25,2023 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Naibu waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekonolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya MISA.

Amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya vyombo vya habari huku akisisitiza kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani hakuna chombo kilichofungiwa na vilivyokuwa vimefungiwa vimefunguliwa.

Aidha amesema katika kipindi hiki mafunzo au semina kwa waandishi zinahitajika hivyo kuiomba Misa Tanzania na wadau wengine kuwapatia mafunzo mbalimbali waandishi wa habari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Salome Kitomari amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwatumikia Watanzania, lakini zaidi kwa namna amechukua hatua kadhaa zilizowezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuondoa vikwazo vingi.

Kitomari amesema MISA Tanzania imepita kwenye safari ya miaka 30 yenye milima na mabonde na kutokana na mambo yote hayo ameupongeza uongozi, sekretarieti na wanachama wa MISA Tanzania kwa kushikamana mpaka kufikia hatua hiyo.

Sanjari na hayo ameongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na kutoa mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa waandishi wa habari, Kuwezesha uanzishwaji wa vyombo vingine vya habari zikiwamo Radio za Kijamii na kufanya marekebisho kwenye sheria mbalimbali tangu Sheria ya Magazeti, Sheria ya Huduma za Habari, Sheria ya Haki ya Taarifa na nyinginezo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Misa Tanzania, Elizabeth Riziki amesema Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara,Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 baada ya kikao cha wanahabari waliokutana Windhoek, Namibia kujadili mambo mbalimbali yaliyokuwa yanaukabili Ukanda wa Nchi za Kusini.

MISA ina matawi tisa katika nchi za Zambia, Msumbiji, Malawi, Lesotho, Botswana, Namibia, Angola, Tanzania na Zimbabwe ambako ndiyo makao makuu ya matawi yote.

Amefafanua kuwa katika mkutano huo wa siku mbili wadau watajadiliana kuhusu kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na namna ambavyo umma unahusishwa kwenye uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa lakini pia watajadili changamoto zilizopo kwenye sekta ya habari na kuweka mkakati wa kuzitatua ikiwamo namna ya kuboresha maisha ya waandishi wa habari.

Pia amesema Majadiliano hayo yana lengo la kuongeza ukaribu na ushirikiano baina ya waandishi wa habari na Jamii, pia kuibua hoja zitakazowaleta pamoja Jamii na waandishi wa habari katika kuwa na mpango kazi wa utekelezaji ili kuhakikisha kila mwanajamii anatumia vizuri nafasi ya uhuru wa kujieleza kupitia vyombo vya habari kwaajili ya maendeleo endelevu.

Ikumbukwe kuwa Misa Tanzania inaadhimisha miaka 30 huku kauli mbiu ikiwa ni "Uhuru wa Kujieleza Msingi wa Haki Zote kwa Maendeleo Endelevu.

Thursday, May 25, 2023

SHULE ZA SEKONDARI TUMBI NA MWANALUGALI ZAPOKEA MILIONI 300

SHULE ya Sekondari ya Tumbi imepokea kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule.

Aidha Shule ya Sekondari ya Mwanalugali imepokea kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula.