Thursday, February 23, 2023

MAMLAKA YA SERIKALI MTANDAO KUONGEZA UWEZO WA MAWASILIANO


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMLAKA ya serikali Mtandao (eGA) imepanga kupanua uwezo wa Mtandao wa mawasiliano serikalini ( Government Network) na kuufikisha wilaya zote nchini Ili kurahisisha utekelezaji wa jitihada za serikali Mtandao na kuwafikishia huduma wananchi wote popote walipo.

Hayo yamesemwa na Mkurugezi mkuu wa mamlaka ya serikali mtandao Mhandisi Benedict Ndomba wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa mamlaka hiyo.

Ndomba amesema kuwa mfumo wa ubadilishaji taarifa serikalini imewezesha zaidi ya taasisi 50 kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo na amezitaka taasisi za umma ambazo hazijaunganishwa katika mfumo huo ziunganishwe Ili ziweze kubadilishana taarifa na taasisi nyingine pale inapohitajika.

"Jumla ya taasisi 200 zinatumia mfumo wa ofisi Mtandao kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi katika taasisi za umma pia umesaidia kupunguza matumizi ya karatasi kutunza mazingira na kuokoa fedha za serikali,"alisema Ndomba.

Serikali mtandao ni matumizi ya Teknolojia ya habari na mawasiliano ( TEHAMA) Katika utendaji kazi wa taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi wenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Katika taasisi ya umma pamoja na kuboresha utoaji huduma kwa umma Ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi haraka na gharama nafuu. 

WASIOENDELEZA ARDHI KUNYANGANYWA

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amezitaka Serikali za Vijiji kuorodhesha majina ya wawekezaji ambao wamehodhi ardhi bila kuiendeleza ili irudishwe kwa ajili ya matumizi mengine.

Aliyasema hayo alipokuwa kwenye ziara ya kwenye Kata ya Lugoba Halmashauri ya Chalinze kuzungumza na wananchi kutatua kero na changamoto kwenye Jimbo la Chalinze ambapo yeye ndiyo Mbunge wa Jimbo hilo.

Ridhiwani alisema kuwa maeneo mengi aliyopita kikiwemo Kijiji cha Makombe  kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa wananchi juu ya baadhi ya maeneo yaliyoombwa na wawekezaji hayajaendelezwa na kuwa mapori.

"Vijiji na Vitongoji orodhesheni majina ya wawekezaji wote walio katika maeneo yenu ambao hawajaendeleza ardhi waliyoiomba kufanya uwekezaji lakini wameiacha bila kuiendeleza kwani huo siyo utaratibu ni vema wakanyanganywa na kupewa watu wengine ili kuyatumia kuleta maendeleo,"alisema Ridhiwani.

Alisema kama kuna maeneo mnaona yametelekezwa na wawekezaji wasipate shida wanachotakiwa viongozi kupitia mikutano mikuu ni kutoa hoja na kuandikwa muhutasari kisha upelekwe Halmashauri na kupelekwa Wizarani ili kubadilishwa matumizi na kurudishwa Kijijini na kupangiwa shughuli nyingine.

"Tena kuna baadhi ya wawekezaji wanapokwenda kuomba maeneo wanatoa ahadi nyingi kuwa wakipewa watasaidia huduma za jamii au kutoa ajira kwa Vijana wa eneo husika lakini hawafanyi hivyo ni vema wakaachia ardhi waliyopewa,"alisema Ridhiwani.

Naye Diwani wa Lugoba Rehema Mwene alisema kuwa Kijiji cha Makombe kinakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara, ukosefu wa maji, uchakavu wa Zahanati na baadhi ya maeneo kukosa umeme.

Mwene alisema kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya wawekezaji kuchukua maeneo na kutoyaendeleza hivyo kufanya kuwe na mapori makubwa ambayo yanahatarisha usalama wa watu.

Kwa upande wake kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Makombe Godfrey Nyange akisoma risala ya Kijiji alisema kuwa kuna migogoro ya mipaka baina ya Kijiji hicho na Vijiji vya Kinzagu na Mindutulieni.

Nyange alisema kuwa changamoto nyingine ni wanufaika wa Mfuko ya Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuondolewa kwenye mfumo na wengine kutolipwa fedha zao za kila mwezi. Naibu Waziri alitembelea Vijiji vya Makombe, Mindutulieni na Lunga kwenye Kata ya Lugoba.



TANESCO KUONGEZA UZALISHAJI UMEME


Na Mwandishi Wetu Dodoma

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) linatarajia kuzalisha megawati 5,000 kupitia miradi mbalimbali ifikapo kwa mwaka 2025 hivyo kuongeza uzalishaji umeme kupitia gridi ya Taifa.

Hayo yamesemwa na kaimu Mkurugezi wa huduma kwa wateja wa shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) Martin Mwambene wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali ya shirika hilo na uelekeo wake kwa mwaka wa 2023 .

Mwambene amesema kuwa kwa sasa shirika hilo lina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 1,820 wakati mitambo iliyopo ina uwezo wa kuzalisha megawati 1,300 pekee. 

Amesema kuwa TANESCO kwa kutambua matatizo ya umeme yaliyopo nchini imekuja na mradi wa Gridi Imara ambapo katika bajeti ya mwaka huu imetengewa shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.

"Katika mradi wa Grid Imara utajumuisha ununuzi wa mashine umba 6000, mita 700,000 za umeme, nguzo 380,000 ununuzi na ufungaji wa nyaya zenye urefu wa km 40,000, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme mkubwa takribani kilomita 948 na ujenzi wa vituo 14 vya kupooza umeme,"amesema Mwambene. 

Aidha amezungumzia pia maendeleo ya ujenzi katika Bwawa la Mwalimu NYerere kuwa upo katika asilimia 88 na zoezi la uwekaji maji limefikia mita za ujazo 133 kutoka usawa wa bahari

TCU KUTHIBITI UBORA


Na Mwandishi Wetu Dodoma

TUME ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) imeendelea kuimarisha mifumo yake ya uthibiti ubora na mifumo ya ndani ya vyuo vikuu Ili kuhakikisha vinaendana na mwelekeo wa nchi pamoja na kuandaa na kuratibu mafunzo kwa viongozi wahadhiri na maofisa wa vyuo vikuu vya umma na binafsi hapa nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo katika usimamizi wa uendeshaji wa taasisi zao.

Hayo yamesemwa na katibu mtendaji tume ya vyuo vikuu Tanzania Prof. Charles Kihampa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za tume hiyo kwa kipindi Cha Miaka miwili ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita.

Kihampa amesema kuwa Katika kuhakiki ubora tume imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara wa kawaida na wa kushtukiza kwa mujibu wa Sheria na utaratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa Elimu itolewayo na vyuo vikuu hapa nchini inakidhi viwango vya ubora kikanda, kitaifa na kimataifa.

Amesema kuwa nafasi za masomo Katika vyuo vya Elimu ya juu Katika program za shahada ya kwanza zimeongezeka kutoka 157,770 Mwaka 2020/2021 Hadi 172,168 Mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la nafasi 14,398 ya asilimia 9.1.

Aidha amesema mwaka 2022/2023 serikali imetenga kiasi Cha shilingi bilion 6.4 kupitia mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi ( higher Education for Economic Transformation- HEET) kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu ambapo zaidi ya mitaala 300 ya vyuo hivyo vinafanyiwa mapitio Ili kuhuishwa kwa kizingatia maoni ya wadau mbalimbal

Thursday, February 16, 2023

WAKULIMA WATAKIWA KUTUMIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI



Na Mwandishi Wetu Dodoma

BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imetoa wito kwa wakulima kutokubali kurubuniwa na madalali badala yake waingie kwenye mfumo wa Stakabadhi ghalani ili kuuza mazao yao kulingana na bei iliyopo sokoni.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Asangye Bangu Jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za bodi hiyo.

Bangu amesema kuwa kumekuwa na wimbi la madalali kwenda mashambani kwa wakulima na kuwarubuni na kununua kwa bei ya chini hali ambayo inawakandamiza wakulima.

"Tangu kuanzishwa kwa mfumo huo mwaka 2007/2008 hadi 2020/2021 ukuaji wa uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2 kwa mwaka kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala,"amesema Bangu.

Amesema bodi imeendalea na juhudi za kuboresha mfumo uliokuwepo wa kizamani wa usimamizi wa ghala ambapo kwa kushirikiana na bodi inakuja na mfumo mpya wenye kuweza kurahisisha kazi za maandalizi ya taarifa utoaji stakabadhi na udhibiti wa matukio ghalani hivyo kupunguza muda wa michakato na kuongeza ufanisi na usalama wa mzigo.

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) ni taasisi chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyoundwa kwa Sheria namba 10 ya 2005 na Marekebisho Kifungu 4 Sura 339 mwaka 2016 iliyopewa majukumu ikiwemo kutoa leseni kwa waendesha ghala, meneja dhamana na wakaguzi wa ghala.

Majukumu mengine ni kuchapa na kuidhinisha vitabu vya Stakabadhi za Ghala, kusajili na kuingiza taarifa za wadau muhimu wa mfumo, kuwakilisha nchi katika masuala ya taifa na kimataifa yahusuyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala pamoja na majukumu mengine kama taasisi itakavyoelekezwa na Waziri wa Viwanda na Biashara.

Wednesday, February 15, 2023

KAMATI ZA MAGONJWA YA MLIPUKO KUTOA ELIMU KWA JAMII

IMEELEZWA kuwa uanzishwaji wa kamati za magonjwa ya milipuko kutasaidia kuielimisha jamii kukabili magonjwa ili yasisambae kwa kasi na kutoleta athari.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alipokuwa akifungua mkutano wa kamati hiyo inayoundwa na wanajamii, wataalamu wa afya, viongozi wa dini na kamati ya usalama ya Wilaya.

John amesema kuwa kwa kuzingatia hilo itasaidia kukabili magonjwa ya mlipuko kwa kutoa elimu juu ya kukabiliana na magonjwa hayo.

Amezitaka kamati ya magonjwa ya milipuko kutoa elimu juu ya magonjwa kulingana na mila desturi na tamaduni za eneo husika.

Kwa upande wake Johnson Mndeme kutoka Wizara ya Afya Idara ya Kinga sehemu ya afya kwa Umma amesema kuwa malengo ya kuanzishwa kamati hizo ni kutoa elimu juu ya magonjwa ya mlipuko ili kuepukana na dhana potofu.

Kwa upande wake maganga mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha Peter Nsanya amesema kuwa wanakamati wanapaswa kutoa elimu ya kupambana na magonjwa mbalimbali ndani ya jamii.


TBA YAENDELEA NA MIPANGO YA UJENZI KWA NYUMBA WATUMISHI



Na Mwandishi Wetu Dodoma

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) wamefanikiwa kuendelea kutekeleza Malengo waliyojiwekea kwenye mpango mkakati wa mwaka 2021/22 hadi 2025/2026 pamoja na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuhakikisha utengenezaji wa makazi bora kwa watumishi.

Hayo yamebainishwa na katibu mkuu mtendaji (TBA) Daudi Kondoro wakati akizungumza na wandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu wa wakala huo katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita.

Kondoro amesema wakala wameendelea kutoa huduma ya uhakika ya makazi kwa serikali na kwa watumishi wa umma kwa kutoa huduma ya uhakika ya makazi na nyumba ambapo mpaka sasa kuna nyumba 1,622 zilizopangishwa kwa watumishi wa umma na pamoja na nyumba 7,700 zilizouzwa kwa watumishi wa umma Tanzania Bara Bara.

"TBA imetengeneza fursa za ajira na kutoa mafunzo kwa vitendo ambapo imetengeneza ajira takribani 100,000 kwa vijana walio na ujuzi na ambao hawana ujuzi kupitia miradi ambayo imekua ikitekelezwa,"alisema Kondoro.

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeishukuru serikali ya Rais Dkt. Samia kwa kukuendelea kuwawezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo kupewa fedha bilioni 54.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi.