JESHI la Polisi mkoani Pwani limekanusha uvumi ulioenea na
kudai kuwa mkazi wa Kijiji cha Dondo wilaya ya Mkuranga Hamis Mahimbwa (20)
kuwa amekufa kwa kuchunwa ngozi mwili mzima ila ni kutokana na kuungua na moto.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini
Kibaha kaimu kamanda wa Polisi mkoani humo mrakibu Msaidizi wa Polisi (SSP)
Athuman Mwambalaswa amesema kuwa hakuna tukio kama hilo mkoani hapo.
Akifafanua juu ya tukio la mtu huyo kufa amesema kuwa mnamo
Agosti 6 mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku huko katika kijiji cha Dondo Tutani
kata ya Kisiju wilayani humo Hamis Mahimbwa (27) alikutwa na wananchi akiwa
ameungua moto mwili mzima.
Kamanda Mwambalaswa amesema marehemu alipiga kelele kuomba
msaada baada ya kuungua na moto na kumchukua na kumpeleka hospitali kwenye
kituo cha afya cha Kalole Kisiju na kuanza kupatiwa matibabu lakini kutokana na
kuungua sana na moto alifariki dunia Agosti 7 mwaka huu majira ya saa 11:00
alfajiri.
Amesema kuwa baada ya kifo hicho ilipelekwa taarifa kwenye
kituo cha polisi cha Mkuranga na jalada la uchunguzi MKU/IR/1202/2014
lilifunguliwa ili kubaini kifo chake.
Amebainisha kuwa baada ya kufunguliwa jalada hilo Ofisa
Mpelelezi Mkuu wa Polisi wa makosa ya Jinai wa wilaya akiwa na timu ya askari
wa upelelezi waliungana na maofisa wa usalama waliungana na Daktari wa wilaya
ya Mkuranga Kibela kwenda kwenye eneo la tukio na kituo cha afya cha Kisiju kwa
uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
Aidha amesema kuwa daktari alichukua sampuli ya ngozi ambapo
kwenye eneo la tukio ilikutwa suruali, majivu ya tisheti aliyokuwa amevaa,
kandambili, kibiriti, chupa ya plastiki ya soda ambayo ilikuwa na mafuta ya
petroli na katika eneo hilo hakukuwa na purukushani ya watu wengi ambapo
mashahidi waliokwenda kumsaidia alipopiga kelele walimkuta marehemu akiwa
anongea na kudai kuwa ameungua kwa moto bila ya kusema aliye muunguza.
Kaimu kamanda wa polisi huyo wa mkoa wa Pwani amesema baba
mlezi wa marehemu Athuman Mahimbwa alipohojiwa alisema kuwa mwanae alikuwa
akiugua ugonjwa wa Kifafa kwa miaka 17 na alimwambia kuwa anakufa kwa kuungua
na moto na kutokana na uchunguzi uliofanywa na polisi pamoja na daktari
umebainisha kuwa kifo chake kimesababishwa na moto na si kuchunwa ngozi.
No comments:
Post a Comment