Thursday, November 3, 2022

HUDUMA ZA NDEGE ZAONGEZEKA NCHINI.

VIWANJA VYA NDEGE VYAONGEZA HUDUMA ZA NDEGE NCHINI.


Na Wellu Mtaki, Dodoma

JUMLA ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika kipindi cha mwaka 2021/2022 ikilinganishwa na huduma iliyotolewa mwaka 2020/2021 sawa na ongezeko la asilimia 13. 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Huduma za Utabiri - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa Fedha 2022/23 katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO Novemba 2, 2022 Jijini Dodoma.

Dkt Kabelwa amesema kuwa sekta ya usafiri wa anga inaendelea kukua kutokana na kuzingatiwa kwa mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma na ongezeko hilo linatokana na jitihada za kuifungua nchi zinazofanywa na serikali, pamoja na kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa na kuihakikishia dunia usalama wa anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kwa ndege zote za kimataifa.

Amesema kuwa mamlaka hiyo katika mwaka 2021/22 iliendelea na utengenezaji wa rada mbili zitakazofungwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na cha Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 45.

Ameongeza kuwa Mamlaka imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa Wananchi kujenga utaratibu wa kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)yamegawanyika katika sehemu kuu tatu ambapo sehemu ya kwanza ni kutoa huduma za hali ya hewa; sehemu ya pili ni kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha (14) na sehemu ya tatu ni kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini Tanzania kulingana na Kifungu cha (5) cha Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019.

Mwisho

No comments:

Post a Comment