Tuesday, August 26, 2014

Na John Gagarini, Kibaha
RAIA wa nchi ya Ethiopia Dawita Alalo (25) amekufa alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye kituo cha afya cha Chalinze kata ya Bwiringu wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Marehemu alikuwa ni kati ya raia 48 wa nchi hiyo walikamatwa wakiwa kwenye msitu wa kijiji cha Visakazi Ubena Zomozi tarafa ya Chalinze Agosti 22 mwaka huu, baada ya kuingia nchini bila ya kibali.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kaimu kamanda wa polisi mkoani humo Mrakibu Mwandamizi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa marehemu ni miongoni mwa wahamiaji haramu 11 waliokuwa wamelazwa kituoni hapo wakipatiwa matibabu.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 26 majira saa 7:30 usiku alipokuwa akipatiwa matibabu kituoni hapo baada ya kuugua ugonjwa wa malaria.
Wakati huo huo mlinzi wa baa ya Silent Inn Jamat Mandama (55) amefariki dunia baada ya kunywa pombe nyingi bila ya kula chakula.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27 mwaka huu majira ya saa 1 usiku huko Umwe kata ya Ikwiri wilayani Rufiji.
Aidha alisema kuwa mlinzi huyo alikutwa amekufa akiwa lindoni kwenye baa hiyo.
Na John Gagarini, Kibaha
ASKARI sita wa jeshi la polisi mkoani Pwani wamenusurika kifo kutokana na ajali ya barabarani baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongwa na lori la mizigo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kaimu kamanda wa polisi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa askari hao walikuwa doria.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 26 majira ya saa 9:30 usiku eneo la Maili Moja Ujenzi wailayani Kibaha barabara kuu ya Dar es Salaam Chalinze.
Alisema kuwa gari hilo lenye usajili namba PT 2012 lilikuwa likiingia kwenye kituo cha mafuta cha Delina na kugongwa na lori hilo lenye namba za usajili T 927 CAU na tela namba T 769 CJX.
“Lori hilo bada ya kuligonga gari hilo lapolisi kwa nyuma likaenda kugongana na lori lingine lililokuwa likielekea Jijini Dar es Salaam lenye namba T 672 BAC lenye tela namba T 672 BBW,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alibainisha kuwa askari watatu walijeruhiwa vibaya ambao ni namba F 4333 DC Tamimu ambaye amevunjika mguu wa kulia mara mbili, WP 6100 DC Jaqline ambaye amejeruhiwa kichwani na H 3348 DC Armand ambaye amejeruhiwa kichwani na kifuani.
“Askari wote wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kwa matibabu zaidi ambapo tunaendelea kumtafuta dereva wa lori lililosababisha ajali hiyo,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Mwisho.

   

No comments:

Post a Comment