Thursday, August 14, 2014

DEREVA TEXI ALIYEPOTEA SIKU 8 AKUTWA AMEKUFA

Na John Gagarini, Kibaha
BAADA ya dereva wa Texi Richard Ponera (36) mkazi wa Mwendapole wilayani Kibaha mkoani Pwani kupotea kwa siku nane amepatikana akiwa ameuwawa  na kuporwa gari alilokuwa akiliendesha.
Marehemu ambaye alikuwa akifanyia shughuli zake kwenye kituo kikuu cha Mabasi cha Maili Moja wilayani humo alipotea Agosti 6 Mwaka huu majira ya saa 1 usiku alipokodishwa na watu wawili wasio fahamika waliojifanya kuwa ni wateja.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo Mrakibu Msaidizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa mwili wake ulitupwa vichakani.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa huko eneo la Mihande Mashambani Mlandizi wilayani Kibaha ukiwa umeharibika vibaya huku gari  alilokuwa akiendesha lenye namba za usajili T 905 BHT aina ya Corolla nyeupe.
“Chanzo cha mauaji hayo ni katika kuwania mali ambayo ni gari hilo ambalo halijapatikana na hakuna mtu ambaye amekamatwa hadi sasa na bado uchunguzi unaendelea kuwatafuta watu waliohusika na tukio hilo,” alisema Mwambalaswa.
Alisema kuwa jeshi hilo linaendelea kufuatilia juu ya tukio hilo na halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria watu waliohusika na tukio hilo la kusikitisha, marehemu alizikwa juzi na ameacha watoto wawili ambao ni Ruben (14) anayesoma kidato cha kwanza St Anne na Kontrada anayesoma darasa la sita shule ya Msingi Jitegemee Jijini Dar es Salaam.

Mwisho. 

No comments:

Post a Comment