Friday, November 29, 2024

WENYEVITI WAAPISHWA WATAKIWA WASIUZE ARDHI


WENYEVITI wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa hivi karibuni kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa wasijihusishe na uuzaji ardhi ili kuepukana na migogoro ya ardhi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa wakati wa kuapishwa kwa wenyeviti hao pamoja na wajumbe wa Serikali za Mitaa kwenye Halmashauri hiyo.

Shemwelekwa alisema kuwa wenyeviti hao waachane na masuala ya uuzaji ardhi kwani inayohusika ni Halmashauri kwani baadhi yao walikuwa wakijihusisha na uuzaji ardhi.

"Msijihusishe na masuala ya uuzaji ardhi pia itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi hivyo wao wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo,"alisema Shemwelekwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mussa Ndomba alisema kuwa wenyeviti wasifanye vita na watendaji wa mitaa kama kuna jambo waangalie namna ya kutatua.

Ndomba alisema kuwa wale ni wataalamu wasigombane nao kwani hawatafanya kazi vizuri na wanaweza kuwakwamisha kwani wanambinu nyingi wanaweza kuwakwamisha kwenye majukumu yao hivyo washirikiane nao na kama kuna changamoto wakae nao chini ili kutatua na kurekebishana.

"Masuala ya mihuri nimelisikia wananchi wapate huduma bure bila ya gharama na kuhudumiwa haambiwi toa fedha sijui ya nini anatakiwa apate huduma bora na kwa wakati,"alisema Ndomba.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa jukumu lao kubwa kurudisha deni kwa wananchi ambao wamewakopesha kura walizowapigia na wanatakiwa kuwatumikia na wasinunue bali wapewe huduma bure.

Koka alisema kuwa wanapaswa kuwatumikia na kuwashirikisha kwenye vikao pia waitishe mikutano na kuwapatia mrejesho wa masuala mbalimbali na kutekeleza mipango wanayoiweka.

Mbunge wa Wafanyakazi Mkoa wa Pwani Dk Alice Kaijage alisema kuwa wananchi wamefanya jambo zuri kuwachagua viongozi hao kutoka CCM kwani wana uwezo mzuri wa kusimamia miradi ya maendeleo ambayo mipango huanzia ngazi ya Mitaa na kupitishwa Bungeni.

Kaijage aliwapongeza viongozi hao wa Serikali za Mitaa kwa ushindi walioupata nakuwataka  wakafanye kazi kwa kuwatumikia wananchi na kazi zao wanapozifanya wanapaswa kumtanguliza Mungu.

Moja ya wenyeviti walioapishwa Elizabeth Nyambilila alisema kuwa kipaumbele chake cha kwanza atakachoanza nacho ni kuhamasisha ujenzi wa shule ya msingi.

Nyambilila alisema kuwa tayari walishaanza mikakati kwanza ni kupata eneo hivyo wataenda kutafuta eneo kwa ajili ya kufanya ujenzi hio ili kuwapunguzia changamoto watoto wa mtaa huo kusoma mbali.

No comments:

Post a Comment