Na John Gagarini, Kibaha
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Piniel Medical Mission la
Jijini Dar es Salaam limewapa fedha wanafunzi wanne wa shule ya sekondari
Kilangalanga ambao wamefaulu daraja la kwanza kwenye mtihani wa Taifa wa kidato
cha sita.
Waliozawadiwa fedha hizo ni pamoja na Peter Didas, Ally
Makutubu, Obote Juma na Venance Peter ambao kila mmoja alikabidhiwa kiasi cha shilingi
100,000 kila mmoja.
Akiwakabidhi fedha hizo mgeni rasmi kwenye makabidhiano hayo
ambayo yalifanyika shuleni hapo Mlandizi Kibaha mwakilishi wa ofisa elimu
wilaya ya Kibaha Blandina Mwenura aliwapongeza wanafunzi hao na kuwataka wanafunzi
watakaofanya mitihani hiyo kutoogopa masomo ya sayansi.
Mwenura alisema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakifanya
vibaya kutokana na kuyaogopa masomo hayo ambayo ndiyo masomo muhimu katika
kupata wataalamu mbalimbali.
“Nalipongeza shirika hili kwa kujitolea kuhamasisha masomo
haya ambayo wanafunzi wamekuwa wakiyakimbia na kukimbilia masomo ya Sanaa
wakidhani kuwa ndiyo rahisi,” alisema Mwenura.
Aidha aliwataka wadau wengine kujitokeza zaidi kuwatia moyo
wanafunzi wanaosoma masomo hayo ili kujenga nchi yenye wataalamu wenye uwezo
mzuri kwani watafanya kazi kwa mapenzi kwa kile walichokisomea.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa shirika hilo Jaqline
Ngoma alisema kuwa walitoa ahadi kwa wanafunzi wa shule hiyo kuwa endapo
mwanafunzi wa kidato cha sita atapata daraja la kwanza watampatia kiasi hicho
cha fedha na huo ndiyo utekelezaji wa ahadi hiyo.
“Lengo letu ni kuwatia moyo wanafunzi wanaosoma masomo ya
sayansi wawe na ujasiri na kuondoa woga kwani wataalamu kwa sasa wanapungua
mfano wataalamu wa afya hivyo lazima tutumie njia ya kuwahamasisha ili wengi
wajiunge na masomo hayo,” alisema Ngoma.
Shule hiyo ya serikali ni ya kutwa ni ya wavulana na
wasichana na bweni kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita wavulana wanaochukua
masomo ya mchepuo wa Sayansi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment