Sunday, October 19, 2014

WACHINA WAVUTIWA BAGAMOYO

Na John Gagarini, Bagamoyo
JIMBO la Jilin nchini China limekubali kuwekeza hapa nchini kwenye eneo la Uwekezaji la (EPZ) la Kamal lililopo Kijiji cha Kerege kwa Kiwete wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Uwekezaji huo utafanyika baada ya ujio wa baadhi ya viongozi wa Jimbo hilo kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji wilayani humo na kuonekana kuvutiwa na sehemu hiyo.
Akizungumza jana mara baada ya kutembelea maeneo kadhaa akiongozana na mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza na sekretarieti ya mkoa wa Pwani na kuvutiwa na eneo hilo la uwekezaji la EPZ, Naibu Gavana wa Jimbo hilo Zhoncheng Sui alisema ameridhika na eneo hilo.
Sui alisema kuwa kutokana na urafiki wa kihistoria uliyopo kati ya Tanzania na China toka enzi za viongozi wa mataifa hayo Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Sung kumekuwa na ushirikiano ambao ni wa damu hivyo lazima udumishwe kwa ushirikiano wa kimaendeleo.
“Tumeona mambo mengi ambayo tunaweza kushirikiana ambapo moja ni pale kwenye eneo la uwekezaji ambapo tutakuja kuwekeza hapo kwani kuna miuondombinu mizuri ya barabara, maji na umeme pia waiteni na wenzetu waliopo hapa Tanzania ili nao waje wajionee na kuangalia namna wanavyoweka kuwekeza kwenye mkoa huu wa Pwani,” alisema Sui.
Awali akimkaribisha naibu gavana wa Jimbo hilo la Jilin mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza alisema kuwa mkoa wa Pwani una mambo mengi ambayo wawekezaji wanaweza kuwekeza ikiwa ni pamoja na kwenye kilimo, uvuvi, utalii na mifugo.
“Fursa zipo nyingi ndani ya mkoa wetu na hata miundombinu ya barabara, anga, bandari, uememe na reli viko vizuri kwa ajili ya kufanikisha uwekezaji ambao una hitaji uwepo wa mawasiliano mazuri,” alisema Mahiza.
Ujumbe huo ulikuwa na ziara ya siku moja wilayani Bagamoyo kutembelea  maeneo ya uwekezaji kwenye ujenzi wa soko la kimataifa la samaki, eneo itakapojengwa bandari na eneo la uwekezaji la Kamal.

Mwisho.
 Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza katikati mwenye kilemba akiwa na ugeni toka nchini China wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa wilaya ya Bagamoyo mara baada ya kumaliza mkutano wa pamoja uliofanyika kwenye hoteli ya Oceanic bay Hotel $ Resort  

 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza kulia akiteta jambo na kiongozi wa ujumbe  kutoka Jimbo la Jilin nchini China Zhongcheng Sui wali[potembelea wilaya Bagamoyo kuangalia maeneo ya uwekezaji 



 Mkuu wa mkoa katikati na ugeni kutoka nchini China wakiangalia bomba ambalo limetoboka na maji kumwagika, kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi

No comments:

Post a Comment