Na John Gagarini, Kibaha
WAZAZI wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuwalinda
watoto wao waepukane na matumizi mabaya ya Teknolojia ya mawasiliano ili
wasifuate tamaduni mbaya za nchi za Magharibi ambazo zimewaharibu vijana
Tanzania.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Mji wa Kibaha, Jenifa Omollo wakati wa
mahafali ya tisa ya darasa la saba ya shule ya awali na Msingi ya Kibaha
Independent (KIPS).
Omollo alisema kuwa teknolojia ya mawasiliano ni nzuri endapo
inatumiwa vizuri lakini ina athari endapo itatumiwa vibaya hasa kwa vijana
kuiga tamaduni za nje zinazohamasisha vitendo viovu.
“Tuko kwenye utandawazi ambao unatumia teknolojia ya
mawasiliano na kuifanya dunia kuwa Kijiji na kumekuwa na muingiliano mkubwa wa
tamaduni ambazo nyingine ni mbaya zinazokinzana na maadili ya kitanzania ikiwa
ni pamoja na mavazi, ngono, matumizi ya dawa za kulevya na matumizi mabaya ya
mitandao ya kuangalia picha za ngono,” alisema Omollo.
Alisema kuwa kundi la vijana limeathiriwa kwa kiasi kikubwa
na tamaduni hizo mbaya ambapo vijana hao wanafikiri ndiyo kwenda na wakati
kumbe wanajiharibia maisha yao ya baadaye.
“Kwa sasa kuna matumizi mabaya ya teknolojia kupitia njia za
simu, kompyuta na televisheni hivyo lazima wazazi wawaelekeze matumizi sahihi
ya vifaa hivyo ambavyo endapo vitatumiwa vizuri vinaweza kuwa na manufaa mazuri
kwa watumiaji,” alisema Omollo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mkurugenzi wa shule hiyo Said
Mfinanga alisema kuwa shule yao moja ya vitu inavyozingatia ni maadili mazuri
ya Kitanzania ili wanafunzi wanapotoka hapo wawe na tabia njema.
Mfinanga alisema kuwa licha ya shule kufundisha masomo ya
mawasiliano ya Kompyuta lakini wanazingatia maadili ili kuepuka na matumizi
mabaya ya Teknolojia na kuzingatia kutoa elimu bora.
Shule hiyo ni ya kutwa na bweni ilianzishwa mwaka 2002 na ina
jumla ya wanafunzi 480 na ni miongoni mwa shule zinazofanya vizuri kwenye
wilaya hiyo pamoja na mkoa ambapo mwaka huu jumla ya wahitimu 39 walipewa vyeti
vya kuhitimu darasa la saba.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment