Friday, November 11, 2022

RC MADARASA YAKAMILIKE


MKUU WA MKOA ATAKA MADARASA YAKAMILIKE NOVEMBA 20

Na Wellu Mtaki, Dodoma

MKUU wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewataka wakuu wa shule zote waliokabidhiwa fedha za ujenzi wa madarasa katika mkoa wa Dodoma kukamilisha miradi hiyo ifikapo Novemba 20 mwaka huu.

Senyamule ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati wa ziara ya kutembelea baadhi ya shule kuona muendelezo wa hatua zilizofikiwa katika shule hizo huku akifafanua kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alitoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha watoto wanaokwenda kidato cha kwanza mwaka 2023 wasikose madarasa ya kusomea.

Amesema kuwa mkoa wa Dodoma ulipata shilling billion 6.7 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 339 ambapo fedha hizo zimegawanywa katika shule mbalimbali mkoani hapo.

Aidha amewataka walimu wa Shule ya Sekondari Zuzu kuongeza juhudi ya ufundishaji katika shule hiyo ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Zuzu Hezron Lupondo amesema kuwa shule yake ilipata shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa chumba kimoja cha darasa na ofisi huku akimuhakikishia Mkuu wa mkoa wa Dodoma kuwa watafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huo pamoja na kuongeza ufaulu katika shule hiyo.

Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Mnadani Claudian Kabuyombo amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Awamu ya sita kwa kuendelea kuimarisha sekta ya elimu.

No comments:

Post a Comment