Thursday, October 2, 2014

KIBAKA AUWAWA KWA KUCHOMWA MOTO KWA WIZI WA PIKPIKI

Na John Gagarini, Kibaha
KIJANA mwenye umri kati ya miaka (25) na (30) anayedahaniwa kuwa ni kibaka ambaye jina lake halikuweza kufahamika ameuwawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kuiba pikipiki.
Wananchi hao walifikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mtuhumiwa huyo akiwa na mwenzake waliiba pikipiki hiyo huko Gairo mkoani Morogoro na kutaka kuiuza Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa Polisi mkoani humo Athuman Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 25 mwaka huu majira ya saa 1 asubuhi eneo la Pera Chalinze wilaya ya Bagamoyo.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa watuhumiwa hao wawili walikuwa na pikipiki ainaya ya Toyo yenye namba za usajili T 336 BZC ambayo inadhaniwa kuwa waliiba huko Gairo na walifika Chalinze kwa lengo la kutaka kuiuza.
“Vijana hao ambao ni wa kabila la Kimasai walifika hapo huku wakitafuta wateja wa pikipiki hiyo na wananchi hao walipowauliza uthibitisho wa pikipiki hiyo yaani kadi walishindwa kuonyesha na ndipo walipoanza kuwapiga na mmoja alifanikiwa kukimbia huku mwingine akipigwa kisha kuchomwa moto,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa mashambani ukiwa umechomwa moto na kuharibika vibaya sehemu mbalimbali za mwili.
Aidha aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na kuwataka kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment