Saturday, October 7, 2017

MAMIA YA WANANCHI WALILIA AJIRA WAMOMBA RC AWASAIDIE






Na John Gagarini, Kibaha

MAMIA ya wananchi wa wilaya ya Kibaha na mkoa wa Pwani wamelilia mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo awasidie kupata ajira wazuia msafara wake kwa mabango kwenye kituo cha ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kilichopo kwenye Kijiji cha Soga inayojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki.

Wananchi hao walifikia hatua hiyo wakati mkuu wa mkoa wa Pwani akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ilipotembelea kujionea ujenzi huo ambao tayari umeanza na kusema kuwa watu wa mkoa huo wamekuwa wakibaguliwa na kuajiriwa watu kutoka Jijini Dar es Salaam zaidi wananchi hao.

Kwa upande wa Rukia Ally amesema kuwa wametumia gharama kubwa kujenga mabanda wanayofanyia biashara hiyo ya chakula na wamekopa mikopo kwenye taasisia za kifedha hali ambayo inawapa wasiwasi huenda wakauziwa mali zao.

Ally amesema kuwa wanahofu kuuziwa mali zao kwani watashindwa kurudisha fedha walizokopa kwa ajili ya kujenga mabanda na kunuanua bidhaa kwa ajili ya biashara hiyo hivyo kumwomba mkuu wa mkoa kuwasaidia ili kampuni hiyo iruhusu waendelee kupata huduma ya chakula nje na si ndani kwa mzabuni.

Kwa upande wake meneja mradi kutoka kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) Mhandisi Maizo Mgedzi amesema kuwa wao wanaajiri kutokana na sifa za waombaji ambao wengi ni madereva na waendeshaji wa mitambo.
Kutokana na malalamiko hayo mkuu huyo wa mkoa wa Pwani ametoa siku saba kwa vyombo vya dola kufutailia suala la rushwa kama lipo na kutaka wahusika waliotajwa na wananchi hao kusimama kupisha uchunguzi.

Aidha ametaka kupelekewa majina ya watu waliajiriwa kama wanatoka mkoa wa Pwani au la kwani serikali imekuwa ikitaka wanufaika wa kwanza wawe wanaoishi kwenye eneo la mradi.

Pia ametaka utaratibu wa chakula nao uangaliwe ili akina baba na mama lishe walioko nje ya eneo hilo la mradi huo waruhusiwe kuendelea kufanyabishara badala ya kuwazuia wafanyakazi wasitoke nje baada ya kupewa mazabuni kwa ajili ya kuwapa chakula.

Naye mwakilishi wa mkandarasi wa kampuni hiyo Merz Oz alisema kuwa waliamua kuacha utaratibu wa wafanyakazi wao kula chakula nje kwa madai kuwa wanatumia muda mwingi na kufanya shughuli kushindwa kufanyika kwa wakati.

Oz alisema kuwa sababu nyingine ni kuhakikisha wafanyakazi wanapata chakula chenye ubora hasa ikizingatiwa kampuni yao ni ya kimataifa hivyo haiwezi kuwaacha wafanyakazi wao wanakula bila ya utaratibu na huwapatia bure chakula hicho jambo ambalo lilipingwa na wananchi.

Mwisho.



Wednesday, September 6, 2017

WATATU WAFA WAKITOKA BUNGENI DODOMA KUSHUHUDIA KUAPISHWA WABUNGE VITI MAALUMU CUF

Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu wamefariki dunia huku wengine watatu wakijeruhiwa walipokuwa wakitokea Bungeni mkoani Dodoma kushuhudia kuapishwa kwa wabunge saba wa Viti Maalumu wa Chama Cha Wananchi (CUF) baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na lori la mizigo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa watu hao walifia papo hapo.
Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 6 majira ya saa 8:30 usiku eneo la Kijiji cha Ubena Zomozi barabara ya Dar es Salaam-Morogoro wilaya ya Kipolisi Chalinze-Bagamoyo.
“Gari lililokuwa limetoka Dodoma kwenda Muheza mkoani Tanga ni aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 968 CSK likiendeshwa na dereva Uled Sarumaa (32) mkazi wa Muheza liligongana na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 929 CBK lenye tela namba T 472 CAX lililokuwa likiendeshwa na Yasin Kanoni (35) mkazi wa Jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo hivyo,”alisema Shana.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni dereva wa Noah Sarumaa, Mary Komba (40) mkulima mkazi wa Muheza na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Isaack mfanyabiashara anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (37).
“Majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Juma Nindi (47) mfanyabiashara wa Muheza, Chausiku Hassan (47) mkulima wa Muheza na Ester Mafie (67) mkulima mkazi wa Muheza,” alisema Shana.
Aidha alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kusubiri uchunguzi wa daktari na kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi huku majeruhi wakiwa wamelazwa kituo cha afya cha Chalinze
Alibainisha kuwa na chanzo cha ajali kinachunguzwa na alipoulizwa juu ya waliokufa kama ni viongozi wa CUF amesema kuwa bado hajapata taarifa kuhusiana na hilo pia dereva wa lori Yasin Kanoni alikimbia mara baada ya tukio hilo na kwa sasa anatafutwa.
Mwisho. 

BABA WA KAMBO AMJERUHI MTOTO KWA KUIBA MAYAI MAWILI





Mtuhumiwa Abdala Machupa akiwa kituo cha Polisi Kongowe
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi Mkoani Pwani linamshikilia Abdala Machupa (49) fundi ujenzi mkazi wa Kongowe kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kumkata na kisu kichwani mwanae wa kufikia (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka (5) mwanafunzi wa shule ya awali ya Kongowe Kati kwa madai ya kuiba mayai mawili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kamanda wa Polisi mkoani humo Jonathan Shana alisema kuwa mtuhumiwa huyo alipata taarifa hizo mitaani za mwanae kuiba mayai hayo.
Kamanda Shana alisema kuwa  mtoto huyo alitutuhumiwa kuiba mayai kwa Bibi Baby Septemba 4 majira ya saa 2 usiku na kumfiki mama yake mzazi aliyefahamika kwa jina moja la Hadija ambaye alimkanya mwanae kwa kumchapa viboko.
“Mnamo Septemba 5 mtuhumiwa huyo alipata taarifa mtaani kuwa mtoto wake kaiba mayai alirudi nyumbani na kuanza kumchapa kwa fimbo na kama haitoshi alichukua panga lakini mwanae mwingine Hamis Abdala miaka (8) akamzuia ndipo alipochukua kisu na kumkata kichwani mara mbili,” alisema Shana.
Alisema kuwa wananchi baada ya kupata taarifa walifika na kuingilia kati ili kumwokoa mtoto huyo na wao ndipo walipomshambulia na kumjeruhi kichwani na kisogoni kisha walimfikisha polisi.
“Mtuhumiwa alipatiwa matibabu na kwa sasa bado yuko mahabusu na amekemea tabia ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto ambapo upelelezi umekamilika na mtuhumiwa alitarajiwa kufikishwa mahakamani jana,” alisema Shana.
Awali akizungumzia juu ya tukio hilo mwenyekiti wa mtaa wa Bamba Amri Mavalla alisema kuwa wakati mtuhumiwa huyo akimwadhibu mama mzazi wa mtoto huyo ambaye ni mjamzito alipoteza fahamu kwa hofu kwa mwanae.
Mavalla alisema kuwa aliletewa taarifa majira ya saa 6 ofisini kwake na ndipo alipokwenda kupata taarifa juu ya tukio hilo ambapo mama mzazi wa mtoto huyo alishindwa kuchukua yoyote wakati baba yake akimwadhibu kutokana na hali yake.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo wasamaria wema walimpa huduma ya kwanza mama huyo wakati huo wakimkimbiza mtoto huyo kituo cha afya cha Kongowe kwa ajili ya matibabu ambapo anaendelea vizuri.
“Mtoto huyo alichukua mayai hayo akiwa anacheza na wenzake lakini yeye peke yake ndiye aliyeadhibiwa na wenzake hawakuchukuliwa hatua yoyote na ameshonwa nyuzi 12 utosini na nyuzi  nane karibu na sikio,” alisema Mavalla.
Aidha alisema kuwa mtuhumiwa huyo alibadilisha nguo akiwa na lengo la kutaka kukimbia na alipoulizwa kampiga mwanae na nini alisema kamchapa tu na fimbo.

Mwisho.

Monday, August 14, 2017

WATATU WAFA PWANI


Na John Gagarini, Kibaha

WATU watatu wamefariki dunia na wengine 11 wamejeruhiwa kutokana na ajali mbili tofauti zilizotokea mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana imesema kuwa matukio hayo yalitokea wilaya za Kisarawe na Bagamoyo.

Kamanda Shana amesema kuwa tukio la kwanza lilitokea Agosti 10 majira ya saa 11:15 jioni eneo la Mwambisi wilaya ya Kisarawe basi dogo aina ya Eicher lenye namba za usajili T192 DDD likitokea Masanga kwenda Buguruni Jijini Dar es Salaam liliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku 11 wakijeruhiwa.

Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni breki kushindwa kufanya kazi na kusababisha gari hilo kupoteza mwelekeo na kupinduka na kusababisha kifo cha mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (60) ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.

Amebainisha kuwa majeruhi wawili Fatma Hamis (35) aliyeumia kifuani na John Clement aliyevunjika mguu wa kulia wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Aidha amesema kuwa baada ya gari hilo kupinduka liligonga mzinga wa nyuki ambao waliingia kwenye basi na kujeruhi watu tisa ambao wamelazwa kwenye hospitali ya Kisarawe na dereva wa gari hilo alikimbia baada ya tukio hilo ambapo jeshi hilo linamtafuta.

Katika tukio la pili dereva wa pikipiki na abiria wake wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari.

Shana amesema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 13 majira ya saa 11:40 jioni ambapo pikipiki hiyo aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 315 BLM iliyokuwa ikiendeshwa na Ally Seif (19) mkazi wa Kerege iligongana na gari aina ya Mitsubishi Fuso likitokea Dar es Salaam kwenda Bagamoyo likiendeshwa na dereva ambaye hakufahamika.

Amebainisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa bodaboda kulipita gari lililokuwa mbele yake kwa kasi bila ya kuchukua tahadhari na kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo hivyo vya dereva na abiria wake Mohamed Rajabu (18) mkazi wa Kerege    

Amewataka wamiliki wa magari kufanya matengenezo ya magari yao pindi yanapokuwa na hitilafu na madereva wasikubali kuendesha magari mabovu pia wafanye ukaguzi wa kina katika magari yao kabla ya kuanza safari kwani ubovu wa magari huchangia ajali kwa kiasi kikubwa.


Mwisho.

Sunday, August 13, 2017

PAKISTANI KUENDELEA KUSAIDIA MIRADI YA MAENDELEO NCHINI





















































Na John Gagarini, Chalinze

NCHI ya Pakistani imesema kuwa itaendelea kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa nchi hiyo na Tanzania.

Hayo yalisemwa na Balozi wa Pakistani hapa nchini Amir Khan wakati wa sherehe za kupokea majengo ya madarasa ya Shule ya Msingi Pakistani Mtete yaliyokarabatiwa na marafiki wa Pakistani.

Khan alisema kuwa nchi yake imekuwa na miradi mbalimbali ya kimaendeleo hapa Tanzania na hiyo inatokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo.

“Tumekuwa na miradi mingi hapa Tanzania na tutaendelea kushirikiana kama walivyofanya wenzetu na kujitolea kukarabati shule hii,” alisema Khan.

Alisema kuwa miradi kama huo uliofanyika kwenye shule hiyo ni fedha ambazo walitoa marafiki wa Pakistani kwa ajili ya kuhakikisha sekta ya elimu inaboreka.

“Suala la elimu ni muhimu kwa watoto ambao baadaye tunatarajia watakuwa wataalamu wazuri hivyo lazima kuwawekea mazingira mazuri ya kusomea,” alisema Khan.

Aidha aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya shule hiyo ili ukarabati uliofanyika uwe na maana hata mazingira yanaendelea kuwa mazuri.

“Kuhusu uzio kwenye shule hiyo alisema kuwa atapeleka ombi hilo kwa marafiki wa Pakistani ili walifanyie kazi kama ilivyoombwa na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,” alisema Khan.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete aliwapongeza Marafiki hao wa Pakistani kwa kuisaidia shule hiyo na kusema kuwa watahakikisha wanenzi ukarabati huo kwa kuitunza miundombinu ya shule.

Ridhiwani alisema kuwa jambo watakalolifanya ni kuhakikisha eneo hilo linapimwa na kuwekewa mipaka ili kukabiliana na wavamizi.

“Tutahakikisha linapimwa na kuwekewa mipaka yake kwani baadhi ya watu wamekuwa wakivamia maeneo yakiwemo yale ya taasisi,” alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa pia watahakikisha miundombinu mingine inatengenezwa ili kuifanya shule hiyo kuwa na mazingira mazuri ya utoaji elimu.


Mwisho.

MBUNGE APONGEZA KAMATI MALIASILI UTALII







Na John Gagarini, Chalinze

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ameipongeza serikali kwa kuipeleka kamati ya Maliasili na Utalii kufuatilia changamoto zinazokabili Vijiji vinavyopakana na Hifadhi.

Aliyasema hayo kwenye kikao cha mwaka cha Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze na kusema kuwa kumekuwa na changamoto nyingi kwenye vijiji hivyo.

Ridhiwani alisema kuwa baadhi ya changamoto ni mipaka baina ya vijiji hivyo na mbuga hiyo hali ambayo imejenga mahusiano mabaya baina ya vijiji na mbuga hiyo.

“Kamati hyo kuja itakuwa ni moja ya njia za kupata ufumbuzi wa changamoto nyingi zilizopo kwa pande zote na itasidia kupunguza tatizo lililopo, ” alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa sehemu ya Hifadhi ya Wami Mbiki ambayo ni njia ya kupita wanyama nayo imeingiliwa hivyo kuna haja ya hatua kuchukuliwa ili kunusuru maeneo hayo.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri Said Zikatimu alisema kuwa kamati hiyo itasaidia sana kuleta suluhu kwani migogoro kwenye vijiji vilivyojirani na hifadhi ni kero kubwa.

Zikatimu alisema kuwa wanaafiki kamati hiyo kuja na kusikiliza ili kutatua changamoto kwenye vijiji husika ili navyo vipate haki zao.


Mwisho.