Na John Gagarini, Kibaha
IMEBAINIKA kuwa baadhi ya watoto wanaojishughulisha na
biashara ndogondogo wilayani Kibaha mkoani Pwani wamejiingiza kwenye mahusiano
ya kimapenzi ambapo fedha wanazopata wananunulia simu za mkononi ili
kuwasiliana na wapenzi wao.
Watoto hao licha ya kuwa na umri mdogo lakini tayari wanajiingiza
kwenye masuala ya mapenzi jambo ambalo ni hatari na linalosababisha kuingia
kwenye ngono wakiwa na umri mdogo hivyo kuongeza vitendo vya ubakajiani ndani
ya jamii.
Akizungumza mjini Kibaha wakati wa mafunzo ya kupinga vitendo
vya ukatili kwa watoto kwa timu za kuzuia vitendo hivyo ndani ya jamii kwenye
kata ya Kibaha wilayani humo mwenyekiti wa mafunzo hayo Alkhas Katopola alisema
kuwa baadhi ya watoto wanamiliki simu ambazo wanazitumia kwa ajili ya
mawasiliano na wapenzi.
“Inashangaza sana kuona watoto wadogo wanamiliki simu za
mkononi na kikubwa wanachokifanya na hizo simu ni masuala ya mapenzi hivyo
kutokana na umri wao kuwa mdogo ni kama vile wanabakwa kwa sasabu wengi wana
mahusiano ya kimapenzi na watu wazima,” alisema Katopolo.
Katopola alisema kuwa wengi wa watoto hao ni wale ambao
hawakupata nafasi ya kwenda au kuacha shule kutokana na sababu mbalimbali za
kimaisha au wenyewe kukataa kuendelea na masomo.
“Pia baadhi ya watoto hawa wanategemewa na familia zao kwa
ajili ya mahitaji ya nyumbani hivyo wazazi au walezi wanashindwa kuwadhibiti
mara wafanyapo vitendo visivyofaa ikiwa ni pamoja na kujihusisha kwenye masuala
ya mahusiano ya kimapenzi,” alisema Katopola.
Kwa upande wake mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la
(KICODET) la Kibaha lililoandaa mafunzo hayo Dk Rose Mkonyi alisema kuwa lengo
la mafunzo hayo ni kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa watoto kwenye
Halmashauri ya Mji wa Kibaha.
“Vitendo vya ukatili kwa watoto ni vingi na ndiyo sababu ya
kuandaa mafunzo hayo ili jamii iweze kujua namna ya kutoa taarifa kwenye vyombo
vya sheria na si kuvifumbia macho kama baadhi ya familia zinavyofanya kwani
baadhi ya wanaofanya vitendo vya ukatili ni ndugu hivyo kuhofia mahusiano
kuvunjika,” alisema Dk Mkonyi.
Dk Mkonyi alisema kuwa mafunzo hayo ambayo yatatumika kuunda
timu za ufuatiliaji wa matukio mbalimbali ya ukatili kwa watoto yamewajengea
uwezo wa kuweza kuwa na mtandao baina yao na vyombo vya sheria kama vile
viongozi wa mitaa, waalimu, jeshi la polisi, mahakimu na wadau wengine
wanaohusika kukabiliana na vitendo hivyo.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Faustina Kayombo
ambaye ni ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha alisema kuwa
tatizo kubwa ni usiri unaofanywa na umaskini imekuwa ni vyanzo chanzo vikuu vya
kuendela kwa vitendo hivyo.
Mradi huo ni wa miaka miwili ambapo mafunzo hayo
yamefadhiliwa na Plan International, UNICEF, Save the Children na Jumuiya ya
Ulaya na serikali kwa kushirikiana na shirika hilo la KICODET.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment