Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI nane wa kitongoji cha Benki kata ya Igunga wilaya ya
Igunga mkoani Tabora wameiomba Halmashauri ya wilaya kuwalipa fidia ya mashamba
yao ambayo yamechukuliwa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya upanuzi wa hospitali
ya wilaya.
Wakazi hao walitoa ombi hilo kufuatia Halmashauri hiyo kuwa kimya
kwa muda mrefu baada ya mashamba yao kuchukuliwa tangu mwaka 2010 nakufanyiwa
tathmini mwezi Februari mwaka huu lakini hadi sasa bado hawajalipwa fidia za
maeneo yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Kibaha mwenyekiti
wa kamati ya waathirika hao Daniel
Shamalatu alisema kuwa mashamba yao yana ukubwa wa zaidi ya hekari 24 ambazo
zilichukuliwa kwa ajili ya upanuzi huo wa hospitali ya wilaya.
Shamalatu alisema kuwa maeno yao yalichukuliwa bila ya wao
kupewa taarifa ambapo mazao yao waliyokuwa wameyapanda yalifyekwa na ujenzi
kuanza bila ya kupewa fidia.
“Tulipoona kimya tulikwenda mahakamani ili tuweze kulipwa
fidia zetu lakini baraza la madiwani liliingilia kati na kututaka tuondoe kesi
mahakamani ili tukubaliane nje ya mahakama, kweli tuliondoa kesi hiyo
mahakamani lakini hakuna kinachoendelea ambapo sasa ni karibu mwaka umepita
lakini tunaona kimya na tunapofuatilia halmashauri tunaambiwa suala letu
linashughulikiwa,” alisema Shamalatu.
Alisema kuwa wao hawapingi ujenzi huo lakini wanachotaka ni
kulipwa fidia kutokana na ukubwa wa mashamba yao na si kiwanja kimoja kila heka
kama walivyotaka kufanya na pia wanataka kujua malipo yao yatafanyika lini.
Akitolea ufafanuzi
suala hilo kwa njia ya simu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Rustika Turuka alisema
kuwa ni kweli mashamba yao yalichukuliwa kwa ajili ya upanuzi wa hospitali
hivyo kutakiwa kupisha ujenzi huo kufanyika.
Turuka alisema kuwa kwa sasa maeneo hayo tayari
yameshafanyiwa tathmini na taarifa ya uthamini imepelekwa wizarani kwa ajili ya
kuandaliwa malipo baada ya kujua takwimu sahihi kutokana na maeneo hayo na
kiasi ambacho watastahili kulipwa ili halmashauri itenge bajeti kwani maeneo
mengine ambayo yalichukuliwa wamelipwa na wao watalipwa mara taratibu
zitakapokamilika.
“Mthamini toka Tabora alishafika na kufanya kazi hiyo na kwa
sasa tunachokisubiri ni taarifa toka wizarani baada ya kuipitia tathmini hiyo
ili watu wanaodai fidia waweze kulipwa hivyo wanapaswa kuwa na subiri kwani
mambo haya lazima yafuate taratibu na kila mtu atapewa haki zake pia eneo hilo kwa sasa ni mji haipaswi kuwa na mashamba,”
alisema Turuka
Aidha alisema wanasubiri taarifa hiyo ambayo itaonyesha ni
kiasi gani wanastahili kulipwa na ndipo watatafuta fedha hizo kisha kuwalipa watu
ambao wanadai ila wanataka walipwe haraka lakini serikali ina taratibu zake za
kufanya malipo.
“Masuala ya malipo ya fidia za viwanja si suala la haraka
linachukua muda mrefu hivyo lazima wawe na subiri wakati masuala yao
yanashughulikiwa ambapo maeneo mengine tayari wameshalipwa hivyo na wao
wanapaswa kuwa na subira na kila mtu atapata malipo yake,” alisema Turuka.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment