Thursday, October 27, 2022

HAZINA YAKUSANYA BILIONI 852.9

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina katika mwaka wa fedha 2021/22 imekusanya 852.9 sawa na asilimia 109.5 ya lengo kutoka katika kampuni ambazo serikali inamiliki hisa. Imesema ongezeko hilo linatokana na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ni zaidi ya kiasi kilichokusanywa Juni 30 mwaka jana ambacho ni sh. bilioni 638.87. Hayo yalibainishwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), Lightness Mauki, wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa ofisi hiyo katika mwaka huu wa fedha. Alisema fedha hizo zimekusanywa katika mapato yasiyo na kodi ambayo yanajumuisha gawio, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi na mapato mengineyo kutoka katika taasisi 287 zilizo chini ya ofisi ya msajiri. “Kuongezeka kwa makusanyo hayo kunatokana na kuimarisha usimamizi,ufuatiliaji na tathmini ya uwekezaji wa mitaji ya umma pamoja na hatua ambazo zilichukuliwa katika kukuza mapato na kudhibiti matumzi. Aliongeza kuwa:"Hadi kufikia Juni 30 mwaka huu Ofisi ya Msajili wa hazina ilikuwa inasimamia mashirika ya umma 287 Kati ya mashirika hayo 237 serikali ina hisa zaidi ya asilimia 51, taasisi 40 serikali inahisa chache na 10 za nje ya Nchi ambazo serikali imeweka uwekezaji. Lightness alisema serikali imewekeza kwenye mashirika hayo fedha sh.trilioni 70. Alisema kuwa serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea na juhudi za kusimamia utendaji wa kampuni ambazo serikali inaumiliki wa hisa chache. Pia, alisema serikali inafanya majadiliano na wabia wenza na kusimamia kwa ukaribu matumizi yasiyo ya lazima, hivyo kuchangia ongezeko la gawio. "Mathalani mafanikio ya jitihada hizo yamejidhihirisha katika utendaji wa Banki ya NBC ambayo imeongeza faida kabla ya kodi kutoka sh. bilioni 7 mwaka 2020 hadi sh. bilioni 60 mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 757, ukuaji huu wa faida umewezesha benki kutoa gawio kwa serikali sh. bilioni 4.5 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa,"alieleza. Akitaja mafaniko ya Ofisi hiyo Lightness alisema wameweza kufanya upanuzi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero ambacho serikali inamiliki asilimia 25 ya hisa. Alisema kutokana na kukua kwa mahitaji ya sukari nchini kulikuwa na uhitajio wa kupanua kiwanda cha sukari hicho ili kutimiza mahitaji. “Bodi ya wakurugenzi baada ya kufanya upembuzi yakinifu iliwasilisha mapendekezo ya kupanua kiwanda hicho ambapo sh. bilioni 571.6 zilitumika, uwekezaji huo unatarajia kuongeza kiwango cha uzalishaji sukari hadi kufikia tani 271,000 kutoka tani 127,000 za sasa,” alisema. .

No comments:

Post a Comment