Thursday, May 18, 2023

WIZARA YA AFYA YAWEKA JITIHADA KUDHIBITI UGONJWA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema  pamoja na kuimarisha huduma za tiba hapa nchini, serikali imejipanga kuweka jitihada za kipekee ili kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa shinikizo la juu la damu na magonjwa yasiyoambukiza.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Mei 17,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya shinikizo la damu Duniani.

Pia amekumbusha umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha na kuhimiza wananchi kufanyaji wa mazoezi, kuepuka tabia bwete, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kupunguza matumizi ya vilevi, kuzingatia ulaji unaofaa wa mlo kamili wenye mboga mboga na matunda ya kutosha ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.

Aidha, amesema kuwa takwimu kutoka kwenye mfumo wa ukusanyaji taarifa za Afya (DHIS2) zinaonesha kuwa jumla ya wagonjwa milioni 2.5 walitibiwa magonjwa yasiyoambukizwa kwenye vituo vya Afya nchini kwa mwaka 2017.

Waziri Ummy amesema kati yao, ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ndio uliongoza miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ambapo waliongezeka kutoka wagonjwa 688,901 kwa mwaka 2017, hadi kufikia wagonjwa milioni 1.3 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la 95.4% katika kipindi hicho.

Amesema katika uchunguzi uliofanywa katika jamii kwenye mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Iringa na Dar es Salaam takwimu zinaonyesha watu 3-4 kati ya 10 wana shinikizo la juu la damu. 

Shinikizo la juu la damu ni ugonjwa unaosababishwa na nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa kuwa kubwa kuliko kawaida kwa muda mrefu na ongezeko hilo huulazimu moyo kufanya kazi kupita kiasi ili uweze kusukuma damu katika mishipa kwa kiwango kilekile kinachohitajika mwilini.

No comments:

Post a Comment