Na Wellu Mtaki, Dodoma
WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) imesema imejipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu 17,000.
Aidha itatoa mafunzo ya utawala Bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt Siston Masanja akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/2023.
Dkt Masanja amesema katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 wakala hiyo imejipanga kudahili Walimu 2,343 katika kozi mbalimbali pamoja na kuandaa kitabu cha kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Dkt.Masanja amesema moja kati ya malengo ya Wakala hiyo ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa elimu bora shuleni kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ya elimu, kuziba ombwe la maarifa na ujuzi ambalo kiongozi au mtendaji hakupata katika mafunzo ya awali ya Ualimu na kuongeza idadi ya viongozi wenye maarifa ya uongozi na usimamizi wa elimu.
Kwa Upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa Serikali imeweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchini ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8.
Aidha, Msigwa ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu pamoja na wakuu wa shule kwenda kusoma ADEM.
Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM ulianzishwa Agosti 31, 2001 ukiwa na majukumu ya kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa elimu katika ngazi zote na kutoa ushauri wa kitaalamu katika mambo yanayohusu uongozi na usimamizi wa elimu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment