Monday, July 24, 2023

URAIA WETU YAZINDULIWA

SHIRIKA la Maendeleo ya Vijana (YPC) la Kibaha Mkoani Pwani limeingia mkataba wa miaka mitatu na Shirika la The Civil Society (FCS) chini ya udhamini wa Jumuiya ya Ulaya (EU) wa kutoa elimu Utawala wa Kidemokrasia kupitia mradi wa Uraia Wetu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Mkurugenzi wa YPC Israel Ilunde amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kwenye mikoa minne ya Kanda ya Mashariki.

Ilunde amesema kuwa mradi huo una lengo la kuendeleza mazingira wezeshi kwa ajili ya utawala wa kidemokrasia nchini ambapo kwa kanda ya mashariki ni mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Morogoro.

Amesema kuwa mradi utawezesha majadiliano kati ya serikali na azaki kwa ajili ya uchechemuzi (ushawishi na utetezi) wa masuala wa kidemokrasia, maendeleo na kuboresha mahusiano na ushirikiano wa kikazi.

Aidha amesema kuwa mradi utatoa fursa wa azaki kujengewa uwezo kujiendesha kupitia shughuli zao ili kuwanufaisha wananchi wa kanda hiyo na Watanzania kwa ujumla.


Sunday, July 23, 2023

RC ATAKA WALIOCHOMA MOTO BONDE MZAKWE WASAKWE


MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani Dodoma kuhakikisha vinawasaka na kuwabaini wote waliohusika na uchomaji moto katika Bonde la Mzakwe.

Senyamule ametoa agizo hilo leo Julai 21, 2023 mara baada ya kufika katika eneo hilo kujionea athari za uharibifu zilizosababishwa na moto ulioanza majira ya saa saba mchana.

Amesema asilimia 70 ya maji katika Jiji la Dodoma yanatoka katika bonde la Mzakwe na ni eneo la hifadhi hivyo ni muhumimu kukakikisha linalindwa na kuhifadhiwa kwa ustawi wa afya na mazingira ya watu wote.

Aidha, amewapongeza vijana wa JKT Makutupora walioshiriki katika zoezi la kuzima moto uliotokea hii leo tarehe katika Bonde la Mzakwe Jijini Dodoma. Senyamule amewapongeza kwa uzalendo walionyesha wa kudhibiti moto huo na kuzuia usilete madhara makubwa, amesema wameonyesha uzalendo mkubwa, uhodari na ushupavu.

 "Tumesikitishwa sana na moto huu kwa kuwa si kwamba umeathiri ikolojia ya eneo hili lakini pia umeharibu miundombinu ya Tanesco ikiwa ni pamoja na nguzo, hivyo kwanza nawapongeza vijana wetu kwa jitihada za kufanikisha kuzima moto huu na pili vyombo vyote vinavyohusika na uchunguzi vifanye kazi yake ili kubaini chanzo” Senyamule amesisitiza.

Amemuagiza Meneja wa Bonde la Wami Ruvu kuhakikisha kuwa wanachonga barabara maalum kwa lengo la kukinga moto katika bonde hilo ili athari za moto zisiwe kubwa pindi moto utokeapo.

Awali Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Dodoma Julishaeli Mfinanga amesema kuwa walipata taarifa kwa njia ya simu kupitia namba za dharura 114 na kuwahi eneo la tukio kwa haraka. Amesema moto umedhibitiwa na hakuna madhara makubwa na wanaendelea na doria kuhakikisha usalama katika eneo hilo.

Saturday, July 22, 2023

*UJUMBE KUTOKA KENYA WAJIFUNZA USIMAMIZI SEKTA YA MADINI*

Ujumbe kutoka Kenya ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini wa nchi hiyo Elijah Mwangi umefika nchini kujifunza kuhusu namna bora ya usimamizi wa Sekta ya Madini ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali ameupokea ujumbe huo.

Akizungumza katika kikao na ujumbe huo, Mahimbali amesema Tanzania ni sehemu salama ya uwekezaji kutokana na uongozi bora wa Serikali unaosimamiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo umepelekea kuifanya sekta hiyo kupata mafanikio makubwa.

Mahimbali amesema Wizara ya Madini ina Taasisi tano ambazo ni Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) pamoja na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ambazo hutekeleza majukumu yake kwa ushirikiano.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini kutoka Kenya Elijah Mwangi ameipongeza Wizara ya Madini kwa usimamizi bora wa sekta hiyo na kumuomba Mahimbali kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo tafiti na usimamizi wa biashara ya madini.

Katika kikao hicho mada mbalimbali zimewasilishwa ambapo Mtendaji Mkuu wa  GST Dkt. Mussa Budeba amewasilisha mada juu ya madini yapatikanayo Tanzania na aina za tafiti zilizokwisha fanyika. 

Dkt. Budeba amesema kwa sasa GST imejikita zaidi kwenye tafiti za madini ya kimkakati ambapo mpaka sasa Tanzania imefanyiwa tafiti za Kijiolojia kwa asilimia 96.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ally Maganga amewasilisha mada juu ya shughuli za Tume ya Madini ikiwemo uwepo wa Masomo na Vituo vya Ununuzi wa Madini, Mfumo wa Leseni pamoja na shughuli za wachimbaji wadogo.

Mhandisi Maganga amesema   uwepo wa masoko na vituo vya kuuzia madini umesaidia kuongeza mapato ya Sekta ya Madini ambapo mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo kwa sasa umefikia asilimia 9.7 ikiwa lengo ni kufikia mchango wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Friday, July 21, 2023

MKE WA MBUNGE AWAPIGA TAFU WASANII.

 


KATIKA kuhakikisha sanaa inakuwa Wilayani Kibaha mke wa Mbunge wa Kibaha Mjini Selina Koka ametoa kiasi cha shilingi milioni 1.2 ili kuendeleza sanaa hiyo kupitia Chama Cha Waigizaji Wilayani Kibaha humo.


Mke huyo wa Mbunge huyo alitoa fedha hizo wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika Visiga Madafu wilayani humo.


Akikabidhi cheki ya fedha hizo aliwataka waigizaji hao kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na kukuza tasnia hiyo ya sanaa ambayo imekuwa na kuwa na maslahi mazuri.


Awali Rais wa chama hicho Dk Cynthia Henjewele alisema kuwa wasanii wanapaswa kuungana na kutumia fursa za mikopo kupitia mfuko wa utamaduni ambayo inatolewa kwa wasanii ambazo hazina riba.

MKE WA MBUNGE ACHANGIA MAMILIONI CHAMA CHA WAIGIZAJI KIBAHA

MKE wa Mbunge wa Kibaha Mjini Selina Koka ametoa kiasi cha shilingi milioni 1.2 kwa Chama Cha Waigizaji Wilayani Kibaha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.

Koka alitoa fedha hizo wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika Visiga Madafu wilayani humo.

Akikabidhi cheki ya fedha hizo aliwataka waigizaji hao kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na kukuza tasnia hiyo ya sanaa ambayo imekuwa na kuwa na maslahi mazuri.

"Tumieni sanaa kwa ajili ya kuelimisha jamii, kuburudisha na kufundisha ili muwe sehemu ya maendeleo ya nchi na kujinufaisha wenyewe kwa wenyewe,"alisema Koka.

Awali Rais Sanaa za Maonyesho Tanzania Dk Cynthia Henjewele alisema kuwa wasanii wanapaswa kuungana na kutumia fursa za mikopo kupitia mfuko wa utamaduni ambayo inatolewa kwa wasanii ambazo hazina riba.

Henjewele alisema kuwa ili wasanii waweze kutambulika wanapaswa kujisajili ili watambulike kisheria ambapo wakijirasimisha watapata fursa mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kibaha Mjini Jumanne Kambi alimshukuru mke wa Mbunge kwa mchango wake wa kukuza sanaa kwenye Wilaya hiyo.

Kambi alisema kuwa kwa kuwa sasa wana ofisi na tayari wana wanachama 700 watahakikisha wanachama wao wanaingia mikataba yenye manufaa kwa wasanii tofauti na kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wanadhulumiwa haki zao.



WANANCHI WATAKIWA KULIPA ANKARA ZA MAJI NA KULINDA MAZINGIRA


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji Safi na usafi wa Mazingira Bunda BUWSSA Bi Ester Gilyoma ametoa wito kwa wananchi wa Halmashauri ya Bunda iliopo Mkoani Mara kwa wale wanaotumia maji ya BUWSSA kuacha tabia ya wizi wa maji na badala yake wahakikishe wanalipa Ankara za maji, sambamba na utunzaji wa vyanzo na miundombinu ya maji katika Halmashauri hiyo.

Bi Ester ametoa wito huo  Jijini Dodoma katika mkutano wake na Wana habari wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/2024.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa hapo awali kulikuwa na changamoto kwa wakazi wa Bunda kwa kupata maji yasiyo Safi na salama ambapo kwasasa ndani ya uongozi wa Raisi wa awamu ya sita ya Dkt Samia Suluhu Hassan Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya maji ikiwemo chujuo la kuchuja na kutibu maji hivyo maji machafu Bunda Sasa basi.

Pia amesema wanaendelea na jitihada za kupunguza au kuondoka kabisa changamoto za upotevu wa maji ikiwa ni pamoja kuwepo kwa Mpango wa kubadili mita goigoi kwani kwa mwaka wa Jana upotevu ulikuwa asiliamia 45,lakini mpaka Sasa upotevu umeendelea kupungua mpaka asiliamia 36.

WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA MAADHIMISHO YA MASHUJAA JULAI 25

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa jirani kushiriki hafla ya Maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya Mashujaa itakayofanyika Julai 25 mwaka huu katika eneo la kudumu la mashujaa lililopo Mji wa Serikali Mtumba ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wito huo umetolewa leo tarehe 20/07/2023 alipofanya Mkutano na waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jengo la Mkapa kwa dhumuni la kuukaribisha Umma wa Watanzania kushiriki kuwaenzi mashujaa waliolipigania Taifa la Tanzania.

"Julai 25 ya kila mwaka Tanzania huwa inaadhimisha kumbukumbu ya siku ya Mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda Uhuru wa Nchi yetu.  Siku hii ni muhimu kwa sababu inatukumbusha kuhusu wajibu wetu wa kutunza historia ya Mashujaa waliopigania, kutetea na kulinda Uhuru wa Nchi ya Tanzania ili kurithisha vizazi vijavyo umuhimu wa kutumia historia hii kukuza na kuendeleza amani na mshikamano wa kitaifa bila kujali tofauti mbalimbali, ikiwemo za kikabila, kidini na  itikadi za kisiasa.

"Ninapenda kuwajulisha kuwa tofauti na ilivyozoeleka katika miaka ya nyuma, ambapo Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa katika Mkoa wa Dodoma yalikuwa yanafanyika katika Viwanja vya Jamatin vilivyopo katikati ya Mji wa Dodoma, mwaka huu (2023) Kilele cha Maadhimisho haya kitafanyika katika Uwanja mpya wa kudumu wa Mashujaa uliopo katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.  Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo atakuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama", Mhe. Senyamule

Aidha, shughuli za Mashujaa zitatanguliwa na uwashaji wa Mwenge wa Mashujaa saa 6:00 Usiku wa tarehe 24 Julai, 2023 kuamkia tarehe 25 Julai 202 ambapo Mhe.Senyamule amepewa heshima ya kuuwasha Mwenge huo wa Mashujaa kwa niaba ya Wanadodoma na Mwenge huo utazimwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof. Davis Mwamfupe tarehe 25 Julai 2023 saa 6:00 Usiku.

Tumebakiza takribani siku nne tuadhimishe Siku ya Mashujaa Maandalizi ya Maadhimisho yamekamilika kwa 100% kwaiyo nichukue fursa hii kuwakaribisha Viongozi na Wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na kutoka nje ya Mkoa wa Dodoma, ikiwemo Mikoa jirani ya Singida, Manyara, Iringa na Morogoro kujitokeza kwa wingi kuja kuungana na Wanadodoma katika kuadhimisha siku hii muhimu, ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza katika kiwanja kipya kilichopo eneo la Mtumba".

Hatahivyo Mhe.Senyamule ametumia fursa hiyo kuzishukuru Taasisi zote, ambazo kwa namna moja au nyingine zimeshiriki katika ujenzi wa Mnara Mpya wa Mashujaa katika Mji wa Serikali – Mtumba