Na John Gagarini, Kibaha
NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba Angella Kairuki amewataka
waumini wa Kanisa la Sabato Maili Moja Kibaha mkoani Pwani na wananchi kuendelea
kuiombea nchi isiingie kwenye machafuko .
Waziri Kairuki aliyasema hayo mjini
Kibaha katika kanisa hilo alipokuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kuchangia fedha
za kununulia vifaa vya mawasiliano na kurekodia vya kwaya ya kanisa hilo na
kusema kuwa wasikubali kutumiwa na baadhi ya watu kwa mambo ambayo ni kinyume
na sheria za nchi.
Alisema nchi imekuwa na amani kwa miaka
mingi sasa ikiwa ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine hivyo haina budi kila
mmoja akasali kuliombea taifa ambalo pia likielekea kwenye chaguzi mbalimbali.
“Msiwakubali watu ambao wamekuwa
wakitumia wananchi ili kuvuruga amani ya nchi na wamekuwa wakitaka kuungwa
mkono lakini wanaokuja kupata matatizo ni wananchi na siyo wao hivyo msikubali
kufuata mkumbo,” alisema Waziri Kairuki.
Aidha Waziri Kairuki alisema hakuna
haja ya kuendelezwa kwa mijadala ya katiba inayopendekezwa ama kuibua hoja
zisizo na tija kwa maslahi ya taifa kwani muda wake umekamilika na hatua
inayosubiriwa ni tamko kutoka kwa Mh Rais litakaloeleza wakati wa kupiga kura
ya maoni kwa wananchi.
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la
Sabato Maili Moja Eliasi Timasi alimshukuru Waziri Kairuki kwa nasaha zake na
kusema wataendelea kuhimiza amani kwa kufanya mawasiliano ya karibu na serikali
pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili waumini wa kanisa
hilo.
Katika shughuli hiyo ya kuchangia vifaa vya
mawasiliano ya kanisa na kurekodia kwaya
kulipatikana zaidi ya sh m 22 ambapo ahadi zilizotolewa ni zaidi ya m 19.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment