Saturday, September 9, 2017
Wednesday, September 6, 2017
WATATU WAFA WAKITOKA BUNGENI DODOMA KUSHUHUDIA KUAPISHWA WABUNGE VITI MAALUMU CUF
Na John
Gagarini, Kibaha
WATU
watatu wamefariki dunia huku wengine watatu wakijeruhiwa walipokuwa wakitokea
Bungeni mkoani Dodoma kushuhudia kuapishwa kwa wabunge saba wa Viti Maalumu wa
Chama Cha Wananchi (CUF) baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na lori
la mizigo.
Hayo
yalisemwa mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana
alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa watu hao walifia papo hapo.
Kamanda
Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 6 majira ya saa 8:30 usiku
eneo la Kijiji cha Ubena Zomozi barabara ya Dar es Salaam-Morogoro wilaya ya
Kipolisi Chalinze-Bagamoyo.
“Gari
lililokuwa limetoka Dodoma kwenda Muheza mkoani Tanga ni aina ya Toyota Noah
lenye namba za usajili T 968 CSK likiendeshwa na dereva Uled Sarumaa (32) mkazi
wa Muheza liligongana na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 929 CBK
lenye tela namba T 472 CAX lililokuwa likiendeshwa na Yasin Kanoni (35) mkazi
wa Jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo hivyo,”alisema Shana.
Aliwataja
waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni dereva wa Noah Sarumaa, Mary Komba (40)
mkulima mkazi wa Muheza na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Isaack
mfanyabiashara anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (37).
“Majeruhi
wa ajali hiyo kuwa ni Juma Nindi (47) mfanyabiashara wa Muheza, Chausiku Hassan
(47) mkulima wa Muheza na Ester Mafie (67) mkulima mkazi wa Muheza,” alisema
Shana.
Aidha
alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye Hospitali Teule ya Rufaa ya
mkoa wa Pwani Tumbi kusubiri uchunguzi wa daktari na kusubiri ndugu kwa ajili
ya mazishi huku majeruhi wakiwa wamelazwa kituo cha afya cha Chalinze
Alibainisha
kuwa na chanzo cha ajali kinachunguzwa na alipoulizwa juu ya waliokufa kama ni
viongozi wa CUF amesema kuwa bado hajapata taarifa kuhusiana na hilo pia dereva
wa lori Yasin Kanoni alikimbia mara baada ya tukio hilo na kwa sasa anatafutwa.
Mwisho.
BABA WA KAMBO AMJERUHI MTOTO KWA KUIBA MAYAI MAWILI
![]() |
Mtuhumiwa Abdala Machupa akiwa kituo cha Polisi Kongowe |
Na John
Gagarini, Kibaha
JESHI la
Polisi Mkoani Pwani linamshikilia Abdala Machupa (49) fundi ujenzi mkazi wa Kongowe
kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kumkata na kisu kichwani mwanae wa kufikia (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka (5) mwanafunzi wa shule ya awali ya Kongowe Kati kwa
madai ya kuiba mayai mawili.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizotolewa na kamanda wa Polisi mkoani humo Jonathan Shana
alisema kuwa mtuhumiwa huyo alipata taarifa hizo mitaani za mwanae kuiba mayai hayo.
Kamanda
Shana alisema kuwa mtoto huyo alitutuhumiwa
kuiba mayai kwa Bibi Baby Septemba 4 majira ya saa 2 usiku na kumfiki mama yake
mzazi aliyefahamika kwa jina moja la Hadija ambaye alimkanya mwanae kwa
kumchapa viboko.
“Mnamo
Septemba 5 mtuhumiwa huyo alipata taarifa mtaani kuwa mtoto wake kaiba mayai
alirudi nyumbani na kuanza kumchapa kwa fimbo na kama haitoshi alichukua panga
lakini mwanae mwingine Hamis Abdala miaka (8) akamzuia ndipo alipochukua kisu
na kumkata kichwani mara mbili,” alisema Shana.
Alisema kuwa
wananchi baada ya kupata taarifa walifika na kuingilia kati ili kumwokoa mtoto
huyo na wao ndipo walipomshambulia na kumjeruhi kichwani na kisogoni kisha
walimfikisha polisi.
“Mtuhumiwa
alipatiwa matibabu na kwa sasa bado yuko mahabusu na amekemea tabia ya vitendo
vya ukatili kwa wanawake na watoto ambapo upelelezi umekamilika na mtuhumiwa
alitarajiwa kufikishwa mahakamani jana,” alisema Shana.
Awali
akizungumzia juu ya tukio hilo mwenyekiti wa mtaa wa Bamba Amri Mavalla alisema
kuwa wakati mtuhumiwa huyo akimwadhibu mama mzazi wa mtoto huyo ambaye ni
mjamzito alipoteza fahamu kwa hofu kwa mwanae.
Mavalla
alisema kuwa aliletewa taarifa majira ya saa 6 ofisini kwake na ndipo
alipokwenda kupata taarifa juu ya tukio hilo ambapo mama mzazi wa mtoto huyo
alishindwa kuchukua yoyote wakati baba yake akimwadhibu kutokana na hali yake.
Alisema kuwa
baada ya tukio hilo wasamaria wema walimpa huduma ya kwanza mama huyo wakati
huo wakimkimbiza mtoto huyo kituo cha afya cha Kongowe kwa ajili ya matibabu
ambapo anaendelea vizuri.
“Mtoto
huyo alichukua mayai hayo akiwa anacheza na wenzake lakini yeye peke yake ndiye
aliyeadhibiwa na wenzake hawakuchukuliwa hatua yoyote na ameshonwa nyuzi 12
utosini na nyuzi nane karibu na sikio,”
alisema Mavalla.
Aidha
alisema kuwa mtuhumiwa huyo alibadilisha nguo akiwa na lengo la kutaka kukimbia
na alipoulizwa kampiga mwanae na nini alisema kamchapa tu na fimbo.
Mwisho.
Monday, August 14, 2017
WATATU WAFA PWANI
Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu wamefariki
dunia na wengine 11 wamejeruhiwa kutokana na ajali mbili tofauti zilizotokea mkoani
Pwani.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kamanda wa Polisi mkoani Pwani
Jonathan Shana imesema kuwa matukio hayo yalitokea wilaya za Kisarawe na Bagamoyo.
Kamanda Shana
amesema kuwa tukio la kwanza lilitokea Agosti 10 majira ya saa 11:15 jioni eneo
la Mwambisi wilaya ya Kisarawe basi dogo aina ya Eicher lenye namba za usajili
T192 DDD likitokea Masanga kwenda Buguruni Jijini Dar es Salaam liliacha njia
na kupinduka na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku 11 wakijeruhiwa.
Amesema kuwa
chanzo cha ajali hiyo ni breki kushindwa kufanya kazi na kusababisha gari hilo
kupoteza mwelekeo na kupinduka na kusababisha kifo cha mwanamke mmoja anayekadiriwa
kuwa na umri wa miaka (60) ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.
Amebainisha kuwa
majeruhi wawili Fatma Hamis (35) aliyeumia kifuani na John Clement aliyevunjika
mguu wa kulia wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Aidha amesema
kuwa baada ya gari hilo kupinduka liligonga mzinga wa nyuki ambao waliingia kwenye
basi na kujeruhi watu tisa ambao wamelazwa kwenye hospitali ya Kisarawe na dereva
wa gari hilo alikimbia baada ya tukio hilo ambapo jeshi hilo linamtafuta.
Katika tukio
la pili dereva wa pikipiki na abiria wake wamefariki dunia baada ya kugongwa na
gari.
Shana amesema
kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 13 majira ya saa 11:40 jioni ambapo pikipiki
hiyo aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 315 BLM iliyokuwa ikiendeshwa na
Ally Seif (19) mkazi wa Kerege iligongana na gari aina ya Mitsubishi Fuso likitokea
Dar es Salaam kwenda Bagamoyo likiendeshwa na dereva ambaye hakufahamika.
Amebainisha kuwa
chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa bodaboda kulipita gari lililokuwa mbele yake
kwa kasi bila ya kuchukua tahadhari na kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo
hivyo vya dereva na abiria wake Mohamed Rajabu (18) mkazi wa Kerege
Amewataka wamiliki
wa magari kufanya matengenezo ya magari yao pindi yanapokuwa na hitilafu na
madereva wasikubali kuendesha magari mabovu pia wafanye ukaguzi wa kina katika
magari yao kabla ya kuanza safari kwani ubovu wa magari huchangia ajali kwa
kiasi kikubwa.
Mwisho.
Sunday, August 13, 2017
PAKISTANI KUENDELEA KUSAIDIA MIRADI YA MAENDELEO NCHINI
Na John Gagarini, Chalinze
NCHI ya Pakistani imesema kuwa itaendelea kusaidia miradi mbalimbali ya
maendeleo hapa nchini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa nchi hiyo na
Tanzania.
Hayo yalisemwa na Balozi wa Pakistani hapa nchini Amir Khan wakati wa
sherehe za kupokea majengo ya madarasa ya Shule ya Msingi Pakistani Mtete
yaliyokarabatiwa na marafiki wa Pakistani.
Khan alisema kuwa nchi yake imekuwa na miradi mbalimbali ya kimaendeleo
hapa Tanzania na hiyo inatokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo.
“Tumekuwa na miradi mingi hapa Tanzania na tutaendelea kushirikiana kama
walivyofanya wenzetu na kujitolea kukarabati shule hii,” alisema Khan.
Alisema kuwa miradi kama huo uliofanyika kwenye shule hiyo ni fedha
ambazo walitoa marafiki wa Pakistani kwa ajili ya kuhakikisha sekta ya elimu
inaboreka.
“Suala la elimu ni muhimu kwa watoto ambao baadaye tunatarajia watakuwa
wataalamu wazuri hivyo lazima kuwawekea mazingira mazuri ya kusomea,” alisema
Khan.
Aidha aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya shule hiyo ili
ukarabati uliofanyika uwe na maana hata mazingira yanaendelea kuwa mazuri.
“Kuhusu uzio kwenye shule hiyo alisema kuwa atapeleka ombi hilo kwa marafiki
wa Pakistani ili walifanyie kazi kama ilivyoombwa na Mbunge wa Jimbo la
Chalinze Ridhiwani Kikwete,” alisema Khan.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete aliwapongeza Marafiki hao wa
Pakistani kwa kuisaidia shule hiyo na kusema kuwa watahakikisha wanenzi
ukarabati huo kwa kuitunza miundombinu ya shule.
Ridhiwani alisema kuwa jambo watakalolifanya ni kuhakikisha eneo hilo
linapimwa na kuwekewa mipaka ili kukabiliana na wavamizi.
“Tutahakikisha linapimwa na kuwekewa mipaka yake kwani baadhi ya watu
wamekuwa wakivamia maeneo yakiwemo yale ya taasisi,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa pia watahakikisha miundombinu mingine inatengenezwa ili
kuifanya shule hiyo kuwa na mazingira mazuri ya utoaji elimu.
Mwisho.
MBUNGE APONGEZA KAMATI MALIASILI UTALII
Na John Gagarini, Chalinze
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ameipongeza serikali kwa
kuipeleka kamati ya Maliasili na Utalii kufuatilia changamoto zinazokabili
Vijiji vinavyopakana na Hifadhi.
Aliyasema hayo kwenye kikao cha mwaka cha Madiwani wa Halmashauri ya
Chalinze na kusema kuwa kumekuwa na changamoto nyingi kwenye vijiji hivyo.
Ridhiwani alisema kuwa baadhi ya changamoto ni mipaka baina ya vijiji
hivyo na mbuga hiyo hali ambayo imejenga mahusiano mabaya baina ya vijiji na
mbuga hiyo.
“Kamati hyo kuja itakuwa ni moja ya njia za kupata ufumbuzi wa
changamoto nyingi zilizopo kwa pande zote na itasidia kupunguza tatizo
lililopo, ” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa sehemu ya Hifadhi ya Wami Mbiki ambayo ni njia ya kupita
wanyama nayo imeingiliwa hivyo kuna haja ya hatua kuchukuliwa ili kunusuru
maeneo hayo.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri Said Zikatimu alisema kuwa kamati hiyo
itasaidia sana kuleta suluhu kwani migogoro kwenye vijiji vilivyojirani na
hifadhi ni kero kubwa.
Zikatimu alisema kuwa wanaafiki kamati hiyo kuja na kusikiliza ili
kutatua changamoto kwenye vijiji husika ili navyo vipate haki zao.
Mwisho.
Monday, August 7, 2017
SIMBA WATOA MISAADA WAFANYA USAFI ZAHANATI YA MWENDAPOLE KIBAHA
Na John
Gagarini, Kibaha
TAWI la Simba
wilayani Kibaha limepongezwa na zahanati ya Mwendapole wilayani Kibaha kwa
kujitolea zawadi kwa wagonjwa pamoja na kufanya usafi.
Hayo
yalisemwa na muuguzi mganga mfawidhi wa zahanati hyo Gloria Leonidas wakati wa
kuushukuru uongozi wa tawi hilo baada ya kumaliza kufanya usafi na kutoa zawadi
za sabuni kwa wagonjwa.
Dk leonidas
alisema kuwa vilabu vyote vinapaswa kuunga mkono kitu kilichofanywa na tawi
hilo la Simba kwa kufanya shughuli za usafi na kujitolea kile walichonacho.
“Timu
zinapaswa kuangalia mbali zaidi kwa kujishughulisha na kuisaidia jamii kama
walivyofanya Wanasimba hawa kwani wameonyesha uzalendo wa hali ya juu,” alisema
Dk Leonidas.
Alisema kuwa
kusaidia sehemu kama hizo za jamii kunaleta motisha kwa watumishi wanaofanya
kazi sehemu hizo za kutolea huduma inawafanya kuona kuwa wanawajali.
“Mkitusaidia
kama hivi tunapata faraja hata wagonjwa nao wanajisikia vizuri kufarijiwa kama
walivyofanya Wanasimba Kibaha tunaomba na klabu za hapa nazo ziige mfano huu,”
alisema Dk Leonidas.
Kwa upande
wake makamu mwenyekiti wa tawi la Simba Kibaha Said Tisa alisema kuwa wamekuwa
na utaratibu wa kujitolea kwa jamii na sehemu za kutolea huduma.
Tisa alisema
kuwa wanaungana na Simba makao makuu wakati wa kuelekea tamasha la Simba Day
ambalo huazimishwa kila mwaka ambapo mwaka huu linafanyika leo uwanja wa taifa.
Alisema kuwa
wataendelea na utamaduni huo ili kuisaidia jamii iweze kuona faida ya timu na
siyo kushiriki uwanjani pekee bali hata kuwajibika kwa jamii.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)