Na John Gagarini, Kibaha
UTINGO wa lori la mizigo Adam Rashid (28) mkazi wa Bwiringu
kata ya Pera wilaya ya Bagamoyo amekufa baada ya lori alilokuwa akisafiria
kugongana na lori lingine
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa polisi
mkoani humo Mrakibu Msaidizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa
malori hayo yaligongana uso kwa uso.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti
19 mwaka huu majira ya saa 10 jioni eneo la Sweet Corner.
“Marehemu alikuwa kwenye gari namba T 650 BED aina ya Fuso
lililokuwa likiendeshwa na na Ramadhan Mwarami (40) mkazi wa Bwiringu likiwa
limebeba simenti likitokea Jijini Dar es Salaam kwenda Chalinze,” alisema
Kamanda Mwambalaswa.
Alisema kuwa lori alilokuwa amepanda marehemu liligongana na
lori lenye namba za usajili T 853 APA aina ya Fuso ambalo lilikuwa likitokea
mkoani Mbeya kwenda Dar es Salaam likiwa limebeba Mahindi likiendeshwa na Shan
Iddi (28) mkazi wa Mwanga liligongana na lori hilo na kusababisha kifo hicho.
Aidha alisema kuwa dereva wa lori alilokuwa amepanda marehemu
aliumia kidogo ambapo marehemu alifariki dunia wakati akipata matibabu kwenye
hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani ya Tumbi.
Wakati huo huo Ofisa Mwandamizi wa jeshi hilo anayeshughulikia
majalada ya kesi katika ofisi ya mkurugenzi wa makosa ya jinai (DCI) Ilembo amenusurika kifo baada ya gari
alilokuwa akisafiria kugonga mti.
Akifafanua kuhusiana na tukio hilo Kamanda Mwambalaswa
alisema kuwa ofisa huyo alikuwa akitokea mkoani Iringa kikazi.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 20 mwaka huu majira
ya saa 9 alfajiri eneo la Vigwaza kata ya Pera wilayani Bagamoyo.
“Chanzo cha ajali hiyo ni gari hilo la polisi kutaka
kugongana uso kwa uso na gari lingine baada ya kulipita gari lililokuwa mbele
yao na alipotokeza akakutana na hilo gari hali iliyofanya dereva akwepe kisha
kuserereka kwenye mtaro na baadaye kugonga mti,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa gari hilo lilipasuka matairi
na vioo vilivunjika ambapo gari lililohusika na tukio hilo halikuweza kusimama
mara baada ya tukio hilo
Mwisho.
No comments:
Post a Comment