Na John Gagarini, Kibaha
MWANARIADHA John Mwandu wa mkoani Pwani amewaomba wadau
mbalimbali kujitokeza kumsaidia kwa hali na mali ili aweze kwenda kambini Eldoret
nchini Kenya kwenye kambi aliyotokea mkimbiaji maarufu duniani David Rudisha wa
nchi hiyo.
Rudisha ambaye ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 amekuwa
akiwandaa vijana wengi wa nchi ya Kenya kwa ajili ya kuinua vipaji vya vijana
ambapo Mwandu ameomba kujiunga na kambi hiyo na tayari amekubaliwa kujiunga
nayo kwa ajili ya mazoezi yam bio za mita 1,500.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha Mwandu
alisema kuwa tayari ameruhusiwa kwenda kwenye kambi hiyo kwa mwaka mmoja lengo
kubwa likiwa ni kujiandaa na mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2016 yatakayofanyika
Rio de Janeiro nchini Brazil.
“Lengo langu la kwenda
Kenya ni kujifunza mbinu wanazozitumia katika mchezo huo na kuwafanya kuwa
mabingwa wa dunia wa riadha, kwani Mungu akipenda Olimpiki ijayo nitahakikisha
naiwakilisha nchi yangu na kuiletea medali kwani inawezekana na diyo sababu ya
kuanza maandalizi mapema,” alisema Mwandu.
Alisema anatarajia kwenda huko mwezi Desemba mwaka huu kwa
ajili ya kambi hiyo ambayo ni nzuri na imetoa wakimbiaji wengi na ana uhakika
akifanikiwa kwenda huko atarudi akiwa na mbinu nyingi za ukimbiaji ambazo
anaamini zitamfanya aweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali.
“Changamoto kubwa niliyonayo ni ukosefu wa fedha za kuweza kunipeleka
kwenye kambi hiyo lakini naamini Mungu ataniwezesha kuweza kufanikisha kwenda
kwenye kambi hiyo ambapo tayari nimeshafanya mawasiliano na Rudisha na ameahidi
kunisaidia,” alisema Mwandu.
Aidha alisema kuwa Tanzania inashindwa kufanya vizuri kwenye
michuano ya kimataifa kutokana na wachezaji wanaochaguliwa hawana uwezo na
huchaguliwa kwa upendeleo na wale wenye uwezo kuachwa hali ianayosababisha
kutofanya vizuri.
Alibainisha kuwa aliwahi kushinda kwenye mbio za Afrika
Mashariki chini ya miaka 17 akiwa anasoma Tegeta High School alikuwa wa pili, Tabora
Marathon kilomita 21, mashindano ya Voda Com kilomita tano ambapo alishika
nafasi ya pili na Ruaha Marathon kilomita sita ambapo alishika nafasi ya tatu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment