Wednesday, September 6, 2017

WATATU WAFA WAKITOKA BUNGENI DODOMA KUSHUHUDIA KUAPISHWA WABUNGE VITI MAALUMU CUF

Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu wamefariki dunia huku wengine watatu wakijeruhiwa walipokuwa wakitokea Bungeni mkoani Dodoma kushuhudia kuapishwa kwa wabunge saba wa Viti Maalumu wa Chama Cha Wananchi (CUF) baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na lori la mizigo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa watu hao walifia papo hapo.
Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 6 majira ya saa 8:30 usiku eneo la Kijiji cha Ubena Zomozi barabara ya Dar es Salaam-Morogoro wilaya ya Kipolisi Chalinze-Bagamoyo.
“Gari lililokuwa limetoka Dodoma kwenda Muheza mkoani Tanga ni aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 968 CSK likiendeshwa na dereva Uled Sarumaa (32) mkazi wa Muheza liligongana na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 929 CBK lenye tela namba T 472 CAX lililokuwa likiendeshwa na Yasin Kanoni (35) mkazi wa Jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo hivyo,”alisema Shana.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni dereva wa Noah Sarumaa, Mary Komba (40) mkulima mkazi wa Muheza na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Isaack mfanyabiashara anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (37).
“Majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Juma Nindi (47) mfanyabiashara wa Muheza, Chausiku Hassan (47) mkulima wa Muheza na Ester Mafie (67) mkulima mkazi wa Muheza,” alisema Shana.
Aidha alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kusubiri uchunguzi wa daktari na kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi huku majeruhi wakiwa wamelazwa kituo cha afya cha Chalinze
Alibainisha kuwa na chanzo cha ajali kinachunguzwa na alipoulizwa juu ya waliokufa kama ni viongozi wa CUF amesema kuwa bado hajapata taarifa kuhusiana na hilo pia dereva wa lori Yasin Kanoni alikimbia mara baada ya tukio hilo na kwa sasa anatafutwa.
Mwisho. 

No comments:

Post a Comment