Thursday, May 18, 2023

MWENGE WAZINDUA MIRADI KIBAHA

KIONGOZI wa mbio za Mwenge Kitaifa Abdala Shaibu Kaim amewataka Watanzania kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi ambayo kwa asilimia 95 yanatokana na uharibifu wa mazngira.

Aidha aliwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kula kwa mpangilio na kufanya mazoezi ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha wakati wa kupokea Mwenge wa uhuru ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

 Kaim alisema kuwa uharibifu huo wa mazingira unasababisha kushusha uchumi wa nchi kutokana na athari hizo hivyo kuna haja ya Watanzania kusimamia maingira ili yasiharibiwe.

"Tuhakikishe tunalinda mazingira yetu ili kukabiliana na athari hizo ambazo zinaleta changamoto za kimaendeleo,"alisema Kaim.

Alisema kuwa mazingira ni uhai hivyo mazingira  yanapaswa kulindwa kwa nguvu zote ili maisha yaendelee bila ya changamoto ambazo zimesababisha hali ya hewa kuwa mbaya.

Aliongeza kuwa ujumbe wa mwaka huu unasema kuwa Mabadiliko Tabianchi Hifadhi ya Mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji na kauli mbiu tunza mazingira okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na ustawi wa uchumi wa Taifa.

"Tuendelee kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kula vyakula kwa mpangilio ambavyo vinashauriwa na wataalamu na kuacha ulaji usio na mpangilio na kufanya mazoezi angalau kwa nusu saa,"alisema Kaim.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Simon John alisema kuwa Mwenge huo wa uhuru ulitembelea jumla ya miradi 12 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.9.

John alisema kuwa fedha za miradi kati ya hizo milioni 520.2 ni mchango kutoka Halmashauri na milioni 683.7 ni kutoka serikali kuu na bilioni 2.4 ni michango ya wananchi.

Alisema kuwa fedha nyingine ni kutoka kwa wahisani ambapo ni kiasi cha shilingi milioni 293.3 na michango ya mwenge iliyoelekezwa katika miradi ya maendeleo ni shilingi milioni 2.5.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment