Na John Gagarini, Kibaha
JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoa wa
Pwani imeiomba serikali kuangalia upya mfumo wa mashine za risiti za Kieletroniki
(EFD) ili itambue gharama za manunuzi ya bidhaa.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na mwenyekiti wa
Jumuiya hiyo mkoani hapa Abdala Ndauka na kusema kuwa mashine hiyo inatambua
ulichouza tu na haitambui gharama zingine.
Ndauka alisema kuwa wafanyabiashara hao hawana
tatizo la kununua mashine hizo kwani wao ni wazalendo na wana nia ya kuchangia
mapato ya serikali.
“Changamoto yetu kubwa ni gharama zingine na sisi
tuko tayari kuzinunua mashine hizo ila serikali ingeweka mfumo wa kutambua
gharama nyingine ili kuwe na unafuu,” alisema Ndauka.
Alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanafanya
biashara zao kwa njia ya mikopo na mitaji yao ni midogo hivyo ni vema ingeweka
mazingira ya kujua na gharama za manunuzi ya bidhaa na gharama za uendeshaji.
“Mashine hizo zinauzwa kati ya shilingi 800,000 na
600,000 kutegemeana na biashara kwa mfanyabiashara mchanga au mwenye mtaji
mdogo hawezi kumudu kuinunua,” alisema Ndauka.
Aidha alisema kuwa walifanya kikao na Naibu Waziri
wa Fedha Mwigulu Nchemba huko Dodoma ambapo walikubaliana kuwa wafanyabiashara
wasifungiwe maduka huku majadiliano yakiendelea.
“Makubaliano na Waziri huko Dodoma yamekiukwa kwani
hata kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aliwaambia watendaji mikoani
kutoyafunga maduka kutokana na kukosa mashine hizo lakini wanashangaa mkoa wa
Pwani maduka yanafungwa na mamlaka hiyo,” alisema Ndauka.
Akizungumzia suala hilo ofisini kwake, meneja wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Pwani, Highness Chacky, alisema kuwa mashine hizo
ni muhimu kwa ajili ya malipo sahihi na wao kutunza kumbukumbu za biashara zao.
Chacky alisema hiyo ni awamu ya pili ambayo inahusisha
wafanyabiashara ambao mapato yao kwa mwaka ni kuanzi kiasi cha shilingi milioni
14 hadi 39 kwa mwaka na biashara ambazo
zilikuwa na misamaha ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
“Mashine zina bei totauti kutegemeana na biashara ni kati ya
shilingi 800,000 na 600,000 ni mali yao na serikali haina hela za kuweza
kuwanunulia mashine hizo lakini wakishazinunua fedha zao zitarejeshwa kwa
kutolipia kodi ambazo wanakuwa wamekadiriwa kwa mwaka hadi pale hela yao
itakapokuwa imekwisha na baada ya hapo wataendelea kulipa kodi,” alisema Chacky.
Alisema kuwa wanaweza kulipia mashine hizo kwa awamu toka kwa
mawakala wa mashine hizo hadi pale watakapomaliza na kukabidhiwa mashine na si
kufanya mgomo kwani ni kuwanyima haki wateja na kusema kuwa hajapata barua
yoyote ya kuitaka TRA isitishe zoezi hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment