Thursday, October 2, 2014

SHERIA ZA USHIRIKA ZIMEPITWA NA WAKATI, UMRI WA URAIS UPUNGUZWE

Na John Gagarini, Mkuranga
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amesema kuwa sheria za Ushirika  zimepitwa na wakati hali ambayo inasababisha baadhi ya watu kutumia mwanya kuwadhulumu wakulima wa zao hilo hapa nchini.
Kutokana na fedha nyingi kutumiwa kwa matumizi binafsi na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kumesababisha chama kikuu cha ushirika cha mkoa CORECU kuwa na madeni makubwa ambapo mabenki yamekataa kukikopesha fedha kwa ajili ya ununuzi wa zao la korosho.
Aliyasema hayo wilayani Mkuranga wakati wa mkutano wa mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao la korosho (CIDTF) kwa wakulima  na wataalamu wa mkoa wa Pwani na bodi ya zao la korosho nchini juu ya msimu mpya wa uuuzaji na ununuzi wa zao hilo.
Mahiza alisema kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika vya zao la korosho mkoani humo wamewadhulumu wakulima malipo ya korosho walizo wauzia wanunuzi hali iliyosababisha hasara kubwa kwa mkoa.
“Mfano mkoa wa Pwani ulikidhamini chama kikukuu cha ushirika cha mkoa (CORECU) kupata mikopo toka kwenye mabenki ambapo CRDB ilitoa bilioni 6 na NMB ilitoa biloni 3 lakini fedha hizo zimeshindwa kurejeshwa hali ilioyosababisha chama hicho kishindwe kukopeshwa tena,” alisema Mahiza.
Alisema kuwa kila wanapojaribu kuwachukulia hatua viongozi hao inashindikana kutokana na sheria zilizopo za ushirika ambazo zinaonekana zinawalinda viongozi hao hivyo kushindwa kuadhibiwa huku wakulima wakiendelea kudai fedha zao.
“Ukiwashitaki kwa makosa ya jinai ushirika unasema huwezi kuwashitaki kwa kosa la jinai lakini baada ya kufuata taratibu za kisheria tayari tunaweza kuchukua hatua ambazo ni stahiki kwa viongozi hao ambao baadhi yao wamezitumia fedha hizo kwa manufaa binafsi,” alisema Mahiza.
Aidha alisema kuwa sheria hizo si nzuri kwani zinawaumiza wakulima lakini kwa sasa mkoa umefikia hatua nzuri za kuweza kuwashtaki waliohusika na kula fedha za wakulima kwani ushirika sio kudhulumu watu bali ni kuboresha maslahi ya wakulima.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Athuman Nkinde alisema kuwa maandalizi ya msimu wa kilimo kwa zao hilo tayari zimeanza na mkoa wa Pwani utapatiwa pembejeo za dawa za kupulizia pamoja na miche bora ya zao hilo ipatayo 70,000.
Nkinde alisema kuwa matarajio ni mkoa huo kuzalisha zao hilo kwa wingi ili kuboresha kipato cha wakulima kwani zao hilo ni utajiri endapo wakulima na wataalamu watawaelekeza kilimo bora cha zao hilo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa Sadifa Juma ameomba suala la umri wa kugombea Uspika na Urais liangaliwe ili kuwapa nafasi vijana kuweza kugombea nafasi hizo kwa kupunguza umri wa sasa wa miaka 40 na kuwa 30.
Aliyasema hayo wakati wa akiwahutubia vijana wa umoja huo kutoka Jimbo la Kibaha Mjini, alipokuwa akifunga kambi ya mafunzo ya vijana ya siku 10 ambayo yalifunguliwa na katibu mkuu wa Abdulrahman Kinana Septemba 19.
Sadifa alisema kuwa kwenye Ubunge unaruhusu umri wa kuanzia miaka 21 lakini kwenye nafasi hizo umri ni kuanzia miaka 40 jambo ambalo ameona kuwa vijana hawatendewi haki.
“Kama ubunge ni miaka 21 na Uspika pamoja na Urais angalau iwe kuanzia miaka 30 na kuendelea kwani kwa umri huo bado kijana ana nguvu na anaweza kutekeleza vema majukumu yake tofuati na kumchagua Rais mwenye umri mkubwa,” alisema Sadifa.
Alisema kuwa mambo yanabadilika ifike wakati sasa vijana nao wapate nafasi kutokana na uwezo wake kwani vijana ndiyo wenye nguvu na wanauwezo mkubwa wa kutekeleza majuku yao ikiwa ni pamoja na kuongoza.
“Nchi kama Kongo na Korea Marais wao ni vijana lakini wanaongoza vizuri hivyo hakuna sababu ya kuwawekea mazingira magumu ya kugombea nafasi hizo za juu wapewe nafasi kama watafanikiwa kuchaguliwa basi wachaguliwe kwani kiongozi siyo umri bali ni uwezo wa kuongoza,” alisema Sadifa.
Kw upande wake kamanda wa Vijana wa Kibaha Mjini Silvestry Koka alitoa sare 50 kwa makamanda wa umoja huo Green (Guard) zenye thamani ya shilingi milioni 2.5 na kuwataka vijana hao kuyatumia mafunzo hayo kukiimarisha chama.
 Awali akisoma risala ya kambi hiyo ya vijana katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Kibaha Mjini Khalid King alisema kuwa kambi hiyo iliwafundisha vijana 101 juu ya masuala mbalimbali yakiwemo ya itikadi za chama, ujasiriamali, uongozi na masuala mbalimbali ya kisiasa.
Mwisho.



No comments:

Post a Comment