Sunday, September 21, 2014

MAJAMBAZI YAVAMIA YAUA YAJERUHI

Na Mwandishi Wetu, Kibaha

WATU wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wanatuhumiwa kumwua mtu mmoja mwenye umri kati ya miaka (35) na (40) ambaye jina lake halikuweza kufahamika na kumjeruhi mwingine baada ya kufanya tukio la uhalifu kwenye maduka yaliyopo kwenye stendi ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani jirani na kituo cha polisi.

Kutokana na tukio hilo Jeshi la polisi Mkoani Pwani linawatafuta watu hao ambao walikuwa na bunduki hao ambao walivamia duka liitwalo Bahati mali ya Hashim Kisaka na ofisi ya kukatia tiketi ya mabasi yaendayo mikoani kisha kupora fedha kwenye maduka hayo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa polisi mkoani
humo Athumani Mwambalasa alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 2 kasoro usiku Septemba 20 mwaka huu.

“Watu hao walivamia katika maeneo hayo wakiwa na silaha ambayo bado haijafahamika na kumuua mtu huyo kwa kumpiga na risasi ya kifuani kisha kumjeruhi mguuni  mfanyabishara wa korosho Ambwene Mwambungu wakati wa tukio hilo ambalo lilifanyika huku umeme ukiwa umekatika na hali iliyofanya kukawa na giza nene na watu hao kutumia mwanya huo kutekeleza tukio hilo,” alisema Kamanda Mwambalaswa.

Kamanda Mwambalasa alielezea kuwa kwenye tukio hilo watu hao wakiwa na silaha hiyo walivamia katika maduka hayo na kuanza
kupiga risasi hewani hali iliyowafanya watu waliokuwa katika eneo hilo kukimbia hovyo huku wakiacha mali zao kuhofia usalama wao kisha kupora fedha na mali ambayo thamani yake bado haijafahamika.

“Marehemu alifikwa na mauti wakati akipelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani ya Tumbi  huku majeruhi wa tukio hilo bado amelazwa akipatiwa matibabu kutokana na majeraha ya mguu aliyoyapata,” alisema Kamanda Mwambalaswa.


Aliwataka wananchi kushirikiana kwa pamoja kutoa taarifa mara moja watakapobaini walipo watu hao pia kutoa taarifa  mara wanapohisi watu wasioeleweka katika maeneo yao.

Mwisho

No comments:

Post a Comment