TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani itaendelea kutoa elimu ya kupambana na rushwa kwa makundi mbalimbali wakati huu wa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Aidha makundi hayo ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, wapiga kura, wagombea, wasimamizi, azaki, taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na waandishi wa habari.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Takukuru Mkoani humo Christopher Myava alisema walishatoa elimu juu ya kupambana na vitendo vya rushwa tangu mchakato wa uchaguzi ndani ya vyama vya siasa.
Myava alisema kuwa makundi hayo ni muhimu kipindi hichi cha uchaguzi lengo likiwa ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa hawatokani na rushwa.
"Tunataka wananchi wachague viongozi bora ambao wataendana na dira ya serikali ya maendeleo kwani serikali inatumia gharama kubwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo viongozi watakaochaguliwa wawe na sifa na uwezo wa kuongoza,"alisema Myava.
Alisema kuwa wanatoa elimu kwa makundi hayo ili kama yataona kuna viashiria vya rushwa waweze kutoa taarifa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani viongozi bora hawatokani na kutoa rushwa bali ni kwa uwezo wao wa kuongoza.
"Tutaendelea kutoa elimu hadi itakapofikia hatua ya kutangaza matokeo ili tuhakikishe wanapatikana viongozi wenye sifa, waadilifu ili wasimamie rasilimali na fedha zinazotolewa ili wananchi wapate maendeleo,"alisema Myava.
Aliongeza kuwa kiongozi atakayechaguliwa apambane na rushwa kwani serikali inatumia gharama kubwa hivyo tutatoa elimu kupitia mikutano na semina.
"Wananchi nao ni sehemu ya mapambano ambapo viashiria vya rushwa ni kama vile kupewa simu, ajira, fedha, ahadi mbalimbali au vitu vya thamani katika hatua za mwanzo tulipata taarifa za vitendo vya rushwa lakini hakuna ushahidi ambao unaweza kutumika kwani ili kufungua shauri lazima kusiwe na shaka,"alisema Myava.
Aliwataka viongozi wanaowania nafasi za uongozi wazingatie sheria, masharti, kanuni na utaratibu wa uchaguzi ili wasije kujikuta wanaingia kwenye changamoto kwa kukiuka miongozo iliyowekwa.
No comments:
Post a Comment