MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Mkoa utatoa kipaumbele kwenye michezo kwani ni moja ya ajira zenye utajiri mkubwa duniani.
Kunenge ameyasema hayo wakati akifunga michezo ya Umoja wa Michezo Taaluma Sanaa kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) mkoa wa Pwani kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Tumbi.
Alisema kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa duniani wanatokana na michezo hivyo ni sehemu ya kutoa ajira kwa watu wakiwemo vijana.
"Mkoa utaunga mkono kwa kuifanya sekta ya michezo kuwa kipaumbele kwa kutoa fursa mbalimbali zinazohusiana na michezo,"alisema Kunenge.
Aidha alisema kuwa ili nchi iweze kuwa na vipaji na wachezaji wazuri lazima michezo ianzie chini kabisa kama nchi ilivyoweka utaratibu wa michezo hiyo kwani washiriki ni watoto wadogo hivyo kuwajengea kujiamini.
"Michezo inakuza uchumi pia ni ajira na ni afya hivyo lazima iwezeshwe kwa kuwajengea vijana mazingira mazuri ya kuendeleza vipaji vyao,"alisema Kunenge.
Alisema kuwa michezo ya mwaka huu imebeba kauli mbiu ya Miundombinu ya elimu na taaluma nchini ni chachu ya maendeleo ya sanaa na Michezo.
Aliwataka wanamichezo hao kudumisha nidhamu ili kuuletea mkoa ushindi.Jumla ya wanamichezo kutoka Halmashauri tisa zilichuana kwenye michezo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment