Monday, October 13, 2014

WAIMBAJI NA KWAYA ZA INJILI ZIJIUNGE NA BASATA

Na John Gagarini, Kibaha

KWAYA na Waimbaji wa nyimbo za Injili nchini wameshauriwa kujisajili Baraza la Sanaa ili watambulike kisheria kwa lengo la kuepuka kudhulumiwa haki za kazi zao.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Angella Kairuki wakati alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuchangia fedha za kununulia vifaa vya mawasiliano na kurekodi albamu ya video ya kwaya ya kanisa la Sabato la Maili Moja Kibaha mkoani Pwani.

Waziri Kairuki alisema kuwa baadhi ya kwenye makanisa ya na waimbaji mbalimbali hawajaona umuhimu wa kujisajili ili ziweze kutambulika na kunufaika kama zilivyo kazi nyingine za sanaa.

“Kwaya na waimbaji wa nyimbo za injili nazo zinawajibu wa kujisajili katika baraza hilo ili ziweze kupata haki zao pamoja fursa mbalimbali pia kukabiliana na baadhi ya watu wanaotumia kazi zao kujinufaisha binafsi huku walengwa wakiwa hawaambulii kitu hivyo sio vyema kukaa bila kujisajili rasmi,” alisema Waziri Kairuki.

Alisema ameona ni vyema akawahimiza kwani  jambo hilo lina manufaa kwa waimbaji na kwaya za makanisa ili waweze kupiga hatua kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wengine wa nyimbo za injili ambao tayari wamepiga hatua.

Alibainisha kuwa muziki unachangia amani,upendo na mshikamano hivyo wajitahidi pia kuimba nyimbo za kuiombea nchi yetu kwa masuala hayo muhimu pamoja na kumtukuza mungu.

“Nawaomba wanakwaya wa nyimbo na waimbaji wa nyimbo za injili kutengeneza albamu za video zenye maadili kwa michezo na mazingira yake pasipo kwenda kinyume na maadili ya kidini na kugeuza injili kuwa biashara, kwani zipo baadhi ya kanda za wasanii wengine ambazo hazionyeshi maadili mazuri,” alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki alisema serikali ipo pamoja na wasanii wa aina zote na inatambua kazi za sanaa ,tasnia ya wasanii na ndio maana katika katiba inayopendekezwa walihakikisha wanatambua kazi za wasanii, katika hafla hiyo kulipatikana zaidi ya sh m 22 ambapo ahadi zilizotolewa ni zaidi ya Mil 19.

Mwisho



No comments:

Post a Comment