Saturday, September 20, 2014

KINANA AIBUA MAKUBWA KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amezishauri Halmashauri nchini kulipatia Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) viwanja bure ili liweze kujenga nyumba kwa bei nafauu ambazo wananchi wa hali ya chini wataweza kuzinunua.
Aliyasema hayo jana mjini Kibaha kwenye mkutano wa hadhara pamoja na kukabidhiwa mashine rahisi za kufyatulia matofali kwa vijana wa mkoa wa Pwani kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani hapa.
Kinana alisema kuwa tatizo la ukosefu wa nyumba za kuishi ni kubwa hasa kwenye miji hivyo endapo NHC ingejenga nyumba nyingi ingesaidia wananchi kuweze kununua nyumba hizo kwa bei nafuu au kupangisha kwa gharama ndogo.
“Nawapongeza NHC kwa kufanya mageuzi makubwa ya ajira kwa kuwasaidia vijana pia kwa kuwapatia mashine hizi ambazo zitakuwa ni mkombozi kwao kwani mbali ya kujiongezea kipato pia wataweza kujenga nyumba kwa gharama nafuu na za kisasa,” alisema Kinana.
Alisema haya ni mapinduzi makubwa na mapya kwenye Taifa ambalo liko kwenye kazi kubwa ya kuhakikisha vijana wanapata ajira kwani mashine hizo zitawazalishia fedha na kuleta mabadiliko kwenye sekta ya ujenzi hapa nchini na kufanya gharama za nyumba kushuka.
Akimkabidhi mashine hizo meneja wa NHC Paulina Mrango alisema kuwa wameamua kutoa mashine hizo kwa lengo la kuisaidia serikali kukabiliana na uhaba wa ajira pia kufanya ujenzi kwa gharama nafuu.
Mrango alisema kuwa wametoa mashine 28 kwa vikundi vya vijana kwenye Halmashauri zote za mkoa wa Pwani ambapo mpango huo utakuwa kwa nchi nzima ili kufanikisha ufyatuaji wa matofali ya kisasa kwa kutumia gharama ndogo ya malighafi.
“Tumetoa mashine hizo 28 zenye thamani ya shilingi milioni 12.6 kwa Halmashauri na tutazipatia fedha kiasi cha shilingi 500,000 kama mtaji wa kuwakopesha wanavikundi hao ambapo vikundi vitakavyopewa mashine hizi vitapatiwa mafunzo ya wiki mbili na wakufunzi kutoka VETA ili wajue namna ya kuzitumia,” alisema Mrango.
Aidha alisema kuwa mbali ya tofali hizo kuwa za gharama nafuu pia itasaidia utunzaji wa mazingira kwani maeneo ya vijijini wengi wanatumia tofali za kuchoma ambazo zinachomwa kw akutumia kuni zinazotokana na miti hivyo kuharibu mazingira.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SHIRIKISHO la Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba serikali kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu na wazee wanapata dawa wanazoandikiwa na daktari mara waendapo hospitalini.
Akiuliza swali mbele ya katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana kwenye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake mkoani humo, mwenyekiti wa shirikisho hilo Ally Mkanga alisema kuwa wamekuwa wakinyimwa dawa na kutakiwa kwenda kununua kwenye maduka ya dawa.
Mkanga alisema kuwa sera inasema kuwa wazee, watoto chini ya miaka mitano na wanawake wanaojifungua huduma ni bure lakini hupaswa kununua pia mbali ya kutakiwa kulipia dawa  kwenye mahospitali hazipatikani na kutakiwa kununua kwenye maduka hayo.
“Tunaiomba serikali ihakikishe sera zake za matibabu bure kwa makundi yanayopaswa kutolipia dawa hayalipishwi kwani inakuwa changamoto kubwa kwao hasa wazee na watu wenye ulemavu,” alisema Mkanga.
Alisema watu wenye ulemavu wanapata shida wanapokwenda hospitali kwani mazingira kwao si rafiki hivyo wameiomba serikali kuhakikisha inaweka mazingira rafiki kwa wao kupata huduma za afya.
Akijibu swali hilo mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa ni kweli kuna changamoto hizo lakini wameweka madirishwa kwa ajili ya wa wazee kwenye hospitali ya wilaya ya Mkoani lakini tatizo dawa wanazopewa ni za hadhi ya kituo cha afya.
“Kituo cha afya cha Mkoani kilipandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya lakini mgao wake wa dawa inapata kama kituo cha afya na si hospitali ya wilaya jambo ambalo ni changamoto kubwa hasa ikizingatiwa Hospitali ya Tumbi imepandishwa hadhi  na kuwa mkoa ya Rufaa ambapo wagonjwa wote wanatakiwa waanzie hapa hivyo kumekuwa na mlundikano mkubwa wa wagonjwa,” alisema Kihemba.
Kihemba alibainisha pia katika kukabiliana na tatizo la dawa kwenye mahospitali wameunda kamati ya dawa ili kuhakikisha inafuatilia suala la upatikanaji wa dawa na kutolewa kwa utaratibu unaotakiwa ili kuondoa malalamiko kwa wagonjwa wanaopata huduma kwenye halmashauri ya wilaya.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wadogo wilayani Kibaha mkoani Pwani wameilalamikia Halmashauri ya wilaya ya Kibaha kwa kuwalipisha kodi na ushuru mkubwa na kuwa mzigo mkubwa kwao hivyo kushindwa kufanya biashara.
Akiuliza swali mbele ya katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa hadhara ambao ulifanyika kwenye uwanja wa Bwawani wa Bwawani Maili Moja wilayani Kibaha, mwenyekiti wa soko la Maili Moja Ally Gonzi alisema wamekuwa wakilipa kodi nyingi.
Gonzi alisema kuwa halmashauri hiyo imekuwa ikiwatoza kodi na ushuru mbalimbali na kuwa kero kwa wafanyabiashara wadogo kwenye soko na maeneo mengine ya mji huo na kuwafanya wawe kwenye wakati mgumu wa kufanya biashara zao.
“Tunaiomba serikali itupunguzie mzigo wa kodi kwa ni nyingi na wengine biashara zao ni ndogondogo na za mkopo lakini tunabanwa tulipie tunajikuta mitaji inakufa kutokana na kodi hizo ambazo ni kubwa kuanzia 50,000 na hadi zaidi ya 100,000 hivyo tunashindwa kujikwamua kwenye hali ngumu,” alisema Gonzi.
Aidha alisema kuwa  Halmashauri imekuwa ikitumia nguvu kubwa kwa kutumia askari wenye silaha au mgambo wakati wa kuja kuchukua kodi kwa wafanyabiashara ambao wanajitafutia riziki za familia zao.     
Kwa upande wake  Kinana alizitaka Halmashauri nchini kupunguza kodi ambazo ni kero kwa wananchi pia ziwashirikishe wafanyabiashara kabla ya kuzipitisha kwani baadhi yao wanatafuta hela za kula tu.
Kinana alisema kuwa miaka michache iliyopita serikali ilifuta kodi ambazo zilikuwa kero lakini kodi hizo zimerudi mlango wa nyuma na kuwafanya wafanyabiashara wadogo wazilalamikie kwani zimekuwa mzigo mkubwa kwao.
“Hawa wanajitafutia fedha kwa ajili ya familia ili wapate chakula na riziki hivyo lazima halmashauri zifikirie upya suala la kodi kuwa nyingi kwa wafanyabiashara wadogo kutokana na hali hii nitaongea na wabunge wa CCM ili kuondoa kodi ambazo ni mzigo kwa wafanyabiashara wadogo,” alisema Kinana.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Adhu Mkomambo alisema kuwa wao kama Halmashauri watakaa kuangalia namna ya kurekebisha kodi na ushuru mbalimbali ili kuondoa kero hizo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WALINZI wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wameulalamikia uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kushindwa kuwaajiri kwa kipindi cha  miaka 10 sasa.
Akizungmza kwa niaba ya wenzake mbela ya katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana kwenye mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Bwawani wilayani Kibaha mkoani Pwani, Jafar Mtimbuka alisema kuwa amefanya kazi kwa kipindi cha miaka 10 bila ya kuajiriwa huku akiwa kama kibarua.
Mtimbuka alisema kuwa wamefanya kazi kama vibarua kwa kipindi hicho pasipo kuajiriwa na kuambiwa kuwa hawana sifa jambo ambalo si la kweli kwani baadhi yao wamehitimu mafunzo ya mgambo na wengine Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Katibu hata kama nitafukuzwa kazi sawa lakini tunaomba utusaidie kwani tumefanyakazi muda mrefu kama vibarua bila ya ajira wanasema hatuna sifa wakati mimi nimehitimu mafunzo ya JKT nashangaa wanasema kuwa hatuna sifa,” alisema Mtimbuka.
Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri hiyo Jenifa Omolo alipotakiwa kujibu suala hilo alisema kuwa analifahamu suala hilo lakini walinzi hao hawana sifa na halmashauri haikuwa na utaratibu wa kuajiri kada hizo zikiwemo zile za chini.
Omolo alisema kuwa kwa sasa wamepata kibali kwa ajili ya kuajiri kada za chini wakiwemo walinzi na wengine hivyo kama watakuwa na sifa wataajiriwa kulingana na uwezo wao.
Naye katibu Mkuu Kinana alisema kuwa mtu kafanya kazi miaka 10 anaambiwa hana sifa jambo ambalo halipendezi inabidi waangaliwe na wanastahili kuajiriwa kama wafanyakazi wengine.
“Mwenye sifa aajiriwe na huyu wa miaka 10 ana haki ya kuajiriwa haiwezekani mseme hana sifa kwa miaka hiyo aliyofanyakazi kwani sheria ni miezi mitatu na amefanyiwa vibaya si haki,” alisema Kinana.
Kinana alisema kuwa mlinzi huyo aajiriwe na fedha zake za utumishi kwa kipindi hicho ziunganishwe kwenye mafao yake wakati wa kustaafu kwenye pensheni yake.
Mwisho.      
        
     

      

No comments:

Post a Comment