Na John Gagarini, Chalinze
MBUNGE Mteule wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amesema kuwa hana chuki kwa wale ambao hawakumpigia kura kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu kwani hizo ni changamoto za uchaguzi.
Aliyasema hayo jana kwenye uwanja wa Miembe Saba Chalinze wilayani Bagamoyo wakati wa mkutano wa hadhara wa kuwashukuru Wanachalinze kwa kumchagua kuwa mbunge kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili.
Ridhiwani alisema kuwa licha ya baadhi ya maeneo kutompigia kura za kumchagua kuwa mbunge lakini atawatumikia wananchi wote bila ya kujali kama walimpigia kura au la kwani kila mtu ana haki ya kumpigia kura mgombea yoyote anayempenda.
“Nawashukuru wananchi wote walionipigia kura na hata wale ambao hawakunipigia kura kwani hiyo ndiyo demokrasia nitahakikisha nawahudumia wananchi wote bila ya kuwabagua nitahakikisha napeleka maendeleo kwa watu wote wa jimbo hili,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa kutopigiwa kura kwa wingi siyo sababu ya kuwagawa wananchi kwani hizo ni changamoto za uchaguzi ambao unakuwa na mambo yake ambapo baadhi ya maeneo walipiga kura kwa kuzingatia ukabila.
“Sitakuwa na chuki wala hasira kwa wale ambao hawakunipigia kura nitashirikiana nao katika suala la maendeleo ili kuhakikisha jimbo letu linakuw ana maendendeleo na wananchi wanaboresha maisha yao ili yasonge mbele,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema kuwa atahakikisha Mji wa Chalinze ambao umekuwa Halmashauri ya Mji Mdogo unajengwa kwa kuwekewa huduma muhimu ili wananchi waweze kuboresha biahara zao hasa ikizingatiwa kuwa mji huo ni wa kibiashara.
“Moja ya mambo nitakayo yafanya ni kufanya Chalinze kuwa makao makuu ya Halmashauri hiyo na baadaye kuwa wilaya kwani mchakato unaendelea na tunaamini baada ya muda tutapewa wilaya hivyo tutaweza kujitegemea na kujiimarisha kiuchumi,” alisema Ridhiwani.
Alibainisha kuwa wananchi wasiwe na wasi wasi kwani kukichagua Chama Cha Mapanduzi CCM ni kuchagua maendeleo hivyo wasubiri kuona jinsi serikali mpya itakavyofanya kazi kwani kwao ni kazi tu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Chalinze Nasa Karama alisema kuwa mbunge huyo ameonyesha uwezo mkubwa kwani kwa kipindi alichochaguliwa cha mwaka mmoja na miezi mitatu ameweza kufanya mambo makubwa ambapo alitumia ziadi ya shilingi bilioni moja na zaidi kwa ajali ya miradi ya maendeleo.
Mwisho.
Ridhiwani Kikwete |