Na John Gagarini Kibaha
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Mkuza Wilaya ya Kibaha Mjini imetoa fedha na vyeti vya pongezi kwa walimu wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Nyumbu kwa kufanya vizuri kwenye baadhi ya masomo na kuondoa ziro kwenye shule hiyo.
Akizungumza kwenye mahafali ya 16 ya shule hiyo Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mkuza Hashim Kibonge alisema kuwa wameamua kuwapa motisha walimu ili waendelee kufanya vizuri ili kuongeza ufaulu shuleni hapo.
Kibonge alisema kuwa walimu hao wametekeleza vema ilani ya CCM juu ya masuala ya Elimu ikiwa ni moja ya vipaumbele vilivyopo kwenye ilani ya chama juu ya uboreshaji wa elimu.
"Tumetoa vyeti kwa walimu wa masomo ya Kiingereza, Baiolojia na Kiswahili walimu wote wamefanya vizuri lakini masomo haya tumeona tuwapongeze hawa lakini wote wamepambana kuleta mafanikio shuleni,"alisema Kibonge.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mkuza Matata Ngolo alisema kuwa wamekuwa wakiifuatilia shule hiyo na kuona jinsi inavyopambana kuhakikisha watoto wanapata elimu inayostahili.
Ngolo alisema shule hiyo licha ya kuwa na wanafunzi wengi lakini imeendelea kufanya vizuri kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambapo ufaulu kwa mwaka jana ilikuwa asilimia 99.
Naye Mgeni rasmi Naibu Kamishna wa Elimu Bahati Chikwindo alisema kuwa Wizara itasaidia shule hiyo kuhakikisha inakabili changamoto za shule hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala.
Chikwindo alisema kuwa watasaidia pia upatikanaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ili wanafunzi waweze kupata elimu hiyo ambayo ni muhimu kwa kipindi hichi cha utandawazi.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Juma Mrope alisema kuwa shule hiyo ndiyo shule inayoongoza kwenye Mkoa huo ambapo ina wanafunzi 2,136 huku wahitimu wa kidato cha nne walikuwa ni 460.
Mrope alisema kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni kutokuwa na jengo la utawala hali ambayo inasababisha watumie madarasa matatu hivyo kusababisha mlundikano wa wanafunzi kwani kuna upungufu wa madarasa unaofanya wanafunzi wasome kwa awamu mbili.
Akisoma risala ya wahitimu wa kidato cha nne Ahmed Kikoto alisema kuwa wanahitaji viti na meza zaidi ya 300, wanahitaji maktaba, ukarabati wa sakafu na kuomba kujengewa ukumbi.
Kikoto alisema kuwa wanawashukuru wadau mbalimbali kwa kuwapatia miradi mbalimbali ikiwemo wa Tehama na serikali kujenga shule shikizi ya Sofu ambapo imepunguziwa wanafunzi 75.
No comments:
Post a Comment