Thursday, August 28, 2014

RT YATAKIWA KUANDAA MKUTANO WA KATIBA

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Riadha Tanzania (RT) kimetakiwa kiandae mkutano mkuu wa chama ili kupitia rasimu ya katiba baada ya mkutano kama huo kuahirishwa Juni na kutakiwa kufanyika Novemba mwaka jana lakini hadi sasa hakuna taarifa ya kufanyika mkutano kama huo .
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mwenyekiti wa chama cha riadha mkoa wa Pwani (CRAA) Joseph Luhende alisema kuwa baada ya kushindikana kufanyika kwa mkutano kwa ajili ya kupitisha rasimu hiyo huko mkoani Morogoro iliamuliwa kuwa mkutano kama huo ufanyike lakini hadi sasa imekuwa kimya.
Luhende alisema kuwa upitishaji wa rasimu ya chama ilishindikana kutokan na kuchelewa hivyo kupangwa Novemba mwaka jana na hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya kufanyika mkutano kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo.
“Mbali ya kushindikana kupitishwa kwa rasimu ya katiba hiyo pia vyama vilitakiwa visitumie katiba ya zamani na tulivyouliza tuliambiwa kuwa tusubiri na sasa inakaribia kufika mwaka lakini hakuna lolote linaloendelea hali ambayo inakatisha tamaa,” alisema Luhende.
Alisema mchezo wa riadha unakumbwa na changamoto nyingi hivyo rasimu hiyo ingepitishwa ingesaidia kuboresha riadha lakini utekelezaji umekuwa mgumu na rasimu ndiyo inayopelekea kupata katiba ambayo ni kila kitu sawa na dira ya mwelekeo wa mchezo huo.
“Utendaji kazi unakuwa mgumu kutokana na kutakiwa tusitumie katiba ya zamani hivyo ni vema rasimu hiyo ikapitishwa ili tuweze kupata katiba mpya ambayo itatuongoza,” alisema Luhende.
Aidha alisema kuwa kutokana na mipango ya RT kutokuwa mizuri kumechangia nchi kufanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa mfano ile ya Olimpiki ambapo Tanzania iliambulia patupu kwenye mchezo huo na kuwataka viongozi wa shirikisho hilo kuwa makini katika kutekeleza majukumua yao.
Akijibu kuhusiana na suala hilo kwa njia ya simu katibu mkuu wa RT Suleiman Nyambui alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa fedha ndiyo inapelekea wao kushindwa kuandaa mkutano mkuu wa kupitisha rasimu hiyo ya katiba ili kupata katiba mpya.
“Tunaendelea kuwasiliana na wafadhili mbalimbali ili tuweze kupata fedha kwa ajili ya kuandaa mkutano huo wa kupata katiba ambayo itaongoza chama baada ya mkutano wa awali kushindwa kuendelea baada ya viongozi wa mikoa ambao walisema hawajaisoma vizuri hivyo ikashindika kuijadili rasimu hiyo,” alisema Nyambui.
Nyambui alisema walipeleka katiba mikoani kwa ajili ya wao kutoa mapendekezo lakini hawakuweza kuyapeleka ambapo ni mikoa mitatu tu ndiyo iliyotoa mapendekezo yake  ambayo ni Dar es Salaam, Arusha na Dodoma huku mingine ikiwa bado.
“Tunatarajia kuitisha mkutano mkuu kabla ya mwaka haujaisha ili kukamilisha zoezi la kupata katiba baada ya marekebisho kufanyika kwenye mkutano na kikwazo kikuu ni ukosefu wa fedha,” alisema Nyambui.
Mwisho.



No comments:

Post a Comment