Friday, December 6, 2024

MAFIA WALILIA BOTI ZA MWENDOKASI


WANANCHI wa Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani wameiomba Serikali kuwapatia huduma ya boti zinzokwenda haraka badala ya kutumia boti ambazo hutumia masaa mengi baharini ambapo kwa sasa usafiri wa baharini umerahisishwa kama ilivyo kwa wasafiri wanaoenda Zanzibar.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafia Juma Ally kwenye kikao cha bodi ya barabara ya Mkoa wa Pwani kilichofanyika Mjini Kibaha.

Ally lisema kuwa wanaishukuru serikali kuwapatia boti kwenda Mafia lakini boti hiyo hutumia masaa mengi ambapo ni kati ya masaa sita au saba tofauti na boti zinazoenda Zanzibar ambazo hutumia nusu ya masaa hayo.

“Usafiri tunaotumia unasaidia lakini ungeboreshwa kwa kupata boti ambazo zinatumia injini badala ya hizoi ambazo zinatumia kasi ili tusafiri kwa haraka tofauti na ilivyosasa,”alisema Ally.

Alisema kuwa boti hizo za sasa zinatumia pangaboi lakini tunashauri tupatiwe zile ambazo ni jeti ambazo mwendo wake ni wa kasi.

“Tukipata boti za mwendo kasi hata watalii wataongezeka lakini kwa sasa wtaalii ni wachache kwani tunapata watalii 10,000 lakini usafiri huo ukipatikana wataongezeka na tutakuwa na watalii wengi hivyo kuongeza mapato ya Halmashauri yetu,”alisema Ally.

Aidha alisema kuwa kutokana na kutokuwa na boti hizo za mwendokasi kabla ya kufanya safari lazima kuwe na maji mengi jambo ambalo ni changamoto kubwa lakini ingekuwa boti za kasi zingefanya safari tu bila ya kusubiri maji kuwa mengi.

“Ombi letu lingine tunaomba Bandari ya Kisiju Wilayani Mkuranga iboreshwe ili itumika kwani kula ni rahisi tofauti na Bandari ya Nyamisati iliyopo Wilayani Kibiti hilo nalo tunaomba lifanyiwe kazi kikubwa ni kurahisisha usafiri wa wakazi wa Mafia,”alisema Ally.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa pwani akitoa ushauri alisema kuwa jambo kubwa ni kuangalia maslahi mapana ya wananchi hivyo miradi mbalimbali izingatie vipaumbele kutokana na maeneo na vitakavyoendana na vipaumbele vya Rais.

Kunenge alisema kuwa wajumbe wanapaswa kuangalia vipaumbele kwa uhalisia kwani fedha ni ndogo hasa ikizingatiwa nchi ilfanya uchaguzi ambao umetumia gharama kubwa hivyo kuwe na vipaumbele katika utekelezeji wa miradi.


TARURA PWANI

Thursday, December 5, 2024

*LYDENGE AZURU GEREZA LA KIGONGONI* 


Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Sophia Lydenge amewaongoza askari wa kike toka Wilaya hiyo kutoa msaada kwa wafungwa wanawake wanaotumikia adhabu ya kifungo kwa makosa mbalimbali kwenye gereza la Kilimo Kigongoni Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani. 

Lydenge ameeleza wakiwa  kwenye maadhimisho ya kupinga siku 16 za ukatili wa wanawake na wasichana,  wana mtandao wa Polisi wanawake Wilaya ya Kipolisi Chalinze waliona wafike kwenye gereza la Kigongoni ili kutoa msaada huo kwa wanawake wanaotumikia adhabu ya kifungo wakiwa na imani kuwa watabadilika kimatendo na kuwa mfano wa kuigwa watakapokuwa wamemaliza kutumikia adhabu zao. 

Miongoni mwa vitu vilivyokabidhiwa leo ikiwa ni mwendelezo wa kusaidia makundi yenye uhitaji kwenye Jamii ni pamoja na Cherehani moja, mafuta ya kupaka, taulo za kike pamoja na sabuni za kufulia na kuogea.

Aidha, Lydenge ameomba uongozi wa gereza kupokea Cherehani hiyo na ikatumike kwenye kuwafundisha wanawake waliopo gerezani ili wakitoka wawe na ujuzi wa kazi ya kufanya.

Akipokea msaada huo Mrakibu Msaidizi wa Magereza Kaziro Ambros kwa niaba ya Mkuu wa gereza hilo amewashuku mtandao mtandao wa Polisi wanawake Wilaya ya Kipolisi Chalinze na kuahidi Cherehani iliyopokewa itatumika kwa lengo kusudiwa kwa kutumika kama nyenzo ya kufundishia ushonaji kwa wafungwa wanawake ili kuweza kuwajenge uwezo kwenye eneo la ushonaji.

Monday, December 2, 2024

MAONYESHO YA WIKI YA UWEKEZAJI NA BIASHARA PWANI KUFANYIKA MAILI MOJA KIBAHA KUANZIA DESEMBA 16 HADI 20 MWAKA HUU

JUMLA ya watu 25,000 wanatarajiwa kuhudhuria maonyesho ya wiki ya Uwekezaji na Biashara yatakayoshirikisha washiriki 550 yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 16 hadi 20 mwaka huu.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Kunenge amesema kuwa maonyesho hayo yatafunguliwa Desemba 17 na yatafanyika kwenye viwanja vya iliyokuwa stendi ya zamani ya Maili Moja Kibaha.

"Maonyesho hayo ni ya nne kufanyika ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2018, 2019, 2022 na mwaka huu ambapo watu watatoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa wakati wa maonyesho watu watakaohudhuria watapata fursa za kujifunza, kuona fursa zilizopo, kuona teknolojia gani zinatumika na kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika Biashara na kujipatia bidhaa.

Ameongeza kuwa mkoa umejipanga vizuri hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa una viwanda 1,553 na tangu Rais aingie madarakani viwanda vikubwa ni 78.

Friday, November 29, 2024

WENYEVITI WAAPISHWA WATAKIWA WASIUZE ARDHI


WENYEVITI wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa hivi karibuni kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa wasijihusishe na uuzaji ardhi ili kuepukana na migogoro ya ardhi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa wakati wa kuapishwa kwa wenyeviti hao pamoja na wajumbe wa Serikali za Mitaa kwenye Halmashauri hiyo.

Shemwelekwa alisema kuwa wenyeviti hao waachane na masuala ya uuzaji ardhi kwani inayohusika ni Halmashauri kwani baadhi yao walikuwa wakijihusisha na uuzaji ardhi.

"Msijihusishe na masuala ya uuzaji ardhi pia itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi hivyo wao wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo,"alisema Shemwelekwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mussa Ndomba alisema kuwa wenyeviti wasifanye vita na watendaji wa mitaa kama kuna jambo waangalie namna ya kutatua.

Ndomba alisema kuwa wale ni wataalamu wasigombane nao kwani hawatafanya kazi vizuri na wanaweza kuwakwamisha kwani wanambinu nyingi wanaweza kuwakwamisha kwenye majukumu yao hivyo washirikiane nao na kama kuna changamoto wakae nao chini ili kutatua na kurekebishana.

"Masuala ya mihuri nimelisikia wananchi wapate huduma bure bila ya gharama na kuhudumiwa haambiwi toa fedha sijui ya nini anatakiwa apate huduma bora na kwa wakati,"alisema Ndomba.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa jukumu lao kubwa kurudisha deni kwa wananchi ambao wamewakopesha kura walizowapigia na wanatakiwa kuwatumikia na wasinunue bali wapewe huduma bure.

Koka alisema kuwa wanapaswa kuwatumikia na kuwashirikisha kwenye vikao pia waitishe mikutano na kuwapatia mrejesho wa masuala mbalimbali na kutekeleza mipango wanayoiweka.

Mbunge wa Wafanyakazi Mkoa wa Pwani Dk Alice Kaijage alisema kuwa wananchi wamefanya jambo zuri kuwachagua viongozi hao kutoka CCM kwani wana uwezo mzuri wa kusimamia miradi ya maendeleo ambayo mipango huanzia ngazi ya Mitaa na kupitishwa Bungeni.

Kaijage aliwapongeza viongozi hao wa Serikali za Mitaa kwa ushindi walioupata nakuwataka  wakafanye kazi kwa kuwatumikia wananchi na kazi zao wanapozifanya wanapaswa kumtanguliza Mungu.

Moja ya wenyeviti walioapishwa Elizabeth Nyambilila alisema kuwa kipaumbele chake cha kwanza atakachoanza nacho ni kuhamasisha ujenzi wa shule ya msingi.

Nyambilila alisema kuwa tayari walishaanza mikakati kwanza ni kupata eneo hivyo wataenda kutafuta eneo kwa ajili ya kufanya ujenzi hio ili kuwapunguzia changamoto watoto wa mtaa huo kusoma mbali.

DK ALICE AWASHUKURU WANANCHI KWA KUWAPATIA USHINDI CCM UCHAGUZI SERIKALI

MBUNGE wa Wafanyakazi Mkoa wa Pwani Dr Alice Kaijage amewashukuru wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kuwachagua wenyeviti wote na wajumbe wa Serikali za Mitaa wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM)


Dk Kaijage ameyasema hayo wakati wa uapisho wa wenyeviti Serikali za Mitaa wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Amesema kuwa wananchi wamefanya jambo zuri kuwachagua viongozi hao kutoka CCM kwani wana uwezo mzuri wa kusimamia miradi ya maendeleo.

"Nawapongeza viongozi wetu wa Serikali za Mitaa kwa ushindi mlioupata nendeni mkafanye kazi kwa kuwatumikia wananchi na kazi zenu mnapozifanya mnapaswa kumtanguliza Mungu,"amesema Dk Kaijage.

Monday, November 18, 2024

VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VINAVYOSIMAMIA ULINZI NA AMANI KUSINI MWA AFRIKA (SADC) ZIANDAE MITAALA KUZINGATIA MATISHIO YANAYOZIKABILI NCHI WANACHAMA

Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu Meja Jenerali Iddi Said Nkambi amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Serikali na Kiraia zinazohusika na Ulinzi wa Amani chini ya Mwavuli wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) kuhakikisha zinandaa mitaala ya kuendeshea mafunzo ya Ulinzi wa Amani kwa kuzingatia matishio yanayozikabili nchi wanachama.

Meja Jenerali Nkambi ameyasema hayo leo tarehe 18 Novemba 2024 wakati wa ufunguzi wa Semina fupi ya siku 5 inayohusu  uwasilishaji wa mitaala mipya ya mafunzo itakayotumika kuandaa  Majeshi ya SADC, semina inayofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani (PTC) kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam.

Semina hiyo inayoendeshwa na Chuo cha Ulinzi wa Amani cha Kikanda chenye Makao Makuu yake nchini Zimbabwe inahudhuriwa na washiriki kutoka nchi wanachama wa SADC ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo katika kukabiliana na matishio pindi wanapokuwa katika majukumu ya Ulinzi wa Amani ndani ya ukanda wa SADC na sehemu zingine watakapopewa jukumu.