Na John Gagarini, Kibaha
HATIMAYE mkoa wa Pwani umetoa tamko la kuzizuia Halmashauri
za mkoa huo kuendelea kutoza ushuru wa hoteli na nyumba za kulala wageni ambao
ulifutwa na bunge mwaka 2009 huku Halmashauri ya mji wa Kibaha ikiwa inaendelea
kuutoza na kusababisha malalamiko ya wafanyabiashara hao.
Kufuatia halmashauri hiyo kuendelea kutoza ushuru huo kupitia
umoja wao Wamiliki wa Hoteli wilayani Kibaha mkoani Pwani (UGEHOKI) walipeleka
malalamiko yao ofisi ya katibu tawala wa mkoa huo kupinga kutozwa ushuruhuo wa
asilimia 20.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo Mhandisi Michael Mrema, alisema kuwa
halmashauri zote zilipewa miongozo kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
juu ya kusitisha utozaji huo hadi watakapopewa utartibu mwingine wa ukusanyaji.
“Tulipokea barua toka kwa wamiliki hao juu ya kulalamikia
ushuruhu huo ambao ulisitishwa wakati wizara zinazohusika zitakapokuwa zimeweka
utaratibu mwingine wa namna ya ukusanyaji wa ushuru huo ambao ulilalamikiwa na
wamiliki hao kuwa ni mkubwa sana,” alisema Mrema.
Mrema alisema kuwa barua hiyo toka TAMISEMI ya kusitisha
ushuru huo yenye kumbukumbu namba Na. FA 2/266/01/10 ya Mei ya mwaka 2014 kwa
halmashauri zote nchini ambayo ilitokana na barua yenye kumbukumbu Na.
CE.325/387/03/47 ya tarehe 16 ya mwezi wa Aprili mwaka 2014 iliyotoa uafafanuzi
zaidi.
“Katika ufafanuzi TAMISEMI ilisema kuwa ushuru wa nyumba za
kulala wageni umeainishwa katika sheria ya fedha sura 290 kifungu cha 6(1)(q)
na 7(1)(u) na kwamba awali ushuru huo ulikuwa ukitozwa kupitia sheria ya hoteli
sura 105 ambayo imefutwa baada ya kutungwa sheria mpya sheria ya Utalii na 29
ya mwaka 2008 na kuanza kutumika rasmi Julai Mosi 2009 baada ya kutangazwa
kwenye gazeti la serikali namba 212 la tarehe 1 Julai 2009 ni wazi kuendelea
kutozwa ni kukiuka sheria za Utalii,” alisema Mrema.
Aidha Mrema alisema kutokana na barua hizo Halmashauri
zilipaswa kutoendelea kutoza ushuru huo hivyo hazipaswi kuendelea kuutoza na
zikiendelea kutoza kunaweza kusababisha halmashauri na watoa huduma hao ni kusababisha migogoro mikubwa ya
kisheria na kwa sasa wizara za TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Wizara ya Maliasili
na Utalii zipo katika majadiliano ya kuamua namna bora ya kurejesha ushuru huo.
Alizitaka halmashauri hizo kutekeleza agizo hilo na maagizo
mengine yanayotoka ngazi za juu ili kuepusha migogoro na watoa huduma na
wananchi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato mbalimbali.
No comments:
Post a Comment