Monday, September 4, 2023

MWENYEKITI WA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA TANZANIA AKUTANA NA UONGOZI MKOA WA IRINGA

 

Picha ikimuonesha Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe akizungumza na uongozi wa jumuiya ya Makambako mkoani Iringa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya jumuiya leo Septemba 4, 2023.

Sunday, September 3, 2023

REHEMA KAWAMBWA ATEULIWA UJUMBE SOKA LA WANAWAKE COREFA

 

REHEMA KAWAMBWA ameteuliwa kushika nafasi ya ujumbe kamati tendaji ya chama cha mpira wa miguu mkoa wa pwani(corefa) kuwakilisha soka la wanawake ya muda kusubiri uchaguzi baada ya mjumbe aliyekuwa anashika nafasi hiyo Faraja Makale  kujiuzulu.

MKE WA MBUNGE KIBAHA MJINI MLEZI CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA PWANI

MKE wa mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka amekubali kuwa mlezi wa Chama Cha Waandishi Wa Habari Wanawake mkoani Pwani, ambapo ameahidi kuwabeba ili kutimiza malengo yao.

Akizungumza na wanachama wa Chama hicho ,ambao alikutana nao kwa mara ya kwanza baada ya kukubali ombi hilo, alieleza waandishi ni kama makundi mengine katika jamii ambayo yanahitaji kujiinua kupitia miradi mbalimbali, biashara na kupitia shughuli zao .

Selina alisema anawaunga mkono waandishi wa habari,na atahakikisha wanajiinua katika Chama chao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

"Nimekubali Kuwa mlezi wenu nachosisitiza ni Umoja, Mshikamano ,msiniangushe, naamini tutafanya mengi ,"Simamieni katiba yenu,shirikianeni katika mambo ya Chama na ya kijamii ,saidianeni na mjiepushe na kukwazana ,kila mmoja aondoe tofauti zake kwa mwenzake na mtafika"alishauri Selina.

Vilevile Selina anawaomba kujiwekea malengo kwa juhudi na mikakati madhubuti, na kwa dhana hiyo ameambatana na Ujumbe kutoka Taasisi ya kifedha ya Azania , ili kuwaunganisha kuweka akiba kwa manufaa Yao.

Nae Neema Masanja na Nuru Athuman maofisa kutoka Taasisi ya kifedha ya Azania Tawi la Tegeta walieleza,ni bank ambayo haina makato ya kumuumiza mtanzania wala mwanamke.

Nuru alifafanua, ni wakati wa akinamama kunufaika na ujio wa akaunti na mkopo mahsusi kwa wanawake ya MWANAMKE HODARI ambapo,riba yake ni nafuu asilimia moja kwa mwezi na haina makato na unafungua akaunti bure.

Awali Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi Wa Habari Wanawake mkoani Pwani, Mwamvua Mwinyi, alimshukuru Mama Koka kwa kukubali ombi hilo la Ulezi.

Alieleza kwamba, Chama hicho ,kimeanza rasmi Michakato ya kuwa chama kamili 2013, kina viongozi wanne,wanachama 15 ,kwa miaka mitano kilisimama kwa muda kujiweka sawa na sasa kimekuja kivingine.

"Ongezeko la vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo kubakwa ,kulawitiwa, mimba za utotoni pamoja na baadhi yao kunyimwa haki ya Elimu ,linaonekana kuwa kubwa, tumekuwa tukishuhudia baadhi ya watoto wakinyimwa haki zao za msingi na wengine kulawitiwa ama kubakwa huku mijibaba iliyohusika kutuhumiwa kutenda vitendo hivyo ikiona ni jambo la kawaida suala ambalo linatakiwa kulipiga vita kwa nguvu zote,pasipo kulifumbia macho hata kidogo " 

Mwamvua anaeleza,masuala hayo ndio yaliyowagusa na kuwashawishi kuanzisha chama ili kuweza kushirikiana na jamii,dawati la jinsia,ustawi wa jamii kwa lengo la kutimiza adhma ya kutokomeza vitendo hivyo.


Saturday, September 2, 2023

WAKAGUZI WA POLISI PWANI WATAKIWA KUWA WATII

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi wa Polisi Pius Lutumo, amefunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa Polisi toka Wilaya zote na vikosi vyake kwa awamu ya pili huku akiwataka wakaguzi hao kuwa na UTII na kwenda kufanya kazi kulingana na viapo vyao, mafunzo hayo ya muda wa miezi miwili yamefungwa Leo katika viwanja vya Polisi Mkoa wa Pwani ambapo Kamanda Lutumo ameelza hategemei kuona Mkaguzi aliyehitimu Leo hii kufanya kazi kinyume na viapo vyao kwenye kuwahudumia wananchi

WATANZANIA WAASWA KUENZI VILIVYOACHWA NA WAASISI WA TAIFA

Katibu wa Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani ndugu Omary Abdull Punzi katika Mahafali ya 22 ya Shule ya msingi Kambarage wilaya Kibaha Mkoani Pwani amewambia wazazi,walimu wanafunzi na wageni waliohudhuria mahafali kulinda vitu vyao vikiwemo vilivyoachwa na waasisi wa Taifa letu.

Punzi amesema kuwa wananchi wanawajibu wa kulinda vya kwao na kufanya matendo yaliyo kuwa mema waliorithishwa na wazee pamoja na kuunga nuhudi za Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kuwa wanapaswa kuwekeza katika idara ya Elimu na maeneo mingine sambamba na hilo aliwaeleza Falsafa mbili za kuwa mzalendo za TA TE TI TO TU na ile ya SA SE SI SO SU Falsafa hizi zinapendwa sana kuzungumzwa na Mheshimiwa Paul Petro Kimiti Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Taifa Mhe Kimiti alishika nafasi mbalimbali serikalini.

Katika Mahafali hiyo Mgeni Rasmi alikuwa Ndugu Festo Issingo Meneja wa benki ya NMB Mkoa wa Pwani alichangia madawati 100 baada ya kuambiwa kuna uhaba wa madawati.

Kwa Upande wa Mkuu wa shule ya Msingi KAMBARAGE alimshukuru Katibu wa Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani na Meneja wa benki ya NMB Mkoa wa Pwani. 

Kwa niaba ya wazazi na walimu walimpendekeza ndugu Omary Abdull Punzi Katibu wa Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa mlezi wa Shule ya Kambarage Nyerere kwa kuwasaidia mawazo ili kufanikisha malengo yao.

Friday, September 1, 2023

WADAU WAOMBWA KUCHANGIA UZIO KUNUSURU WANAFUNZI KUBAKWA

SHULE ya Msingi Mwendapole Wilayani Kibaha imeomba wadau kuisaidia upatikanaji wa fedha kiasi cha shilingi milioni 80 ili kujenga uzio kukabiliana na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanafunzi ikiwemo kubakwa.

Aidha mtu mmoja alihukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa shule hiyo huku wengine wawili kesi zao zikiendelea mahakamani kutokana na tuhuma za kubaka wanafunzi wa shule hiyo.

Hayo yalisemwa na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Rajab Chalamila wakati wa mahafali ya darasa la saba ya shule hiyo ambapo wanahitaji kiasi hicho ili kufanikisha ujenzi wa ukuta wa shule.

Kwa upande wake Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU) LTD Mantawela Hamis alitoa kiasi cha shilingi 100,000 ikiwa ni mchangao wa chama hicho.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya shule Abdulrahman Likunda alisema kuwa wamekuwa wakiihamasisha jamii kuichangia shule hiyo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali shuleni hapo.


Thursday, August 31, 2023

JAMII PWANI YATAKIWA KUWALINDA WATOTO ILI WAISHI KWENYE MAZINGIRA MAZURI

WADAU wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) Mkoani Pwani wameshauriwa jamii kuwalinda watoto ili kuepukana na vitendo vya ukatili.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi wa Anjita Child Development Foundation Janeth Malela wakati wa kikao cha maandalizi ya uzinduzi wa Programu hiyo kwa Mkoa wa Pwani.

Malela alisema kuwa programu hiyo itasaidia kuimarisha ukuaji na maendeleo ya mtoto kikamilifu kimwili, kiakili, kukuza lugha, mawasiliano kijamii na kihisia. 

"Programu inalenga kuimarisha utoaji huduma bora za Afya, Lishe, Malezi yenye Mwitikio, ujifunzaji wa Awali na Ulinzi na Usalama kwa watoto wa miaka 0 hadi 8 na kuimarisha ushirikiano wa wadau wa sekta mbalimbali katika huduma za MMMAM,"alisema Malela.

Aidha alisema kuwa lengo kuu ni kusaidia watoto kwenye masuala ya malezi,makuzi,ujifunzaji,ulinzi wa mtoto,afya ili wakue katika mazingira mazuri na kukua kutokana na sheria zilizopo.

Kwa upande wake ofisa maendeleo ya jamii mkoa wa Pwani Rachel Chuwa alisema kuwa moja ya changamoto wanazozipata watoto ni baadhi ya wazazi na walezi kutowahudumia watoto wao kwa wakati kutokana na kutafuta mahitaji ya nyumbani.

Chuwa alisema kuwa malezi na makuzi wazazi wanapaswa wawahudumie lakini kwa sasa wanalelewa na televisheni na mitandao na suala la lishe shuleni baadhi wanatoa chakuka lakini waengine hawatoi hivyo mpango huo utasaidia kuondoa changamoto zolizopo ili wapate huduma stahiki.

Naye mkurugenzi wa shirika la maendeleo kwa vijana (YPC) Israel Ilunde alisema kuwa mpango huo ni muhimu sana kwani vijana wanakumbana na changamoto za kimaadili kutokana na kutopata malezi bora kutokana na hali ya kimaisha.

Ilunde alisema kuwa mpango huo utasaidia sana katika kuwalea watoto na kuondoa vitendo viovu kutokana na malezi watakayoyapata hivyo rasilimali zitengwe ili kuwalea watoto katika misingi mizuri ya kimaadili.

Mikoa 10 ambayo imeshazindua programu hiyo ni Tabora, Arusha, Morogoro, Rukwa, Manyara, Mbeya, Dodoma, Dar es Salaam, Kagera na Lindi.