Friday, July 21, 2023

MKE WA MBUNGE AWAPIGA TAFU WASANII.

 


KATIKA kuhakikisha sanaa inakuwa Wilayani Kibaha mke wa Mbunge wa Kibaha Mjini Selina Koka ametoa kiasi cha shilingi milioni 1.2 ili kuendeleza sanaa hiyo kupitia Chama Cha Waigizaji Wilayani Kibaha humo.


Mke huyo wa Mbunge huyo alitoa fedha hizo wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika Visiga Madafu wilayani humo.


Akikabidhi cheki ya fedha hizo aliwataka waigizaji hao kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na kukuza tasnia hiyo ya sanaa ambayo imekuwa na kuwa na maslahi mazuri.


Awali Rais wa chama hicho Dk Cynthia Henjewele alisema kuwa wasanii wanapaswa kuungana na kutumia fursa za mikopo kupitia mfuko wa utamaduni ambayo inatolewa kwa wasanii ambazo hazina riba.

MKE WA MBUNGE ACHANGIA MAMILIONI CHAMA CHA WAIGIZAJI KIBAHA

MKE wa Mbunge wa Kibaha Mjini Selina Koka ametoa kiasi cha shilingi milioni 1.2 kwa Chama Cha Waigizaji Wilayani Kibaha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.

Koka alitoa fedha hizo wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika Visiga Madafu wilayani humo.

Akikabidhi cheki ya fedha hizo aliwataka waigizaji hao kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na kukuza tasnia hiyo ya sanaa ambayo imekuwa na kuwa na maslahi mazuri.

"Tumieni sanaa kwa ajili ya kuelimisha jamii, kuburudisha na kufundisha ili muwe sehemu ya maendeleo ya nchi na kujinufaisha wenyewe kwa wenyewe,"alisema Koka.

Awali Rais Sanaa za Maonyesho Tanzania Dk Cynthia Henjewele alisema kuwa wasanii wanapaswa kuungana na kutumia fursa za mikopo kupitia mfuko wa utamaduni ambayo inatolewa kwa wasanii ambazo hazina riba.

Henjewele alisema kuwa ili wasanii waweze kutambulika wanapaswa kujisajili ili watambulike kisheria ambapo wakijirasimisha watapata fursa mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kibaha Mjini Jumanne Kambi alimshukuru mke wa Mbunge kwa mchango wake wa kukuza sanaa kwenye Wilaya hiyo.

Kambi alisema kuwa kwa kuwa sasa wana ofisi na tayari wana wanachama 700 watahakikisha wanachama wao wanaingia mikataba yenye manufaa kwa wasanii tofauti na kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wanadhulumiwa haki zao.



WANANCHI WATAKIWA KULIPA ANKARA ZA MAJI NA KULINDA MAZINGIRA


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji Safi na usafi wa Mazingira Bunda BUWSSA Bi Ester Gilyoma ametoa wito kwa wananchi wa Halmashauri ya Bunda iliopo Mkoani Mara kwa wale wanaotumia maji ya BUWSSA kuacha tabia ya wizi wa maji na badala yake wahakikishe wanalipa Ankara za maji, sambamba na utunzaji wa vyanzo na miundombinu ya maji katika Halmashauri hiyo.

Bi Ester ametoa wito huo  Jijini Dodoma katika mkutano wake na Wana habari wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/2024.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa hapo awali kulikuwa na changamoto kwa wakazi wa Bunda kwa kupata maji yasiyo Safi na salama ambapo kwasasa ndani ya uongozi wa Raisi wa awamu ya sita ya Dkt Samia Suluhu Hassan Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya maji ikiwemo chujuo la kuchuja na kutibu maji hivyo maji machafu Bunda Sasa basi.

Pia amesema wanaendelea na jitihada za kupunguza au kuondoka kabisa changamoto za upotevu wa maji ikiwa ni pamoja kuwepo kwa Mpango wa kubadili mita goigoi kwani kwa mwaka wa Jana upotevu ulikuwa asiliamia 45,lakini mpaka Sasa upotevu umeendelea kupungua mpaka asiliamia 36.

WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA MAADHIMISHO YA MASHUJAA JULAI 25

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa jirani kushiriki hafla ya Maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya Mashujaa itakayofanyika Julai 25 mwaka huu katika eneo la kudumu la mashujaa lililopo Mji wa Serikali Mtumba ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wito huo umetolewa leo tarehe 20/07/2023 alipofanya Mkutano na waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jengo la Mkapa kwa dhumuni la kuukaribisha Umma wa Watanzania kushiriki kuwaenzi mashujaa waliolipigania Taifa la Tanzania.

"Julai 25 ya kila mwaka Tanzania huwa inaadhimisha kumbukumbu ya siku ya Mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda Uhuru wa Nchi yetu.  Siku hii ni muhimu kwa sababu inatukumbusha kuhusu wajibu wetu wa kutunza historia ya Mashujaa waliopigania, kutetea na kulinda Uhuru wa Nchi ya Tanzania ili kurithisha vizazi vijavyo umuhimu wa kutumia historia hii kukuza na kuendeleza amani na mshikamano wa kitaifa bila kujali tofauti mbalimbali, ikiwemo za kikabila, kidini na  itikadi za kisiasa.

"Ninapenda kuwajulisha kuwa tofauti na ilivyozoeleka katika miaka ya nyuma, ambapo Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa katika Mkoa wa Dodoma yalikuwa yanafanyika katika Viwanja vya Jamatin vilivyopo katikati ya Mji wa Dodoma, mwaka huu (2023) Kilele cha Maadhimisho haya kitafanyika katika Uwanja mpya wa kudumu wa Mashujaa uliopo katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.  Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo atakuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama", Mhe. Senyamule

Aidha, shughuli za Mashujaa zitatanguliwa na uwashaji wa Mwenge wa Mashujaa saa 6:00 Usiku wa tarehe 24 Julai, 2023 kuamkia tarehe 25 Julai 202 ambapo Mhe.Senyamule amepewa heshima ya kuuwasha Mwenge huo wa Mashujaa kwa niaba ya Wanadodoma na Mwenge huo utazimwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof. Davis Mwamfupe tarehe 25 Julai 2023 saa 6:00 Usiku.

Tumebakiza takribani siku nne tuadhimishe Siku ya Mashujaa Maandalizi ya Maadhimisho yamekamilika kwa 100% kwaiyo nichukue fursa hii kuwakaribisha Viongozi na Wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na kutoka nje ya Mkoa wa Dodoma, ikiwemo Mikoa jirani ya Singida, Manyara, Iringa na Morogoro kujitokeza kwa wingi kuja kuungana na Wanadodoma katika kuadhimisha siku hii muhimu, ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza katika kiwanja kipya kilichopo eneo la Mtumba".

Hatahivyo Mhe.Senyamule ametumia fursa hiyo kuzishukuru Taasisi zote, ambazo kwa namna moja au nyingine zimeshiriki katika ujenzi wa Mnara Mpya wa Mashujaa katika Mji wa Serikali – Mtumba

Thursday, July 20, 2023

*MBOYA MBUZI SODO CUP YAFANA*




KIBAFA INATISHA...ikiwa ni wiki mbili baada ya uongozi mpya wa chama cha soka wilaya ya Kibaha kuingia madarakani imeshuhudiwa viongozi wa chama hicho wakihudhuria mashindano ya soka la ufukweni maarufu kama "Beach soka"

Mashindano hayo yamefanyika Mlandizi yakiwa ni ya Mboya mbuzi SODO cup...

Katika mashindano hayo imeshudiwa viongozi kadhaa wapya wa KIBAFA wakihudhuria ambapo wameongozwa na mwenyekiti wa KIBAFA comrade Robert Munisi...makamu mwenyekiti bwana David Mramba...

Pia alikuwepo katibu msaidizi wa KIBAFA bwana Omary Abdul pamoja na wajumbe  wa kamati tendaji ya KIBAFA bila kusahau mwenyekiti wa kamati ya Beach soka bwana Nassoro Shomvi

Katika hali ya kuonesha KIBAFA wapo kazini pia mbunge wa jimbo la Kibaha vijiijini mheshimiwa Michael Mwakamo alihudhuria mashindano hayo hali iliyoibua shangwe na vibe la aina yake kwa wakazi na mashabiki wa Beach soka waliojitokeza kutoka Mlandizi na Kibaha kwa ujumla...

Katika mashindano hayo timu ya Kilangalanga umeibuka mshindi wa fainali hiyo baada ya kuibamiza timu ya Msalabani goli 4-1 na kuifanya timu ya Kilangalanga kupata zawadi ya mbuzi mnyama huku mshindi wa pili na washiriki wengine nao wakijizolea zawadi lukuki....ambapo mshindi wa pili ambaye ni timu ya Msalabani wamepata zawadi ya kuku ndege....mfungaji bora akipata pesa taslimu elfu30,mchezaji bora wa mshindano sambamba na golikipa bora wakipata mche wa sabuni kila mmoja.

Katika nyakati mbalimbali mwenyekiti wa KIBAFA comrade Robert Munisi amekuwa akisikika akisema KIBAFA ya sasa ni kwa ajili ya kuhakikisha soka linachezwa Kibaha na kuhakikisha Kibaha inakuwa wilaya ya mfano kwa Tanzania nzima

Wednesday, July 19, 2023

*WIZARA YA MADINI YADHAMIRIA KUONDOA CHANGAMOTO KWA WACHIMBAJI WA MADINI WAKUBWA NA WA KATI*

*Dkt. Biteko asikiliza mafanikio na kero za wachimbaji wa madini wakubwa na wa kati*

WIZARA ya Madini imedhamiria kuweka mipango thabiti kuhakikisha changamoto zilizopo kwenye Sekta ya Madini zinatatuliwa kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji wa madini nchini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko wakati akifungua kikao cha kujadili maendeleo, changamoto na kero zinazozikabili Kampuni kubwa na za kati zinazojishughulisha na uchimbaji wa madini nchini.

"Leo ni siku ya kuwasikiliza wachimbaji wakubwa wa madini na wa kati kama tunavyo wasikiza Wachimbaji Wadogo kama wanachangamoto gani ili tuweze kuzifanyia kazi lakini pia tunajiandaa na Mkutano wa Mkuu wa Kisekta wa Mwaka unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu," amesema Dkt. Biteko.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema tayari serikali imerahisisha mazingira ya kikodi kwa wachimbaji wa madini ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokaza katika kutimiza wajibu yao.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Maji, Nishati na Madini kutoka Zanzibar Staibu Hassan ameipongeza Wizara ya Madini kwa hatua kubwa ambapo amesema wizara hiyo imekuwa mwalimu wa mataifa mengi kujifunza usimamizi bora wa shughuli za biashara na uchimbaji madini.

Naye, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi, Mhandisi Philibart Rweyemamu amesema Chama anachokiongoza kipo tayari kushirikiana na serikali ili kuondoa changamoto na kutoa suluhisho la kudumu katika sekta hiyo ili hatimaye kufikia lengo la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo 2025.

"Kikao cha namna hii kitakuwa kinafanyika kila robo mwaka ili kutoa taarifa kwa serikali juu ya maendeleo ya shughuli zetu, kuueleza umma nini kinachofanyika pamoja na kuishauri serikali kitu gani tunafikiri kifanyike ili kurahisisha utendaji wa Sekta ya Madini," amesema Mhandisi Rweyemamu.

Katika kikao hicho Kampuni tano za uchimbaji mkubwa wa madini zimetoa taarifa za utekelezaji wa miradi inayotekelezwa ikiwemo Kampuni ya Nyati Corporation, Sotta Mining, Tembo Nickel Corporation, Twiga Minerals na Faru Graphite Limited.

WATAKIWA WASIDANGANYE MAKAZI

MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Mhe.Rosemary Senyamule amewaasa wananchi na wakazi wa Dodoma kuacha kudanganya maeneo ya makazi ili kuepusha migogoro ya ardhi.

Mhe.Senyamule ameyasema hayo wakati akizindua mpango mkakati kwa ajili ya kushughulikia na kutatua migogoro ya ardhi kwa jiji la Dodoma.

Aidha amesema kuwa jiji la Dodoma limekuwa na ongezeko la wananchi hivyo kufuatia ongezeko hilo limepelekea matumizi ya ardhi kuwa ni mengi na mengine kuwa ya kiholela bila mpangilio ambapo kwa kutatua changamoto hii mkoa wa Dodoma kupitia Mkuu wa mkoa wa Dodoma imeandaa timu kwa ajili ya kutatua na kumaliza migogoro.

"Kuna changamoto mbalimbali zinazochangia migogoro hii kushindwa kuisha kutokana na uchache wa vifaa vya tehama, ukosefu wa huduma bora kwa wananchi,eneo la jiji kuwa dogo, lugha mbaya kwa wananchi zinazotolewa na watumishi wa jiji,kipandikizi yaani kupandikiza zaidi ya kiwanja kimoja kupewa watu tofauti pamoja na wananchi kupuuza jumbe za simu" Amesisitiza Senyamule.

Aidha ameongeza kuwa jambo hili litafanyika ndani ya miezi 6 yaani Julai hadi Disemba ambapo kutafanyika uhakiki wa maeneo ambayo yanamalalamiko ambapo wahusika wanavamia maeneo ambayo sio ya kwao pamoja na kurekebisha mifumo kwa kushirikiana na ofisi ya Rais tamisemi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,Mhe. Jabir Shekimweri amesema kuwa mpango huo utaweza kuwasaidia kutambua mapungufu gani ya ndani na madhaifu gani ya nje ili ili kuishi matarajio ya kiongozi wa kitaifa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha jiji la Dodoma linapagwa vizuri ili kuendana na hadhi ya makao makuu ya nchi.

Amesema ni matumaini yake kwamba elimu ya kutosha itatolewa kwa kamati ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa huku akisisitiza maeneo ya wazi kupewa watu sahihi ili kuhakikisha wanajenga vitu vyenye manufaa kwa wananchi.

Aidha ametoa rai kwa watumishi wa ardhi kuhudumia wateja vizuri kwa kutoa kauli nzuri kwa wateja pamoja na kuheshimu watu.