Wednesday, August 9, 2023

SERIKALI KUONGEZA UZALISHAJI ZAO LA ALIZETI

Serikali inalenga kuinua uzalishaji wa zao la alizeti na kukuza kipato cha wakulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa Agosti 3, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe.Suleiman Mwenda wakati wa Kongamano na Mafunzo ya wakulima wa zao la alizeti kwenye maonyesho ya nanenane Kanda ya kati katika viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.

Kongamano hilo limelenga kuunga mkono na kutekeleza kwa vitendo Juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuinua na kuthamini mchango wa Kilimo katika Taifa letu. Mafunzo hayo amebebwa na kauli mbiu inayosema ”alizeti kwa afya bora na kipato.

”Tumeshuhudia Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe inayotilia mkazo wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya alizeti ili kupunguza uingizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi na hivyo kupunguza matumizi ya bidhaa za kigeni. Jitihada hizo ni pamoja na kutoa ruzuku za mbegu bora na alizeti na vitendea kazi kwa maafisa ugani “ameeleza Mwenda.

Hata hivyo, Mhe. Mwenda ametoa wito kwa wadau wa kilimo kupeana uzoefu kuhusu mafanikio, changamoto na mkakati ya kuongeza tija ya uzalishaji na masoko ya zao la alizeti kwani sekta ya kilimo na mifugo inachangia uchumi wa nchi kwa zaidi ya asilimia 75 na kwa wananchi wa Dodoma na Singida huku alizeti ikiwa ni zao kuu la biashara katika Mkoa hiyo miwili .

Mhe. Mwenda amezitaja moja ya sababu zinazokabili mnyororo mzima wa zao la alizeti na hivyo kulazimu kuendelea na uingizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kuwataka wadau kutumia Kongamano hilo kuweka mikakati ya kuzipatia ufumbuzi, ambazo ni kiwango kidogo cha uzalishaji, mabadiliko ya tabia ya nchi na masoko ya alizeti yasiyo kuwa na mfumo rasmi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema amewataka wakulima wa Mikoa ya Singida na Dodoma kutumia fursa hiyo waliyoipata kufanya kilimo cha tija na kuacha kilimo cha mazoea kutokana na mafunzo waliyo yapata kuhakikisha wanafanya kwa vitendo kama ilivyo dhamira ya Serikali.

DC ATAKA MADIWANI WATUNGE SHERIA RAFIKI KWA WAWEKEZAJI

MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amewataka madiwani kutunga sheria ndogo ambazo zitaboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na wawekezaji badala ya kuweka mazingira ambayo yatakuwa kikwazo katika ukusanyaji wa mapato.

John aliyasema hayo mjini Kibaha kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Hmashauri ya Mji Kibaha na kuwa wanapaswa kuweka mazingira rafiki badala ya kuwa kero.

Alisema kuwa sheria ndogo ndogo wanazotunga ziwavutie wafanyabiashara na wawekezaji siyo ziwe kero na kusababisha kuwakatisha tamaa badala yake ziwe vichocheo vya watu kufanya uwekezaji.

"Zisiwe kikwazo kuwakwamisha wafanyabiashara na wawekezaji na zisiwaongezee gharama bali ziwe zinzoendana na mpango wa taifa wa wa uboreshaji biashara,"alisema John.

Aidha alisema kuwa gharama za tozo mbalimbali za Halmashauri ziendane na mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha mapato yanapatikana. 

"Mmapaswa kuwa wabunifu katika utendaji kwa kubuni mambo mbalimbali ambayo yataweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwani mazingira yakiwa mazuri yatawavutia na watashiriki katika kukuza uchumi wa nchi,"alisema John.

Aliongeza kuwa wanapaswa kuhasaisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili itoe matokeo kwani ucheleweshaji hauwezi kuonyesha matokeo ya haraka kwa walengwa.

Tuesday, August 8, 2023

KATIBU WA TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYAERERE MKOA WA PWANI ATEMBELEA BANDA LA HIFADHI ZA TAIFA

 



 KATIBU wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa Pwani Ndugu Omary Punzi ametembelea Banda la Hifadhi za Taifa katika Maonyesho ya sikukuu ya wakulima nane nane 8.Agosti 2023 yaliyofanyika mkoani Morogoro Kanda ya Mashariki yakijumuisha mikoa mitatu Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Punzi amesema kitu cha Kujivunia ni kuonana kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mwasisi wa Taifa letu la Tanzania Kutolewa katika idara ya Makumbusho na Kuwekwa katika idara ya Maliasili ya Hifadhi na hii Ndiyo heshima kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chiini ya Uongozi wa Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Kilio hiki Hakika kimesikika Tangu Tarehe 14.5.2022 katika kongamano la Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere Katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete DODOMA Mgeni Rasmi alikuwa Mheshimiwa Kasimu Majaliwa Waziri Mkuu wa Tanzania akiwakilishwa na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda Waziri Mkuu Mstaafu.

Monday, August 7, 2023

BILIONI 157.5 ZATUMIKA UNUNUZI BIDHAA ZA AFYA

 

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa fedha kwa Bohari ya Dawa Tanzania ambapo kiasi cha shilingi bilioni 157.5 kwa mwaka wa fedha 2022/23 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya ikijumuisha Dawa,  Vifaa Tiba na vitendanishi vya Maabara.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania Hassan Ibrahim ambaye ni Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini amesema hayo leo Agost, 7, 2023 Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari alielezea utekelezaji wa majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD) na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/24.

Ibrahim amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23 Bohari imeanza kusambaza Dawa kwa mizunguko mara sita kwa mwaka kutoka Mara nne kwa mwaka huku Akisema serikali imetoa ahadi ya kuipatia MSD mtaji ili kumaliza changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo.

Katika kufanikisha ongezeko la uzalishaji wa bidhaa za afya nchini na kuendana na azma ya Serikali ya uanzishaji wa viwanda, MSD ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha miundombinu ya kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi mkoani Njombe na kuanza uzalishaji ndani ya mwaka huu wa fedha 2023/24. 

Amesema katika mwaka huu wa fedha wa 2023/24, MSD inatarajia Kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuboresho matumizi ya takwimu za maoteo, kuhakikisha bidhaa zote za afya zinakuwa na mikataba ya muda mrefu na kuimarisha ushirikiano na wazalishaji wa ndani kwa kutoa fursa kwa wazalishaji wa ndani na kununua kutoka kwa wazalishaji wa nje pale inapobidi.

Kwa upande wake Michael Bajile Meneja Maoteo Ametoa wito kwa watoa huduma za Afya kuwa makini katika takwimu wanazozikusanya kwani Bohari ya Dawa huzalisha kufuata takwimu hizo.

CWT KIBAHA WATAKA MABORESHO KIKOKOTOO

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani kimeomba kanuni ya kikokotoo kuangaliwa upya au kirudishwe cha zamani ambacho kilikuwa ni asilimia 50 badala ya cha sasa ambacho ni asilimia 33.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa chama hicho Mwita Magige alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Magige amesema kuwa kanuni ya kugawa kikokotoo cha sasa iangaliwe upya ambapo mafao wanayoyapata baada ya kustaafu ni madogo tofauti na yale ya awali.

Amesema kuwa kanuni hiyo iangaliwe upya kwa kuboreshwa na ikiwezekana kirudishwe kikokotoo cha zamani ambacho ni kizuri kuliko cha sasa.

Aidha amesema kuwa kuboreshwa kikokotoo kutawafanya walimu wawe na morali ya kazi kwani watakuwa wanafuraha na malipo hayo mara baada ya kustaafu.


HALMASHAURI KUINUA VIPAJI VYA MICHEZO

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imesema kuwa itaweka mazingira mazuri ya michezo ili kuinua vipaji vya vijana ili waweze kujiajiri kupitia michezo ambayo ni kama kiwanda.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) Kibaha Moses Magogwa alipokuwa akikabidhi ubingwa kwa timu ya Umwelani iliposhindwa kwa kuifunga Wapolo kwa penati 3-1 kwenye michuano ya Micho Cup  kwenye uwanja wa Mwendapole ambapo ilijinyakulia kiasi cha shilingi milioni mbili.

Magogwa alisema kuwa michezo ni kiwanda cha ajira ambayo inaajiri vijana wengi ambapo inapaswa kuwekewa mazingira mazuri ili ajira hiyo iendelee kutoa ajira.

"Tutahakikisha halmashauri zote mbili ya Kibaha Mjini na Wilaya ya Kibaha zinaboresha masuala ya michezo kwani nimeona hamasa kubwa iliyopo kwenye michezo tumeona vijana walivyoshiriki michezo,"alisema Magogwa.

Aidha alise kuwa baada ya timu hiyo kushinda itafika ofisini kwa mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kupongezwa kutokana na ushindi huo kwani Mkuu huyo wa Wilaya ndiye aliyepaswa kuwa mgeni rasmi lakini alipata dharura.

"Dc Nickson John anawapongeza kwa kutwaa ubingwa na amewakaribisha muende ofisini kwake akawapongeze kwani naye ni mdau wa michezo na anafurahi kuona vijana wakicheza michezo,"alisema Magogwa.

Aliongeza kuwa changamoto walizomweleza atazifanyia kazi kwani yeye ni mwenyekiti wa kamati ya michezo ya Wilaya atashirikiana na vyama vya michezo ili kuendeleza jitihada za michezo. 

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Wilaya ya Kibaha (KIBAFA) Robert Munis alisema kuwa mpango wa chama ni kuwa ni vituo nane vya kuendeleza soka la vijana.

Munis alisema wanapongeza waandaaji ya mashindano hayo kwani ni sehemu ya mpango wa chama kuwa na mashindano mara kwa mara ili kupata timu bora zitakazoshiriki kwenye ligi za Wilaya.

Kwa upande wa mratibu wa michuano hiyo ya Micho Cup Othamn Shija "Micho" alisema kuwa jumla ya timu 24 zilichuana kwenye awamu ya pili ya mashindano hayo.

Shija alisema kuwa changamoto kubwa ni kukosa wafadhili wa kudhamini mashindano hayo ambayo yana lengo la kuibua vipaji na kuwahamasisha vijana kushiriki michezo badala ya kujiingiza kwenye vitendo viovu pia kukuza soka la Kibaha.

UMWELANI WAKOMBA MILIONI 2 MICHO CUP

TIMU ya soka ya Umwelani imetwaa ubingwa wa Micho Cup baada ya kuifunga timu ya Wapolo kwa penati 3-1 baada ya kutoshana nguvu kwa kufungana 1-1 hadi dakika 90 zinamalizika.

Katika mchezo huo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa Mwendapole hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana magoli hayo.

Wapolo ndiyo waliokuwa wakwanza kuandika bao dakika ya 2 kupitia kwa Adolf Mpangule huku Umwelani wakisawazisha kupitia kwa Baraka Jafary dakika ya 26.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kukiwa na kosa kosa za hapa na pale lakini hadi dakika 90 hakuna mbabe aliyepatikana na kuingia hatua ya matuta.

Ambapo washindi walipata penati 3 huku Wapolo wakikosa penati zote na kupata 1 hivyo kutawazwa mabingwa na kujinyakulia kiasi cha shilingi milioni 2 taslimu.

Wapolo walijinyakulia seti mbili za jezi na mpira mmoja ambapo washindi walikabidhiwa zawadi na katibu tawala wa wilaya ya Kibaha Moses Magogwa ambaye alimwakilisha mkuu wa wilaya ya Kibaha Nickson John.

Magogwa amesema kuwa serikali itashirikiana na wadau wa michezo ili kuendeleza michezo kwenye wilaya hiyo.

Naye mwenyekiti wa chama cha soka wilaya ya Kibaha (KIBAFA) Robert Munis alisema kuwa mashindano hayo yamehamasisha mpira kwenye wilaya hiyo.

Kwa upande wake mratibu wa mashindano hayo Othaman Shija amesema kuwa changamoto kubwa ni kukosa wadhamini wa mashindano hayo na kuomba wadau kujitokeza kudhamini michuano hiyo inayofanyika kila mwaka ikiwa ni mwaka wake wa pili.