VIWANJA VYA NDEGE VYAONGEZA HUDUMA ZA NDEGE NCHINI.
Thursday, November 3, 2022
HUDUMA ZA NDEGE ZAONGEZEKA NCHINI.
Sunday, October 30, 2022
JWT PWANI YAITA WAFANYABIASHARA KUJIUNGA NA JUMUIYA
WAFANYABIASHARA PWANI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA KWENYE JUMUIYA
Na John Gagarini
JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani imewataka wafanyabiashara kujiunga ili wanufaike na fursa mbalimbali zilizopo kwenye Jumuiya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekekezaji wa majukumu ya taasisi hiyo pamoja na fursa zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo katibu wa JWT Mkoa Wellu Mtaki amesema kwenye Jumuiya hiyo kuna fursa nyingi.
Mtaki amesema kuwa Jumuiya hiyo inamuwezesha mfanyabiashara kutatua changamoto zake na mfanyabiashara anauwezo wa kutoa kero maoni na mapendekezo yanayohusu biashara na taasisi ikafikisha sehemu husika kwa ajili ya utatuzi tofauti na mtu kupeleka kero yake mwenyewe.
"Lengo la Jumuiya ni kuwaunganisha kwa pamoja wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwawezesha kutoa mawazo na maoni yao kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa na kuziwasilisha serikalini,"amesema Mtaki
Amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na serikali katika kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara nchini Tanzania na moja ya huduma ni kuwaunganisha na bima za aina tofauti ambazo zimeanza kutolewa kwa wanachama.
"Huduma za bima zinazotolewa ni pamoja na bima ya Elimu au Carrier Life Plan kupitia shirika la bima la Jubilee ambalo linamsaidia mtoto wa mwanachama kunufaika kwenye elimu, bima ya Afya ambayo ina kifurushi cha aina tatu ambacho Scare individual and Family health insurance, pamoja Afya, Jubilee Afya na huduma ya bima ya nafaka," Amesema Mtaki.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara wote mkoani Pwani kuhakikisha wanafuata taratibu na miongozo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kepuka changamoto zitakazojitokeza.
Aidha amesema kuwa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania haijihusishi wala kufungamana na udini, ukabila, siasa, wala ushabiki wa michezo.
RAIS SAMIA KUZINDUA MATOKEO YA SENSA
RAIS SAMIA KUTANGAZA MATOKEO YA SENSA KESHO.
Na Wellu Mtaki, Dodoma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kutangaza matokeo ya Sensa ya watu na Makazi Oktoba 31 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hamza Juma ameyasema hayo Jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwenye kikao maalumu cha wajumbe wa kamati ya maandalizi ya uzinduzi wa tukio hilo.
Juma amesema kuwa maandalizi ya uzinduzi wa tukio la kutangazwa kwa matokeo ya sensa ya watu na anwani za makazi yamekamilika.
Ameeleza kuwa kazi kubwa ya kuratibu na kusimamia imefanywa na viongozi wa mkoa wa Dodoma na kilichobaki watakuwa wamekamilisha Oktoba 30.
Aidha amesema kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi la mwaka huu limefanyika kisasa zaidi tofauti na miaka ya nyuma na litaisaidia Serikali katika kupanga mipango yake ya kiuchumi,kijamii na maendeleo. Zoezi la sensa ya watu na makazi lilifanyika hivi karibuni.
Saturday, October 29, 2022
MATRILIONI YATENGWA MIRADI YA BARABARA NCHINI
TANROADS YATENGA TRILIONI 3.8 UTEKELEZAJI MIRADI YA BARABARA
UVCCM YAPONGEZA SHULE KUFUTA ZIRO
Na John Gagarini Kibaha
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Mkuza Wilaya ya Kibaha Mjini imetoa fedha na vyeti vya pongezi kwa walimu wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Nyumbu kwa kufanya vizuri kwenye baadhi ya masomo na kuondoa ziro kwenye shule hiyo.
Akizungumza kwenye mahafali ya 16 ya shule hiyo Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mkuza Hashim Kibonge alisema kuwa wameamua kuwapa motisha walimu ili waendelee kufanya vizuri ili kuongeza ufaulu shuleni hapo.
Kibonge alisema kuwa walimu hao wametekeleza vema ilani ya CCM juu ya masuala ya Elimu ikiwa ni moja ya vipaumbele vilivyopo kwenye ilani ya chama juu ya uboreshaji wa elimu.
"Tumetoa vyeti kwa walimu wa masomo ya Kiingereza, Baiolojia na Kiswahili walimu wote wamefanya vizuri lakini masomo haya tumeona tuwapongeze hawa lakini wote wamepambana kuleta mafanikio shuleni,"alisema Kibonge.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mkuza Matata Ngolo alisema kuwa wamekuwa wakiifuatilia shule hiyo na kuona jinsi inavyopambana kuhakikisha watoto wanapata elimu inayostahili.
Ngolo alisema shule hiyo licha ya kuwa na wanafunzi wengi lakini imeendelea kufanya vizuri kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambapo ufaulu kwa mwaka jana ilikuwa asilimia 99.
Naye Mgeni rasmi Naibu Kamishna wa Elimu Bahati Chikwindo alisema kuwa Wizara itasaidia shule hiyo kuhakikisha inakabili changamoto za shule hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala.
Chikwindo alisema kuwa watasaidia pia upatikanaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ili wanafunzi waweze kupata elimu hiyo ambayo ni muhimu kwa kipindi hichi cha utandawazi.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Juma Mrope alisema kuwa shule hiyo ndiyo shule inayoongoza kwenye Mkoa huo ambapo ina wanafunzi 2,136 huku wahitimu wa kidato cha nne walikuwa ni 460.
Mrope alisema kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni kutokuwa na jengo la utawala hali ambayo inasababisha watumie madarasa matatu hivyo kusababisha mlundikano wa wanafunzi kwani kuna upungufu wa madarasa unaofanya wanafunzi wasome kwa awamu mbili.
Akisoma risala ya wahitimu wa kidato cha nne Ahmed Kikoto alisema kuwa wanahitaji viti na meza zaidi ya 300, wanahitaji maktaba, ukarabati wa sakafu na kuomba kujengewa ukumbi.
Kikoto alisema kuwa wanawashukuru wadau mbalimbali kwa kuwapatia miradi mbalimbali ikiwemo wa Tehama na serikali kujenga shule shikizi ya Sofu ambapo imepunguziwa wanafunzi 75.
WATANZANIA WATAKIWA KULA NYAMA
DKT. MUSHI AMEWASISITIZA WATANZANIA KUJENGA UTAMADUNI WA KULA NYAMA
Na Wellu Mtaki, Dodoma
MSAJILI wa bodi ya nyama nchini Dkt Daniel Mushi amewasisitiza Watanzania kujenga utamaduni wa kula nyama ili kukabiliana na utapiamlo.
Aidha utafiti unaonyesha Mtanzania mmoja hula kilo 15 za nyama badala ya kilo 50 kama inavyotakiwa
Ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa habari maelezo .
Dkt Mushi amesema kwamba utafiti uliofanywa na bodi hiyo umebaini baadhi ya nchi za Ulaya na nyinginezo mtu mmoja anakula kilo hadi 100 kwa mwaka.
Amepinga kauli ya watu kuwa nyama nyekundu ni hatari bali mlaji anatakiwa kuandaa nyama vizuri kuanzia katika kuipika hadi kwenye ulaji.
Katika hatua nyingine ameeleza kuwa kwa sasa wana mipango thabiti ya kutafuta masoko ya uhakika kwani mahitaji ya nyama nje ya nchi ni makubwa lakini Tanzania inasafirisha nyama kwa kiwango kidogo.
MADAKTARI BINGWA KUSOMESHWA
WIZARA YA AFYA YAANDAA MPANGO WA KUSOMESHA MADAKTARI BINGWA NA WABOBEZI.
Na Wellu Mtaki, Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imetoa ufadhili wa shilingi bilioni nane kwa kuwasomesha madaktari bingwa na wabobezi ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari.
Waziri Ummy amesema mpango huo unaojulikana kama Samia Scholaship utasomesha madaktari ngazi za ubingwa 139 watasoma nje ya nchi na wengine 318 watasomea hapa nchini.
Mwalimu amesema kuwa mpango huo utakuwa ni kwa seti akitolea mfano daktari bingwa wa magonjwa ya figo atakwenda kusoma pamoja na muuguzi na mtaalamu wa dawa ya usingizi ambapo jumla watakuwa watatu katika ugonjwa mmoja.
Amefafanua kuwa katika mpango huo tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameikabidhi Wizara ya afya kiasi cha shilingi bilioni nane ambazo zitatumika kama ada na posho nyingine watakapokuwa mafunzoni.
Ameongeza kuwa Serikali imeamua kufanya hivyo baada ya kuona nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa huduma za kibingwa na ubobezi.