Na John Gagarini, Kibaha
WANAWAKE nchini wametakiwa kutokubali kufumbia macho vitendo
vya ukatili wa kijinsia kwa kuhofia kutengwa na familia zao badala yake wawe
watoa taarifa ili kuwadhibiti watu wanaoendeleza vitendo hivyo ambavyo ni
kinyume cha sheria na uvunjaji wa haki za binadamu.
Tabia ya kuficha ukatili wa kijinsia imesababisha wahusika
kujikuta wakiathirika kutokana na vitendo hivyo ambavyo vimeshamiri kutokana na
kuendelea kwa usiri ndani ya familia.
Hayo yalisema jana mjini Kibaha na mkurugenzi wa benki ya Wanawake
Tanzania Magreth Chacha, wakati wa uzinduzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari
Wanawake Mkoa wa Pwani (PWMO).
Chacha alisema kuwa baadhi ya wanawake wamekuwa wakificha
vitendo hivyo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya wanaume
wasiokuwa na huruma.
“Vitendo vya ukatili wa kijinsi vimekuwa vikifanywa ndani ya familia
huku wanawake amabao ndiyo wahanga wa matukio hayo wamekuwa wakikaa kimya
kuhofia kutengwa na familia zao jambo ambalo limesababisha vitendo hivi
kuendelea,” alisema Chacha.
Alisema kuwa baadhi ya vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na watu
wa karibu wa familia wakiwemo wanandoa na ndugu hali ambayo inasababisha
taarifa hizo kufichwa huku walengwa wakiendelea kuathiriwa na vitendo hivyo
viovu na vya ukatili.
“Baadhi ya vitendo hivyo ni pamoja na wanawake kupigwa,
kutumikishwa kingono, kubakwa, watoto kubakwa, kulawitiwa, kufanyishwa kazi
licha ya kuwa na umri mdogo na vitendo vingine vinavyokwenda kinyume cha sheria
na haki za msingi za binadamu,” alisema Chacha.
Kwa upande wake mwenyekiti wa (PWMO) Mwamvua Mwinyi alisema
kuwa lengo la kuanzishwa chama hicho mbali ya kutetea haki za waandishi
wanawake pia ni kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya mkoa
huo na Tanzania kwa ujumla.
“Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka siku
hadi siku kutokana na baadhi ya wanajamii hususani wanawake kutokuwa katika
kutoa taarifa za vitendo hivyo hali inayofanya kuongezeka kwa ukatili wa
kijinsia,” alisema Mwinyi.
Aliiomba jamii kwa kushirikiana na vyombo vya sheria kwa
kutoaa taarifa juu ya watu wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili hususani maeneo
ya pembezoni mwa miji, chama hicho kilianzishwa mwaka jana na kina jumla ya
wanachama 15.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment