Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Halima Kihemba amekipongeza
kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake
(WLAC) kwa kujitolea kutoa huduma za kisheria bure kwa wananchi wasio na uwezo
wa kumudu gharama za kuwalipa wanasheria.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akifunga mafunzo ya
wasaidizi wa Kisheria wilayani humo ya siku 25 yaliyoandaliwa na Kituo cha
Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).
Kihemba alisema kuwa kituo hicho kimeonyesha umuhimu wa kutoa
msaada wa kisheria ni muhimu kwa watu hususani wanawake na watoto ambao
wamekuwa wakipoteza haki zao kutokana na baadhi ya watu kutumia unyonge wao
wakutokuwa na sauti ndani ya jamii kuwadhulumu haki zao.
“Huduma ya kisehria ni muhimu ndani ya jamii lakini watu
wengi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama hizo hivyo kushindwa kupata haki zao
hivyo mashirika kama haya ni ya kuigwa,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa makundi hayo mawili ndiyo yamekuwa
yakidhulumiwa haki zao kwa kiasi kikubwa hivyo mashirika kama WLAC
yanayojitolea lazima yaungwe mkono na wadau mbalimbali ikiwemo serikali.
Awali akimkaribisha mkuu wa wilaya mkuu wa idara ya Mafunzo
ya WLAC Magdalena Mlolere alisema kuwa lengo la kituo hicho ni kuhakikisha kuwa
watu wanapata haki zao ambazo ni za msingi na ziko kikatiba.
Mlolere alisema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo kwa
wasaidizi wa kiseheria wa vituo vya KPC na KPP ni ili waweze kusaidia wananchi
kutatua migogoro inayojitokeza kabla ya kufika kwenye vyombo vya kisheria
ikiwemo mahakama na polisi.
“Mafunzo hayo pia yatasaidia kupunguza kesi zinazopelekwa
mahakamani ambazo nyingine zimekuwa zikitumia muda mrefu kuamuliwa na kuwafanya
wahusika kutumia muda mwingi kwenda mahakamani huku wakishindwa kufanya
shughuli zao za maendeleo,” alisema Mlolere.
Akisoma hotuba mbele ya mgeni rasmi moja ya wahitimu wa
mafunzo hayo kwa niaba ya wahitimu John Gagarini alisema kuwa changamoto
zinavyovikabli vituo hivyo ni baadhi ya wanajamii kutokuwa wawazi katika
kuyapeleka mashauri hayo kwenye vituo hivyo pia ni ukosefu wa usafiri wa kuweza
kufika kwenye maeneo hasa yale ya vijijini, jumla ya wahitimu 32 walihitimu
mafunzo hayo na kukabidhiwa vyeti na mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha Halima
Kihemba.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment